RAIS wa Venezuela, Hugo Chavez, amefariki dunia jana (05.03.2013) baada
ya kuugua saratani na hivyo kufikisha ukingoni uongozi wake wa miaka
miwili katika taifa hilo la Amerika ya kusini lenye utajiri mkubwa wa
mafuta.
Chavez amefariki katika hospitali ya kijeshi huko Caracass baada ya kuugua na kufanyiwa upasuaji mara nne uliosababisha afya yake kuzorota. Aligunduliwa kuwa na saratani ya tumbo mnamo mwezi Juni mwaka 2011 na amekuwa akifanyiwa matibabu nchini Cuba kabla ya kurejeshwa nyumbani.
Rais wa Venezuela, Hugo Chavez (katikati) akiwa ameweka pozi na mabinti zake, Maria Gabriela, kushoto na Rosa Virginia katika mji wa Havana,
Cuba, Feb. 14, 2013.
Mnamo mwezi Oktoba mwaka jana, Chavez alishinda kirahisi muhula mwingine wa miaka sita kuliongoza taifa hilo kwenye uchaguzi mkuu lakini kutokana na hali yake mbaya ya afya hakuweza kuhudhuria shughuli ya kuapishwa kwake na hivyo kuilazimu mahakama ya juu nchini humo kuahirisha shughuli hiyo kwa mda usiojulikana.
Hisia za huzuni
Kifo chake kimewahuzinisha mamilioni wa wafuasi wake waliopendezwa na mtindo wake wa uongozi pamoja na sera zake kuhusiana na faida itokanayo na mafuta ya taifa hilo yaliyowapunguzia pakubwa mzigo wa gharama ya chakula na matibabu hasa kwa walioishi katika mitaa duni.
Mamia ya wafuasi wa Chavez walikusanyika mbele ya hospitali alikofariki kiongozi huyo wakilia na kupiga kelele wakisema " Sisi sote ni Chavez"
Ban Ki Moon
Kumekuwa na hisia mbalimbali kote ulimwenguni kufuatia kifo cha
Hugo Chavez, huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon akitoa
risala zake za rambirambi, "Amekuwa akitoa mchango wake katika maendeleo
ya nchi yake. Wakati huo huo, kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, ningependa kutoa risala za rambirambi kwa familia, raia na serikali ya Venezuela kwa kumpoteza rais Chavez."
Katika taarifa yake rais wa Marekani, Barack Obama, amesema, "Wakati huu mgumu Marekani inasisitiza kuwasaidia watu wa Venezuela na ari yake ya kuendeleza uhusiano wa maana na serikali ya Venezuela,Huku Venezuela ikianza ukurasa mpya katika historia yake.
Marekani inaunga mkono sera zinazoimarisha kanuni za demokrasia, utawala wa sheria na kuheshimiwa kwa haki za binaadamu."
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, amesema kifo cha Chavez ni janga kubwa na kwamba kiongozi huyo alikuwa mwanasiasa aliyesifika.
Kufuatia kifo cha rais Chavez, makamu wake ametangaza kuwa wanajeshi na polisi wamepelekwa kote nchini humo ili kulinda raia na kuhakikisha kuna amani, huku taifa hilo likiingia katika kipindi kigumu kisiasa na maombolezo.
Rais wa Venezuela, Hugo Chavez.
Uchaguzi kufanyika
Kifo cha Chavez sasa kinatoa fursa ya kufanyika uchaguzi utakaodhihirisha kama mfumo wake wa uongozi wa kisosholisti utaandelea nchini humo bila yeye kuwepo.
Uchaguzi unatarajiwa kufanywa katika siku 30 zijazo na kinyanganyiro kinatarajiwa kuwa kati ya makamu wa rais ambaye Chavez alimtaka kuwa mrithi wake wa kisiasa dhidi ya Henrique Capriles ambaye ni kiongozi wa upinzani aliyeshindwa na Chavez katika uchaguzi wa mwaka jana.
Henrique Capriles.
Kushindwa kwa Maduro kutaleta mabadiliko makubwa nchini humo na kutaathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano wake na mataifa mengine ya Amerika kusini ambayo yalitegemea pakubwa ufadhili wa Chavez kutokana na mafuta hasa taifa la kikomunisti la Cuba ambalo liliweza kujikwamua kutoka hali mbaya kiuchumi katika miaka ya 90 kutokana na usaidizi wa Chavez.
Marekani yakanusha kuhusika
Wakati huo huo, Marekani imekanusha vikali madai ya kuwa ilihusika katika Rais Chavez kupata ugonjwa wa saratani na kuyataja madai hayo kuwa ya kuchekesha.
Serikali ya Marekani ilitoa taarifa muda mfupi kabla kufariki kwa Chavez na kukanusha kuhusika kwa vyovyote vile na kifo cha Rais huyo kwa lengo la kulisambaratisha taifa hilo.
Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili haujakuwa mzuri kutokana na msimamo mkali wa kisosholisti wa Rais Chavez.
Venezuela imetangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa na marehemu Chavez atazikwa Ijumaa ijayo.
0 comments:
Post a Comment