
RAIS Barack Obama wa Marekani amesema nchi yake inaunga mkono hatua ya Israeli kujilinda yenyewe.
Matamshi hayo ameyatoa wakati wa mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa
Israeli, Benjamin Netanyahu yaliyofanyika kwa njia ya simu, kuhusu
mgogoro wa Gaza.
Rais Obama ameelezea pia masikitiko yake kutokana na
vifo vya raia wa Israeli na Palestina.
Ikulu ya Marekani imesema kuwa,
Netanyahu ambaye alimpigia simu Rais Obama, ametoa shukrani zake kwa
Rais Obama na kwa wananchi wa Marekani.
Viongozi hao pia wamejadiliana
kuhusu kuzuia mzozo huo kusambaa.
Obama azungumza pia na Morsi na Erdogan
Aidha, Rais Obama amempongeza Rais wa Misri, Mohamed Morsi kwa juhudi ya
kusaidia kuituliza hali kati ya Israeli na Gaza na kusisitiza matumaini
yake ya kurejea kwa utulivu kwenye eneo hilo.
Akizungumza na Morsi kwa
njia ya simu, Rais Obama ameelezea umuhimu wa kumaliza mashambuliano
haraka iwezekanavyo ili kuzuia maisha ya raia wasio ha hatia kupotea
bila sababu.
Waziri Mkuu wa Misri, Hisham Kandil amesema nchi yake ipo
tayari kupatanisha juu ya kusimamisha mashambiliano kati ya Israeli na
Hamas. Misri ni mshirika wa Hamas, lakini pia imetiliana saini mkataba
wa amani na Israeli mwaka 1979.
Rais wa Misri, Mohammed Morsi
Mbali na Netanyahu na Rais Morsi, Rais Obama amezungumza pia na Waziri
Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kwa njia ya simu ambapo kwa pamoja
wameelezea wasiwasi wao kuhusu hatari zinazowakabili raia wa pande zote
mbili na kuelezea nia yao ya kutaka kumaliza ghasia hizo.
Taarifa ya
Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Rais Obama na Erdogan pia wamesema
ghasia mpya katika Mashariki ya Kati zinahatarisha matarajio ya amani ya
kudumu katika eneo hilo.
Mapigano yaendelea
Mazungumzo hayo kwa njia ya simu yamefanyika, wakati wapiganaji wa Hamas
wakirusha maroketi kwenye miji ya Jerusalem na Tel Aviv jana Ijumaa.
Israeli imesema imezifunga barabara zote kuu kuzunguka mpaka wake na
Gaza, na kulielezea eneo hilo kama la kijeshi.
Hatua hiyo ni ishara
kwamba uvumilivu wa Israeli sasa umefikia kikomo na inajiandaa kuanzisha
mashambulizi ya kwanza ya askari wa miguu katika eneo hilo tangu mwaka
2008 na 2009.
Kiasi Wapalestina 21 na Waisraeli watatu wameuawa tangu
Israeli ilipoanzisha mashambulizi siku ya Jumatano, wakati ilipomuua
mkuu wa jeshi la Hamas, Ahmed al-Jabari.
Ban Ki-Moon azitolea wito Israeli na Hamas
Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon
amezitaka Israeli na Hamas kumaliza mashambulizi yanayoongezeka katika
Ukanda wa Gaza ili kuzuia mauaji zaidi katika Israeli na Palestina.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nersiky amesema Ban ana wasiwasi
mkubwa kuhusu kuendelea kwa ghasia kati ya Gaza na Israeli na anahofia
pia kupanda kwa gharama za maisha ya raia.
Nersiky amesema Ban
anatarajiwa kuzuru eneo hilo hivi karibuni.
Wanadiplomasia wa Umoja wa
Mataifa wamesema kuwa Ban atazuru Israeli na Misri wiki ijayo.

0 comments:
Post a Comment