Waasi wa kundi la M23 wakimshikilia mtu anayeshukiwa
mwanachama wa kundi la FDLR.
SERIKALI ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC inasema kundi la waasi la M23 limeuwa watu 64 tangu lilipouteka mji wa Goma uliopo mashariki mwa nchi hiyo wiki iliyopita.
Shutuma hizo zilitolewa Jumatano na msemaji wa serikali, Lambert Mende, ambaye anasema zaidi ya raia 220 wamejeruhiwa huko Goma.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa kutoa msaada pia wanaripoti kutokea vifo katika mji huo lakini hawajasema ni nani anayehusika na vifo hivyo.
Mende pia alilishutumu kundi hilo la waasi kwa wizi wa ngawira huko Goma kabla ya kundi hilo kutangaza mipango ya kuondoka kwenye mji huo.
Mapema Jumatano mkuu wa jeshi la M23, Sultani Makenga alisema majeshi yake yalianza kuondoka kutoka Masisi, mji uliopo kilomita 50 kaskazini-magharibi mwa Goma na baadaye wataondoka Goma.
Shirika la habari la Reuters lilisema waasi wa M23 pia waliondoka Sake, mji mwingine katika eneo ambalo waliliteka. Mkuu wa kundi hilo Jean-Marie Runiga aliiambia Sauti ya Amerika-VOA siku ya Jumanne kwamba majeshi ya M23 yataondoka Goma ifikapo Ijumaa kama ishara ya nia njema.
Waasi hao wanasema watarudi nyuma kilomita 20 nje ya Goma lakini wataacha kiasi cha wanajeshi 100 kwenye uwanja wa ndege mjini humo.
0 comments:
Post a Comment