WAZIRI KUU MSTAAFU AWAMU YA TATU EDWARD LOWASSA.
WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, jana alifanya maajabu kanisani, baada ya kuendesha harambee na kuchangisha zaidi ya Sh milioni 100 papo hapo.
Lowassa alichangisha fedha hizo wakati wa ibada ya Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Msasani, jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kuchangisha kiasi hicho cha fedha, kanisa hilo lilikuwa limelenga kuchangisha Sh milioni 100.
Pamoja naye, Lowassa alikuwa na mkewe, Regina ambapo alichanga Sh milioni 10.
Pia alikuwa na familia yake ambayo nayo ilichanga fedha kwa viwango tofauti.
Miongoni mwao ni Robert Francis aliyechanga Sh 500,000, Sioi Sumari ambaye ni mkwewe, alichanga Sh milioni 1.5, Noel Severe ambaye ni rafiki wa familia hiyo, alichanga Sh 750,000 na Fred Lowassa aliyewakilishwa na mkewe, alichanga Sh milioni 2.
Harambee hiyo ilifanyika maalum kwa ajili ya kuchangisha fedha za kununulia basi la Kwaya ya Ukombozi, pamoja na kuzindua DVD ya kwaya hiyo.
Akizungumza wakati wa harambee hiyo, Lowassa, aliyataka makanisa nchini, kuwasaidia vijana kupata mashamba, ili kukabiliana na tatizo la ajira.
Alisema kwamba, kama makanisa yataamua kuanzisha mashamba, yatakuwa yamesaidia kwa kiasi kikubwa juhudi za Serikali za kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana nchini.
Kauli hiyo ya Lowassa ni mwendelezo wa kauli yake juu ya tatizo la ajira kwa vijana na mara kadhaa amekuwa akilifananisha na bomu linalosubiri kulipuka.
Mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumza na timu za mpira wa miguu na mikono za Bunge la Tanzania, nyumbani kwake Monduli Arusha, Lowassa aliwataka wabunge hao kuwa chanzo cha kuundwa kwa sheria ya kuwapo kwa shule za michezo nchini.
Alisema kwamba, kama shule hizo zitaanzishwa, zitawafanya vijana wawe wanamichezo mahiri na kuweza kupata ajira katika sekta hiyo, kama ilivyo katika nchi nyingine duniani.
Katika mazungumzo yake kanisani hapo jana, alisema wakati umefika kwa makanisa nchini kushiriki katika harakati hizo kama yanavyofanya katika sekta ya elimu, afya na nyinginezo ili kupunguza tatizo la ajira.
"Nayaomba makanisa nchini, yasaidie kuwatafutia vijana mashamba na kujiingiza katika shughuli za kilimo.
“Sekta ya kilimo ambayo kwa sasa inapewa msukumo mkubwa na Serikali kupitia mpango wake wa Kilimo Kwanza, inaweza kutatua kwa kiasi kikubwa tatizo la ajira kwa vijana.
"Kilimo kinaweza kabisa kutatua tatizo hili la ajira, ni jukumu letu kuwasaidia vijana kuweza kujiingiza katika sekta hii na makanisa ni moja ya taasisi zinazoweza kutoa msaada mkubwa, kuwawezesha vijana kupata mashamba,'' alisema Lowassa.
Naye Mchungaji wa Usharika huo, Eliguard Muro, alimshukuru Lowassa kwa mchango wake katika jamii pamoja na kushiriki katika harambee mbalimbali za kikanisa.
Awali, katika risala iliyosomwa na Mwenyekiti wa kwaya hiyo, Erick Mchome, wanakwaya hao walisema Ukombozi ni miongoni mwa kwaya sita zilizomo katika usharika huo, ambazo zimekuwa na wajibu wa kuhubiri injili vijijini, sambamba na kusaidia watu mbalimbali kadiri inavyowezekana.
“Tumemuomba Mungu sana katika huduma hizi, kwani watu wengi wamejitoa na kumpa Yesu Kristo maisha yao na hata wengine wameweza kubadili dini lakini pia tumefanikiwa kuanzisha mitaa kama vile Kirinyaga, Mkoa wa Kati nchini Kenya ambako kuna kanisa lilitokana na kwaya yao.
“Katika kwaya yetu tulikuwa na mkakati mzito ambao ulikuwa ni kukusanya Sh milioni 100, ili ziweze kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo ya kwaya ikiwa ni pamoja na ununuzi wa basi la kusaidia shughuli za kwaya.
“Kutokana na ziara zetu tunazozifanya sehemu mbalimbali nchini, tulifanikiwa kutembelea Misheni ya Vigwaza mkoani Pwani, ambako pamoja na kuendesha mikutano ya injili, pia tuliguswa na hali ngumu ya maisha walionayo wakazi wa eneo lile.
“Pamoja na ugumu wa maisha walionao, pia wakazi wale hawana huduma muhimu kama maji safi, zahanati na huduma nyingine.
Kwa hiyo, tumeamua kulichagua eneo lile kama eneo maalum ambapo tutakuwa tukienda kutoa huduma ya neno la Mungu na mahitaji mengine ya kibinadamu,” alisema Mchome.
CHANZA GAZETI LA MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment