Kwa ufupi
“Nilifika nyumbani kwangu kama saa sita usiku
nikitokea kazini na nilipofika kwenye lango la kuingia ndani nilipiga
honi ili mlinzi anifungulie. Lakini ghafla nilivamiwa na kundi la watu.
http://www.mwananchi.co.tz
APIGWA, ATOBOLEWA JICHO NA KUNG'OLEWA KUCHA.
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda ametekwa na watu wasiofahamika na kisha kumjeruhi vibaya kwa nondo, mapanga na kisha kumng’oa meno, kucha na kumharibu jicho la kushoto.
Tukio hilo la kinyama linafanana kwa kiasi fulani na lile la alilofanyiwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania, Stephen Ulimboka.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi
usiku wakati Kibanda akirejea nyumbani kwake Goba Punguni, Kata ya Mbezi
Juu, kutoka kazini.
Tayari mwandishi huyo mkongwe wa habari, amesafirishwa jana kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
Aliondoka jana akisindikizwa na daktari kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimu (Moi).
Mkasa wenyewe
Akizungumza kwa tabu alipokuwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), hospitalini Moi, Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006), alisema:
“Nilifika nyumbani kwangu kama saa sita usiku nikitokea kazini na nilipofika kwenye lango la kuingia ndani nilipiga honi ili mlinzi anifungulie.
Lakini ghafla nilivamiwa na kundi la watu ambao walivunja kioo cha gari langu upande niliokuwa nimekaa.
Nilitokea kupitia mlango wa abiria lakini sikuweza kuwakimbia watu wale kwani walinikamata na kuanza kunishambulia kwa vitu vizito.”
“Baada ya kutoka kwenye gari, nahisi nilikanyaga sehemu mbaya, nikateleza na kuanguka wakanifuata...niliona kama watu watatu hivi wakaanza kunishambulia.
Sikuwa nafahamu kilichojiri, lakini nilisikia mwingine akimwambia mwenzake afande ‘mshuti... mshuti’ huyo alipoelekeza mtutu na kujaribu ‘kushuti’ (kupiga risasi) ilikuwa kama vile imegoma.
“Nikiwa bado niko chini, wakanipiga kwa kitu cha ncha kali kwenye jicho la kushoto, wakaning’oa meno na kucha katika vidole vya mkono wa kulia, walinipiga sana na nilipata maumivu makali.
Baada ya kunipiga na kunijeruhi waliniburuza hadi bembeni ya nyumba yangu na kunitupa na wakaondoka, baadaye majirani na wasamaria wema walikuja kuniokoa.
Mashuhuda baada ya tukio
Akizungumza jana, mzazi mwenzake, Angella Semaya alisema wakati Kibanda alipovamiwa hakusikia lolote:
“Niliamshwa na kelele za majirani ndipo nami nikaenda eneo la tukio. Sikuamini kama alikuwa Kibanda kwani alikuwa ametapakaa damu huku akigugumia maumivu makali... kwanza sikumjua kama ni yeye kwa jinsi alivyokuwa.”
“Nina wasiwasi na hawa watu kuwa wametumwa kwa kuwa hawakuchukua chochote zaidi ya kumdhuru mwili,” alisema.
Angella aliondoka jana na Kibanda pamoja na Mwandishi wa Habari, Eric Kabendera ili kumsindikiza Afrika Kusini atakapokuwa anapata matibabu.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006), Hussein Bashe alisema: “Tulikuwa na Kibanda hadi usiku kama 5:30 hivi, tukifuatilia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya na tulipoona hakuna kinachoendelea zaidi, tukaagana kurudi makwetu.”
“Kwa kweli taarifa za kuvamiwa na kushambuliwa kwake zimetushtua, kwani ameumizwa sana hasa jicho.
Daktari alishauri jicho liondolewe lakini nilikataa, jopo la madaktari bingwa wa macho wamemtazama na kuthibitisha kweli limeumia sana, tumewasiliana na mwajiri wetu ameamua kumpeleka Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
“Nawashukuru madaktari kwa jinsi walivyompokea na kumshughulikia katika kiwango kinachotia moyo. Pia waandishi kwa umoja waliouonyesha kwa kujitokeza haraka na kumjulia hali.”
0 comments:
Post a Comment