KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezitaka nchi wanachama
wa umoja huo kuongeza jitihada za kutokomeza maambukizi ya virusi vya
Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto huku zikihakikisha kuwa wanawake
wazazi wenye virusi vya Ukimwi wanaishi na afya zao zinastawi.
Bwana Ban amesema hayo katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya
Ukimwi duniani hii leo ambapo ujumbe maalum ni kutokomeza kabisa
maambukizi mapya ya ukimwi, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na Ukimwi.
Amesema kuongeza juhudi za kupunguza maambukizi kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto ni muhimu kwa kuwa asilimia 50 ya mafanikio ya
kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa miaka miwili
iliyopita yamepatikana miongoni mwa watoto wachanga.
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema lengo la milenia kuhusu
Ukimwi liko bayana ambalo ni kutokomeza Ukimwi na kubadili mwelekeo wa
maambukizi ifikapo mwaka 2015 na kupongeza kuwa kutokana na juhudi za
serikali na taasisi za kiraia kuna mwelekeo wa kutimiza lengo hilo.
Amegusia unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na
kutaka serikali kuondoa hali hiyo ambayo inaongeza hatari zaidi kwa watu
walioko hatarini kuambukizwa virusi vya ukimwi.
Ripoti ya mwaka huu ya Ukimwi iliyotolewa na shirika la Umoja wa
Mataifa la kupambana na ukimwi, UNAIDS, inaonyesha kupungua kwa kiasi
kikubwa kwa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi hususan katika nchi za
vipato vya kati na chini.
0 comments:
Post a Comment