TAKRIBAN miaka 10 sasa tangu mwaka 2002 hadi mwaka huu 2012, Tanzania imekuwa ikishuhudia nyota wake katika tasnia mbalimbali wakipoteza maisha wakati nyota zao bado ziking’ara.
Vifo vya nyota hao licha ya kuacha mapengo yasiyozibika, bado vimeendelea kugonga vichwa vya watu, vikiacha maswali na pengine yatima katika familia zao.
Katika makala haya mwandishi wetu amejaribu kuainisha baadhi ya wasanii wa fani tofauti, waliofariki kipindi ambacho nyota zao ziking’ara na kupendwa na mashabiki.
SHARO MILONEA.
Namna ya uigizaji wake katika hali ya kitanashati na mikogo ya kipekee inayoendana na lugha ya ‘kisharobaro’, ilimfanya msanii huyo kupoteza jina lake halisi ambalo ni Husseni Ramadhani Mkieti.
Ilikuwa vigumu kumsaka msanii huyo kwa jina lake halisi, lakini ilikuwa ni rahisi kumpata iwapo ungemtafuta kwa jina la Sharo Milionea.
Msani huyo alibadilisha jina lake la awali na Sharobaro na kuwa Sharo Milionea, baada ya kuingia mzozo na msanii mwenzake, Bob Junior ambapo kwa kuepusha wasikosane, aliamua kutumia jina hilo jipya lililokolea na kumvaa kuliko maelezo.
Katika mahojiano mbali mbali Sharo Milionea aliwahi kunukuliwa akisema kuwa alipenda kuigiza kama brazameni akitumia maneno kama 'usinichafue meen', 'nimechoka kuimba meen' kamata 'mwizi meen' ili kujitofautisha na wasanii wengine nchini, akiiga staili ya msanii aliyekuwa akimhusudu, Will Smith.
Sharo Milionea, aliyekuwa mahiri kwa kuigiza filamu na uimbaji wa muziki wa kizazi kipya, alikiri kwamba karibu kila jambo katika sanaa yake, ina chembe ya nyota huyo wa Kimarekani anayetamba kwenye muziki na filamu ulimwenguni.
Mkali huyo aliyewahi kutamba na nyimbo kama 'Nahesabu Namba','Tusigombane', 'Chuki Bure', 'Hawataki', 'Sondela', 'Tembea Kisharobaro' ambaye pia alikuwa mbioni kuachia nyimbo nyingine za 'Vululuvululu' na 'Changanyachanganya', amefariki Jumatatu ya Novemba 26 saa mbili usiku maeneo ya Maguzoni Muheza mkoani Tanga kwa ajali ya gari akitokea Dar es Salaam.
AMINA CHIFUPA
Nyota huyu alizaliwa Mei 20 mwaka 1981 na kufariki Juni 26 Juni, 2007 baada ya kuugua. Kifo chake kilitokea siku chache kabla ya kikao cha Bunge la Bajeti, akiwa mbunge.
Chifupa alipata umaarufu wa kuwa Mbunge kijana mwenye umri mdogo ambapo alitikisa kwa kula kiapo mbele ya Bunge katika harakati za kuwamata wauza na watumiaji wa madawa ya kulevya.
Ndani ya miezi 18 alishikilia bango msemo wake wa kutetea vijana, kupunguza rushwa na pia elimu kwa watu wote.
Kabla ya hapo alikuwa ni mtangazaji maarufu wa redio ya Clouds FM.
JAMES DANDU.
Maarufu kama 'Cool James', Mtoto wa Dandu Mwanamuziki aliyezaliwa 1970 katika Jiji la Mwanza.
Alianza shughuli za muziki mwaka 1983, lakini album yake ya kwanza aliitoa 1986. Alijiunga na mwanamuziki Andrew Muturi kutoka Kenya na kuanzisha kundi la Swahili Nation ambapo walifanikiwa kutoa single iliyoitwa Mapenzi.
0 comments:
Post a Comment