BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS MSTAAFU AWAMU YA TATU, BENJAMIN MKAPA AONYA.










RAIS mstaafu, Benjamini Mkapa amewataka Watanzania wakiwemo wasomi kuacha kulalamikia utandawazi na ubinafsishaji uliofanywa wakati wa utawala wake, badala yake wafanye kazi kwa bidii.

Rais Mkapa alitoa rai hiyo juzi, wakati akihutubia mahafali ya tatu ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana mkoani Dodoma.

Alisema kama Watanzania, wataendelea kulalamika nchi ambazo zinaunda Jumuiya ya Afrika Mashariki, zitatumia udhaifu huo kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

“Huu ni wakati wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, kama tutaendelea kulalamika kila kukicha, Tanzania itabaki nyuma katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lazima tuwe makini, Watanzania wafanye kazi waache kulalamika.

“Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki zipo changamoto nyingi, lazima tuwe makini, tufanye kazi kwa bidii kuendana na utandawazi, tukiendelea kulalamikia utandawazi na ubinafsishaji, wenzetu watatumia udhaifu huu kusonga mbele,” alisema Mkapa.

Mkapa aliwataka Watanzania kupiga vita ubaguzi wa aina yoyote ile, ili kuendeleza misingi mizuri iliyoachwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Katika chuo hiki, ingawa ni cha dini ya Kikristo, nilikuwa napitia majina ya wanafunzi wa dini zote wanasoma, nimeona ni wadini zote… hili ni jambo zuri.

“Hii inadhihirisha hakuna ubaguzi wa dini, tuendelee kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kupiga vita ubaguzi wa aina yoyote, tusikubali mtu atubague vyovyote vile,” alisema Mkapa.

Akizungumzia maendeleo ya chuo hicho, Mkapa aliupongeza uongozi na kusisitiza wakati wa utawala wake yeye ndiye aliyeidhinisha kuanzishwa kwa chuo hicho, kutoka Shule ya Sekondari ya Ufundi Mazengo.

“Hongereni sana kwa kuwa hadi sasa mmefanya mengi, zaidi ya matarajio yenu ya awali wakati mkiomba chuo hiki kiidhinishwe.

Aliwataka wanafunzi wa chuo hicho kuacha kutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii, badala yake watumie mitandao hiyo kutafuta vitabu vya kujisomea.

“Tumieni mitandao kupata vitabu mvitakavyo, uhaba wa vitabu au ukosefu wa maabara isiwe visingizio vya ninyi kutokufanya vizuri, mnaweza pia mkatumia mitandao ya simu zenu kujisomea,” alisema.

Alisema anafahamu changamoto za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ikiwemo ongezeko la wanafunzi lakini Serikali inalifanyia kazi tatizo hilo.

“Lakini inasikitisha kuona baadhi ya Watanzania wadanganyifu, ambao wanachukua mikopo wakati wanao uwezo, hivyo kusababisha watoto wa masikini kukosa mikopo, tatizo hili wahusika wanalifanyia kazi,” alisema.

Aliwataka wanafunzi waliohitimu kutumia elimu yao kuwa mabalozi wa chuo hicho, kwa kuwa nguvu na uwezo wanao na kilichobaki ni kujituma tu.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Gabriel Mwaluko alisema, jumla ya wanafunzi 2,020 walihitimu mafunzo yao.

Alisema idadi hiyo, imeongezeka ikilinganishwa na wanafunzi waliohitimu katika mahafali ya kwanza ambao walikuwa 700 tu, mwaka 2010 na mwaka 2011 walihitimu wanafunzi 1,003.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Chuo hicho, Askofu Donald Mtetemela aliwapongeza wahitimu wote na kuwataka kujivunia kuwa zao la Chuo Cha Mtakatifu Yohana.

“Mmejifunza kutumika, nendeni mkatumike, imani, uaminifu na ubora iwe muongozo wenu mnapoenda kufanya kazi, kuweni wakweli na waaminifu,” alisema.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: