MIKAKATI KUZIMA SAKATA LAKE YAFICHUKA.
http://www.freemedia.co.tzhttp:
Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited, Absalom Kibanda, akiwa ndani ya Ndege ya Flightlink.
HATUA ya vyombo vya habari kulivalia njuga suala la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda haiwafurahishi watendaji wa serikali.
Vyombo kadhaa vya habari yakiwemo magazeti, vimekuwa na habari, makala na maoni mfululizo kuisukuma serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi iwasake na kuwafikisha mahakamani wahusika wa tukio la Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006).
Katika habari hizo, vyombo hivyo vinaeleza kushangazwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kushughulikia matukio mepesi haraka na kwa kutumia nguvu nyingi, huku sakata la Kibanda na lile la Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka uchunguzi wake ukidorora.
Msukumo huo wa vyombo vya habari kuvisakama vyombo vya dola na baadhi ya vigogo serikali kuhusika na matukio hayo umepokelewa kwa mtazamo hasi.
Habari za uhakika zinasema kuwa vigogo kadhaa wameanza kuhaha kupanga mikakati ya kuvizima vyombo hivyo, hususani magazeti ya Tanzania Daima na Mtanzania ambayo yamekuwa mstari wa mbele kuandika sakata hilo.
Katika mkakati huo, tayari gazeti la Mtanzania limeandikiwa barua na Msajili wa Magazeti ambapo Kaimu Mhariri wake anatakiwa kwenda kujieleza Idara ya Habari (Maelezo) kuhusu habari iliyochapishwa Machi 20, mwaka huu.
Akithibitisha kupokea wito huo, Mhariri wa Mtanzania, Kulwa Karedia, alisema barua hiyo ina kumb. Na. IR/RN/336/57 ya Machi 21 mwaka huu, na imesainiwa na Jamal Zuberi kwa niaba ya Msajili wa Magazeti.
Alisema kuwa Kaimu Mhariri wao anajulishwa, “Madhumuni ya wito huo ni kujadili habari iliyochapishwa na gazeti lako toleo Na.7262 yenye kichwa cha Urais wa damu.”
Karedia alisema kuwa habari husika iliyoandikwa na Mtanzania ilielezea kuwa sakata la kushambuliwa kwa Kibanda limeanza kuibua tetesi na kutaka Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ahojiwe kutokana na kauli yake.
Membe alihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV Julai mwaka jana, katika kipindi cha Dakika 45 na kudai kuwa anao maadui 11 wakiwemo waandishi wa habari wawili ambao atawatwanga kweupe.
Hatua ya kutaka Membe ahojiwe ni kutokana na Kibanda kuumizwa ikiwa ni takribani miezi tisa tangu kauli hiyo itolewe bila kufafanua maadui zake aliwakusudia akina nani.
Hata hivyo gazeti hili lilidokezwa kuwa baadhi ya vigogo waandamizi wa serikali, CCM na maofisa kadhaa wa Usalama wa Taifa wamekuwa na vikao vya kujadili namna ya kunyamazisha magazeti hayo.
Lengo la mkakati huo ni kuhamisha mjadala ili wananchi wahangaike na mambo mengine wasahau sakata la kuteswa kwa Kibanda.
Miongoni mwa wanaohaha katika suala hili ni waziri mmoja machachari ambaye anatajwa kuusaka urais kwa nguvu akishirikiana na kigogo mwingine wa CCM.
Inadaiwa kuwa kumekuwa na vikao vya mfululizo ambapo vya mara ya mwisho vimefanyika juzi kwa siku mbili ofisini na nyumbani kwa waziri huyo jijini Dar es Salaam kujadili mkakati wao.
Miongoni mwa walioshiriki vikao hivyo yumo pia kigogo mmoja wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Baadhi ya mambo waliyojadili ni kuyafungia baadhi ya magazeti, hasa Tanzania Daima na Mtanzania, ambayo wamesema yanafuatilia na kuripoti sana habari za masaibu yaliyompata Kibanda.
Hata hivyo, baada ya mjadala mrefu walikubaliana kwamba ni rahisi kuanza na Mtanzania kwa sababu za kimkakati na kisiasa.
