KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa ametakiwa kutokanyaga mkoani
Mbeya kuanzia sasa hadi ifikapo mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu.
Kauli hiyo imetolewa juzi mjini hapa na kundi kubwa la wanachama na
wapenzi wa CHADEMA mara baada ya kumalizika kwa mkutano mkubwa ambao
umevunja rekodi ya mikutano iliyowahi kufanyika kwenye viwanja vya
Luanda-Nzovwe, maarufu Uwanja wa Dk. Slaa.
Wamedai kwamba hakuna haja kwa Slaa kwenda mkoani humo kwa ajili ya
mikutano ya kuhamasisha, badala yake wamemtaka atulie na kuanza
maandalizi kabambe ya timu ya uchaguzi mkuu ujao.
Bila kutaja majina yao, wengi wa wanachama hao wamesema kumruhusu Dk.
Slaa kuzunguka mikoani katika operesheni ya M4C ni kumchosha bure kwa
kile walichodai anahitaji kukusanya nguvu katika mapambano makubwa ya
safari ya kuelekea kushika hatamu za nchi 2015.
“Tunamtaka Dk. Slaa mwaka 2015. CCM wanasema eti kazeeka, sisi vijana tunamtaka Dk. Slaa na uzee wake.
“Nchi hii lazima iendeshwe na wazee wenye akili, hekima na busara,
wazee wenye kujua uchungu wa watu wanyonge kama mzee wetu awaonyeshe CCM
jinsi nchi ya wapigania haki inavyopaswa kuongozwa,” walisema vijana
hao waliojitambulisha kwa majina ya Saleh Issa, John Paul na mmoja
aliyejitaja kwa jina la Mussa.
Katika mkutano huo ambao ulihutubiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama
hicho, Freeman Mbowe, ulishuhudia baadhi ya wanachama wa CCM wakichangia
harambee ya papo kwa papo ambapo kiasi cha sh milioni 3.2 zilipatikana.
Baadhi ya askari polisi walioshiriki kulinda mkutano huo, wamekiri
kuwa ulitawaliwa na utulivu wa hali ya juu tofauti na ilivyokuwa
ikihisiwa na walinzi hao wa amani.
Mkutano huo wa juzi ulimalizika kwa chama hicho kusimika uongozi imara
wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini chini ya mratibu wake, Frank James
Mwaisumbe, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, aliyekuwa kada wa
CCM ambaye amejiunga na CHADEMA, Mwaisumbe aliangushwa katika kura za
maoni mwaka 2010 alipogombea ubunge jimbo la Mbeya mjini kwa tiketi ya
CCM.
Licha ya kuwepo kwa mafanikio makubwa katika mkutano huo, baadhi ya
wapenzi na wanachama wa chama hicho walielezea kukerwa na nguvu za ziada
zinazoonyeshwa na vijana wa ulinzi wa chama hicho, Red Brigedi, na
kushauri wapewe mafunzo ya amani na uvumilivu ili kukisimamia vyema
chama hicho.
Tanzaniadaima
0 comments:
Post a Comment