BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SIMBA SPORT CLUB YAENDELEZA KUGAWA POINTI, YAPOKEA KIPIGO CHA BAO 1-0 KUTOKA KWA TOTO AFRIKA.UTWA BAO


Wachezaji wa Toto Afrika wakiwa wamebeba kocha wao, Athumani Bilal kwa furaha ya ushindi baada ya kuitandika Simba SC katika mchezo wa ligi kuu ya vodacom Tanzania bara kwa bao 1-0 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Picha kwa hisani ya Ben Zuber.blog.

 MGAMBO Shooting na Toto African zilifanya kile kisichotegemewa na wengi baada ya kuzinyuka Azam na Simba jana katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, huku vinara Yanga leo wakishuka kwenye Uwanja wa Mkwakwani kuivaa Coastal Union.

Azam ambayo imewasimamisha mabeki wake watatu tegemeo, nahodha Aggrey Morris, Said Morad, Erasto Nyoni pamoja kipa Deogratius Munishi walikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Pia jahazi la mabingwa watetezi, Simba limeendelea kuzama baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Toto African kikiwa ni kipigo chao cha kwanza kupata kwenye Uwanja wa Taifa msimu huu.

Mkwakwani; Wenyeji Mgambo Shooting walianza mchezo wao kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza katika dakika ya 13, kupitia kwa Issa Kandulu aliyetumia vizuri uzembe wa mabeki wa Azam wakidhani ameotea alipoitokea krosi ya Full Maganga na kumchambua kipa Mwadini Ally.

Azam walisawazisha bao hilo katika dakika 29 mfungaji akiwa mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Tchetche aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya pacha wake Michael Bolou.

Mgambo walipata bao la pili katika dakika ya 78 mfungaji akiwa Nasoro Gumbo aliyeunganisha vizuri pasi ya Kandulu na kuiacha Azam iliyosimamisha mabeki wake watatu isijue la kufanya.

Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika, kocha wa Azam, Stewart Hall alisema kipigo hicho hakikutokana na kufungiwa kwa wachezaji wake.

"Kufungwa ni kawaida kwenye mchezo na lazima tusimamie nidhamu kwenye timu yetu, tumefungwa kimchezo siyo kingine," alisema Hall.

Dar es Salaam; Wachezaji wa Toto African sasa wanasubiri kukabidhiwa ahadi ya kupewa Sh500,000, baada ya kuichapa Simba bao 1-0.

Mchezaji Mussa Said aliifungia Toto bao pekee katika dakika ya 73 akiunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Mohamed Jingo.

Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic alisema matokeo hayo yanatokana na kufungiwa kwa wachezaji wake nyota kama Haruna Moshi na Juma Nyoso.

"Viongozi wa Simba hawakunishirikisha kwenye uamuzi wa kuwafungia Moshi na Nyoso, nadhani wanabidi wafikirie upya juu ya uamuzi wao," alisema Milovan.

Katika mchezo huo kipa wa Toto, Erick Ngwengwe alikuwa kikwazo kikubwa kwa safu ya ushambuliaji ya Simba iliyoonekana kukosa mbinu za kumfunga kabisa.

Washambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, Felix Sunzu na Mrisho Ngasa mara kadhaa walipoteza nafasi za kufunga wakiwa wao na kipa huyo.

Toto African waliokuwa wameahidiwa Sh500,000 kama wataifunga Simba walionekana kucheza kwa malengo na kufanya mashambulizi ya kushtukiza kupitia Musa Said aliyekuwa mwiba kwa ngome ya Simba.

Chamazi; Mabingwa wa Ligi Kuu mwaka 1999, 2000, Mtibwa Sugar walilazimika kusawazisha kabla ya kuichapa African Lyon mabao 3-1.

Mshambuliaji Abdulghan Gulam aliifungia African Lyon bao la kuongoza katika dakika ya 22 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Jackson Kanywa.

Mtibwa Sugar waliamka na kusawazisha bao hilo katika dakika ya 32 kupitia Shabani Nditi akimalizia pasi ya kinda Hassan Ramadhani, ambapo dakika tatu kabla ya mapumziko Ally Mohamed alifunga bao la pili kwa Mtibwa akimalizia pasi ya Hussein Javu.

Kama hiyo haitoshi, mshambuliaji Javu alifunga bao la tatu kwa Mtibwa akiunganisha vizuri krosi ya Ally Mohamed katika dakika ya 90.

Mbeya; Wenyeji Tanzania Prisons walilazimishwa sare ya 1-1 na JKT Ruvu. Katika mechi hiyo, mshambuliaji Misango Magae alifunga bao la kuongoza katika dakika ya 10, lakini Jimmy Shoji aliisawazishia JKT Ruvu kwa shuti kali lililochana nyavu katika dakika ya 87.

Arusha; Timu ya Ruvu Shooting ilipata ushindi wao kupitia Seif Rashid aliyefunga mabao mawili na Michael Pius moja, huku Amiry Omary na Edmund Kashamika wakifunga mabao mawili ya JKT Oljoro iliyolala kwa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.

Kagera; Kwa upande wa Kagera Sugar wenyewe walilazimishwa sare ya 0-0 na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Wakati huohuo, Yanga itamkosa kiungo wake Athuman Idd 'Chuji' anayetumikia adhabu ya kadi tatu za njano wakati itakapoivaa Coastal Union leo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kocha Ernest Brandts anatarajia kumtumia Mbuyu Twite kuziba pengo hilo.

Twite alikuwa nje ya mazoezi kwa siku mbili kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa malaria, lakini sasa amepona
na anatarajiwa kucheza mchezo huo.

Daktari wa Yanga, Juma Sufian alisema Mbuyu amepona kabisa na hawana mchezaji yeyote mgonjwa kwenye kikosi hicho kwa sasa.

Akizungumzia mchezo huo, kocha Brandts ambaye anapenda kutumia mfumo wa 4-3-3 alisema mechi itakuwa ngumu, lakini anaamini watashinda.

"Tumejiandaa vizuri kuona tunashinda mechi yetu ya leo na hakuna tatizo katika kikosi chetu,"alisema Brandts.

Naye kocha wa Coastal Union, Hemed Morocco alisema itakuwa mechi yenye upinzani mkubwa, lakini watatumia uwezo wao kuhakikisha wanashinda.

''Mimi naichukulia mechi hii kama ile ya Polisi tuliyocheza juzi na tukashinda kwani kuongoza ligi siyo tija hata sisi tunaweza kuongoza,'' alisema Morocco.

Imeandaliwa na Kalunde Jamal, Clara Alphonce (Dar) Burhan Yakub na Doris Maliyaga(Tanga), William Paul (Kagera) Jackson Odoyo (Arusha), Geofrey Kahango (Mbeya).
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: