KWA UFUPI:
Magufuli alikataa kuipokea barabara hiyo kutoka katika Serikali ya Japan, iliyotoa msaada wa fedha na ujenzi kufanywa na Kampuni ya Kajima, baada ya kujiridhisha kuwa ilijengwa chini ya kiwango.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
UJENZI wa Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam ambayo Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alikataa kuipokea mwaka 2011, baada ya kujengwa chini ya kiwango, umekamilika.
Ujenzi wa kipande hicho cha kilomita 5.1 kutoka Mtongani hadi Mbagala Rangi Tatu, ulikamilika jana baada ya magari kuruhusiwa kutumia barabara bila vikwazo vilivyokuwapo wakati wa ujenzi.
Mafundi wa Kampuni ya Kajima waliokuwa wakijenga kipande hicho cha barabara, jana walionekana wakiwa katika hatua za mwisho za kusawazisha udongo katikati ya barabara hiyo yenye njia nne.
Msongamano wa magari ulikuwa ukiwasababishia usumbufu watumiaji wa barabara hiyo inayounganisha Dar es Salaam na mikoa ya Lindi na Mtwara, sasa umekwisha.
Magufuli alikataa kuipokea barabara hiyo kutoka katika Serikali ya Japan, iliyotoa msaada wa fedha na ujenzi kufanywa na Kampuni ya Kajima, baada ya kujiridhisha kuwa ilijengwa chini ya kiwango.
Magufuli alimweleza Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada kwamba asingeipokea barabara iliyo chini ya kiwango hata kama imetolewa kama msaada kwa Tanzania.
Baada ya msimamo huo wa Serikali, Japan ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa kampuni hiyo ilijenga barabara hiyo chini ya kiwango.
Kutokana na hali hiyo, Balozi Okada aliahidi kurudia ujenzi wa kilometa 5.1 kipande ambacho waligundua kuwa kampuni hiyo ilijenga chini ya kiwango.
Kazi ya ujenzi huo ilianza Juni mwaka huu.
Baada ya kauli hiyo ya Balozi, Dk Magufuli alimtaka mkandarasi huyo kuondoa tabaka la lami na kuweka tabaka jingine gumu lenye sentimita saba jambo ambalo limetekelezwa baada ya marudio.
Ujenzi wa Barabara ya Kilwa yenye urefu wa kilomita 13.5 kutoka bandarini hadi Mbagala Rangitatu ulizinduliwa kwa kuwekwa jiwe la msingi na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2007.
0 comments:
Post a Comment