KADINALI Peter Turkson wa Ghana
hawanii upapa, lakini ni dhahiri ana wanaomwunga mkono ambao wanaamini anatosha
na wamebandika mabango yenye picha yake sehemu mbalimbali za jiji hili.
“Chagua Peter Kodwo Appiah
Turkson kwenye Baraza la Makadinali!,” imeandikwa kwa herufi nzito katika
mabango juu ya picha ya Kadinali huyo, ambaye ni maarufu miongoni mwa
makadinali wanaofikiriwa kumrithi Benedict, ambaye Alhamisi alikuwa papa wa
kwanza baada ya karne sita, kujiuzulu.
Mabango hayo yamebandikwa katika
mbao ambazo zilitumiwa na wagombea wa uongozi nchini mapema wiki hii.
Tofauti na uchaguzi wa Bunge,
wagombea wa upapa kwa kawaida hawatakiwi kuzindua kampeni, hali inayoonesha
kuwa mabango hayo yanatoka kwa wafuasi wa Turkson au yawezekana yanabandikwa na
wafanya mzaha.
Makadinali wanatarajia kukutana
faragha katika kanisa dogo la Sistine kwa siku 10, mkutano ambao chaguo lao
litakuwa limebarikiwa na Roho Mtakatifu na si siasa za kidunia.
Turkson anaweza kuwa mtu wa
kwanza asiyetoka Ulaya kuongoza Kanisa Katoliki baada ya kipindi cha zaidi ya
miaka 1,000 kupita kama atachaguliwa.
Lakini usemi wa zamani wa Kiroma
unaonya dhidi ya kukampeni, hata kama ni kwa siri, ili mtu kuwa papa au hata
kujaribu kubashiri matokeo ya Baraza la Makadinali.
Unasema: “Anayeingia kwenye
Baraza kama papa, anatoka kama kadinali”.
Wakati hayo yakiendelea, Papa mstaafu
alikuwa akiendelea kusoma ujumbe kutoka kwa wanaomtakia heri huku akivinjari
katika bustani za kasri lake.
Papa huyo wa zamani mwenye umri
wa miaka 85 alikuwa pia akiangalia televisheni ikirusha matangazo ya kuondoka
kwake Vatican Alhamisi jioni, na kulala fofofo katika makazi yake hayo ya upapa
katika kasri la Gandolfo, ambako atakaa kwa miezi miwili, msemaji wa Vatican
alisema jana.
“Alilala vizuri. Hali ya hewa
ilikuwa mwanana yenye utulivu,” Padri Federico Lombardi aliwaambia waandishi wa
habari, akikariri alichoambiwa na Katibu Myeka wa papa mstaafu, Askofu Mkuu
Georg Gaenswein kupitia simu kutoka makazi hayo yaliyoko Kusini mwa Roma.
Benedict alichukua CD zake za
muziki anaoupenda sana na vitabu vingi vya Theolojia, Historia na Falsafa,
Lombardi alisema na kuongeza kuwa hivi karibuni ataanza kupiga kinanda chake
usiku.
Kuhusu lini Baraza la kumchagua
Papa mpya litaanza, makadinali ndio watakaoamua, lakini hilo halitafanyika
mpaka idadi ya makadinali 115 kutoka sehemu mbalimbali duniani watakapokuwa
wamewasili.
Haijulikani ni wangapi mpaka jana
walikuwa wamewasili.
Hakuna kilichokuwa
kimeshaandaliwa hadi jana, lakini Vatican inaonekana kujipanga kwa uchaguzi
ifikapo katikati ya mwezi huu, hivyo Papa mpya anaweza kusimikwa kabla ya
Jumapili ya Matawi Machi 24 na hivyo kuongoza Wiki Takatifu kujiandaa na
Pasaka.
0 comments:
Post a Comment