SITTA ASEMA WAVAMIZI WAMEYAGEUZA MAKAZI YA KUDUMU.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
RAMANI YA TANZANIA.
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema mawe ya mipaka ya Tanzania yameng’olewa na nchi jirani ambayo imeteka maeneo hayo kuwa himaya yake.
Sitta aliyataja maeneo hayo yaliyotekwa kuwa ni Murongo mpakani mwa Uganda ambako baadhi ya raia wa nchi hiyo wamejenga makazi yao ya kudumu. Eneo jingine ni Horiri kwa upande wa Kenya, alisema.
Sitta aliyasema hayo jana alipowasilisha taarifa mbalimbali za wizara yake na mapendekezo ya bajeti 2013/2014 katika Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inayoongozwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
Akizungumzia kwa undani juu ya suala hilo, Sitta alisema wananchi wa Murongo ambao ni raia wa Rwanda waling’oa mawe ya mipaka ya Tanzania na kujenga makazi yao ya kudumu.
Baada ya Serikali ya Tanzania kubaini mipaka kung’olewa iliamua kufanya mazungumzo na kufanikiwa kurudisha mawe hayo katika baadhi ya maeneo lakini mengine yalishindikana, alisema.
“Kuna mbaadhi ya mipaka yetu imetekwa kwa kung’olewa mawe ya mipaka.
“Sasa isingekuwa ushirikiano tulionao kati ya Tanzania na Uganda kungekuwa tayari kuna mapigano ya silaha lakini tunasuhukuru mazungumzo yalikwenda vizuri na baadhi ya maeneo tumeyarudisha.
“Kama eneo hilo la Murongo wananchi waling’oa mawe hayo zamani bila sisi kujua na kufanya makazi ya kudumu… sasa tumeona si vema kuwaondoa kwa vile inaweza kuleta msuguano.
“Kwa upande wa Kenya eneo la Horiri pale pia waling’oa mawe hayo lakini mazungumzo yamekwenda vizuri.
“Lakini kikubwa ninachosema ni kuweka mipaka hiyo ioenekane vizuri na kuwaelimisha wananchi juu ya ardhi kwa sababu inaonekana kuwa tishio na hitaji muhimu kwa kila nchi na raia wake,”alisema Sitta.
Alisema si vema kuweka nchi katika hali ya mapambano kwa kila jambo linalojitokeza bali inafanyika mikutano ya hadhara kwenye mipakani ya nchi kuwaelimisha wananchi.
Waziri alisema katika masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bado kuna kazi kubwa ya kufanya tena kwa tahadhari kabla ya kuanza kufungua milango ya ushirikiano.
“Ikiwa Tanzania tutaingia kabla ya kujiweka sawa kuna hatari ya kuingia katika sheria kandamizi ambazo pengine zitawafanya wananchi kushindwa kunufaika na jumuiya hiyo,” alisema.
Sitta alisema miongoni mwa maeneo ambayo Tanznaia inapaswa kuwa makini ni jinsi ya kuingia katika Soko la Pamoja, kuwa na shirikisho moja la fedha na shirikisho la siasa.
Alisema Rai Jakaya Kikwete ameshauriwa akatae kusaini mkataba wa namna ya kutumia vivutio vya nchi kwa vile nchini nyingine zina kivutio kimoja cha sokwe mtu.
“Tunajua ili sheria hiyo ipitishwe lazima marais wa nchi wanachama wakutane na kujadiliana kisha kutia saini, ndiyo maana tumewahi kumpa tahadhari rais wetu juu ya mambo ambayo tunaona yanaweza kutubana.
“Katika shirikisho la siasa hapa kuna tatizo kubwa sana… hilo suala linahitaji umakini mkubwa. ”Lazima tujue rais anapatikana vipi hasa nchi zenye muungano, wabunge na viongozi wengine wanaotokana na siasa.
“Hapa kikubwa ni kuanza kuwapa elimu wananchi polepole kwa sababu ndiyo watakaopitisha jambo hilo kwa kupiga kura za maoni, hivyo hivyo katika shirikisho moja la fedha.
“Pamoja na changamoto zinazokabili wizara yangu kama uhaba wa wafanyakazi, elimu ndogo kwa wananchi juu ya mtengamano na biashara katika nchi nyingine… kweli Watanzania wanateswa sana ndiyo maana tunapanga masoko kama ya ng’ombe na bidhaa nyingine ziwe mipakani kuepusha usumbufu.
“Katika suala la usalama wa chakula, Tanzania inaweza kuwa makao makuu ya ghala la chakula ya jumuiya na hivi sasa tunashirikiana na wizara nyingine kuweka mazingira vizuri.
“Katika sekta ya afya hapa tunaonekana kupata vikwazo kutoka Kenya ambao wanaonekana kulinda bidhaa zao na kupinga za Tanzania hususan konyagi yetu inayotengenezwa kwa korosho lakini wao inatengenzwa kwa miwa… sasa wanaweka vikwazo vya kitoto, hili nimepanga kukutana nao niwaeleze kuacha kuzuia bidhaa zetu mipakani.
“Sekta ya uchukuzi na ujenzi kama wizara tumeona suluhisho la kuondoa msongamano Bandari ya Dar es Salaam ni kujenga barabara za njia sita au nne zitakazopita Tangibovu, Banana, Kinyerezi na kuunganika huko mbele pia nyingine ijengwe Morogoro kupitia Tegeta hadi Chalinze ambazo zote zitaunganika,”alisema.
Pamoja na mambo mengi, Sitta alisema Jumuiya hiyo inapaswa kuwa na nchi sita kwa sasa na baada ya miaka 10 au zaidi ziongezwe.
Alisema kuna baadhi ya nchi hazijatimiza masharti na kama zitaunganishwa zitahatarisha amani na kuleta tishio la Al Shabab.
Sitta aliwasilisha pendekezo la bajeti ya wizara yake 2013/2014 inayofikia Sh bilioni 20.6.
0 comments:
Post a Comment