Kwa sababu zao za kimkakati walikubaliana kuanza na Mtanzania na kuliacha Tanzania Daima ambalo linamilikiwa na kiongozi wa upinzani.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kujiridhisha kwamba mchakato wa kuvishitaki vyombo hivyo unaweza kuchukua muda mrefu na kuibua masuala mengine wasiyotaka jamii iyajue.
Vigogo hao walienda mbali zaidi wakimhusisha Ofisa Mkuu Mtendaji wa New Habari (2006), Hussein Bashe wakidai amekuwa akitumia magazeti ya Rai na Mtanzania kuelekeza yaandike masuala yanayochafua serikali, waziri mmoja na kundi lake na makundi kadhaa ndani ya CCM.
Ingawa suala la uraia wa Bashe lilishamalizika kwa Idara ya Uhamiaji kuuthibitisha, mipango ya kundi hili sasa imejielekeza katika kuibua upya suala hilo kisiasa ndani ya chama kwa kumtumia kijana machachari na bingwa wa propaganda ambaye ana wadhifa mkubwa ndani ya chama.
Taarifa zinasema suala hilo litaibuliwa ndani ya vikao vikuu vya chama vijavyo ili CCM iendelee kusisitiza haitambui uraia wake na iweke shinikizo afukuzwe uanachama.
Vile vile waliweka mkakati kuwa shinikizo hilo litapelekwa hadi kwa mwajiri wa Bashe, Rostam Aziz ili amwondoe kwenye cheo hicho au amfukuze kazi kwa sababu magazeti yake yamekuwa hayatimizi malengo asilia yaliyomsukuma kuyanunua.
Bashe ashangaa
Alipotafutwa Bashe jana kueleza kama ana taarifa za mikakati ya kikao hicho, alijibu kwa kifupi; “Sijazipata taarifa hizo ila nitazifanyia kazi.”
Bashe alikiri kupokea barua ya Msajili wa Magazeti ikiwataka wafike kujieleza Jumatatu mchana, lakini akaongeza; “Hilo suala la uraia wangu kama kweli wanaendelea nalo watakuwa wanajisumbua bure.”
Nape ang’aka
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnuye, alipoulizwa kama anafahamu ama ameshiriki vikao hivyo vya mikakati ya kuyanyamazisha magazeti hayo, aling’aka na kusema CCM hawana matatizo na Tanzania Daima wala Mtanzania.
“Hicho kikao kinafanyikaje? Mimi ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, huyo waziri anashughulika na wizara yake halafu huyo mtu wa Maelezo ana idara yake,” alisema.
Nape alidai hajawahi kuonana na waziri mtajwa kwa muda mrefu na kwamba hata hajui kama amerudi nchini tangu walipokutana nchini Afrika Kusini wiki kadhaa zilizopita.
“CCM kama chama hatuna matatizo na Tanzania Daima wala Mtanzania, hizo ni fitina zenu mnataka kutengeneza, vyombo hivi tunashirikiana vizuri hata niliwahi kutembelea ofisi zao baada ya kuteuliwa na hata kwenye ziara zetu mikoani tunavichukua,” alisema.
Waziri tajwa na kigogo mmoja wa Maelezo hawakupokea simu zao kutoa ufafanuzi hata walipoandikiwa ujumbe mfupi wa simu (sms) hawakujibu.
Sakata la kutekwa, kuteswa na kuumizwa vibaya kwa Kibanda linafananishwa na lile la Dk. Ulimboka kwani hadi sasa uchunguzi wa kuwasaka waliohusika unafanyika kimzaha.
Tangu alipoumizwa Dk. Ulimboka Juni 26 mwaka jana, ni mtuhumiwa mmoja pekee amefikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika na tukio hilo ingawa inaelezwa kuwa alikuwa amerukwa na akili akajipeleka kanisani na kudai kuhusika.
Zikiwa sasa ni wiki tatu tangu kujeruhiwa kwa Kibanda, hakuna mtuhumiwa hata mmoja aliyekamatwa na vyombo vya dola kuhusiana na tukio hilo, ingawa ndani ya wiki moja Jeshi la Polisi limekamata na kumchunguza Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare kisha kumfikisha mahakamani akidaiwa kujihusisha na ugaini kwa kutumia usahidi wa video.
0 comments:
Post a Comment