Mtuhumiwa alijifunika kwa kofia akiwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi
Na Gustav Chahe, Iringa
JESHI
la polisi mkoani Iringa wamebuni njia mpya ya kumfikisha mahakamani
mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha
runinga cha Channel Ten Daud Mwangosi kwa kuwatumia askari kanzu kama
watuhumiwa ili wamfiche mwenzao.
Pasificus Cleophace Simon mtuhumiwa wa
mauaji hayo mwenye namba G 2573 alifikishwa mahakamani hapo jana katika
ulinzi wa polisi huku waandishi wa habari wakizuiliwa kupiga picha na
kuzuiliwa kuingia katika chumba cha mahakama ambako kesi ilikuwa
ikiendeshwa.
Akifikishwa mahakamani hapo, mtuhumiwa huyo alikuwa katika gari la mahabusu (karandinga) kama
watuhumiwa wengine tofauti na siku za mwanzo alipokuwa akifikishwa mahakamani hapo kwa gari la kifahari.
Mara baada ya kuahirishwa kwa kesi
hiyo mwendesha mashtaka wa serikali Blandina Manyanda aliwaambia
waandishi wa habari kuwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa Gradness Nance
Bath kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 14 Mwaka huu igtakapotajwa tena
huku akieleza kuwa upelelezi haujakamilika na mtuhumiwa amerudishwa
mahabusu.
Siku ya kwanza mtuhumiwa huyo
alifikishwa mahakamani hapo kwa gari la kifahari lenye namba za kiraia T
320 ARC linalosadikiwa kuwa ni la RCO huku kwa mara ya pili akifikishwa
kwa miguu na kuondolewa mahakamani hapo kwa gari namba DFP 2175 pick up
akiwa katika ulinzi mkali huku
waandishi wa habari wakidhibitiwa na
polisi na mmoja wao kunusurika kupigwa jambo lililoamsha hisia tofauti
miongoni mwa wananchi wengi mkoani hapa.
Katika hali isiyo ya kawaida, 14
Februari Mwaka huu mtuhumiwa huyo mwenye namba G 2573 akiwa mahakamani
hapo aliwatukana waandishi wa habari matusi ya nguoni kuwataka wasimpige
picha huku akijidai kuwa muda si mrefu ataachiwa na kupambana na
waandishi mitaani.
Pasificus akiwa na jazba alisikika
akisema “mtapiga picha sana mtakavyo lakini hamjui kama kesho tu
nitatoka halafu tupambane mitaani huko. Nawaona sana mnaonipiga picha
tutakuja kukutana tu” alisema mtuhumiwa huyo.
Hata hivyo kuzuiwa kupiga picha kwa
waandishi kunaendelea kwa baadhi ya askari kwa kile walichokuwa
wakitumia amri kwaandishi kutokusimama katika maeneo ya mahakama
wakieleza kuwa sehemu hizo hazitakiwi kusimama jambo alililowafanya
waendesha mashtaka kuwakemea askari hao kuwa wapo kinyume na taratibu za
mahakama.
Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2
mwaka jana katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi alipokuwa
akiwajibika kwa kazi za kihabari wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Read more: http://audifacejackson.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment