WAWAKILISHI wa nchi wahisani na mashirika ya misaada wanakutana leo
mjini Doha, Qatar ili kuunga mpango wa kuchangisha fedha kwa ajili ya
kulijenga upya jimbo la Darfur.
Mkutano huo wa siku mbili, unaohudhuriwa na wajumbe 400, unafanyika kwa mujibu wa mkataba wa amani wa Julai mwaka 2011, uliotiwa saini mjini Doha baina ya Sudan na mfungamano wa makundi ya waasi.
Mkutano huo unafanyika miaka kumi baada ya waasi katika jimbo hilo la magharibi mwa Sudan kuanzisha harakati za kukomesha walichoita udhibiti wa mamlaka na mali, wa viongozi wa kiarabu nchini Sudan.
Uhalifu wa Janjaweed :
Ili kuwakabili waasi ,wanamgambo wa Janjaweed waliokuwa wanaungwa mkono na serikali ya Sudan walitenda unyama dhidi ya raia,ulioishtua dunia na kuifanya Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague itoe hati ya kisheria ya kuwezesha kumkamata Rais wa Sudan Omar al-Bashir kwa tuhuma za kutenda uhalifu wa kivita,uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji halaiki.
Uingereza yaahidi Pauni milioni 11 kwa mwaka:
Katika hatua ya kwanza,Uingereza imetoa ahadi ya kuchangia Pauni Milioni 11 kila mwaka kwa ajili ya jimbo la Darfur kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula na kwa ajili ya mafunzo yatakayowawezesha watu kupata ajira.
Waziri Featherstone ameeleza kuwa fedha hizo zitawasaidia masikini kupata nyenzo wanazohitaji ili kuweza kujisimamia wenyewe na hivyo kuzikabili vizuri zaidi hali za migogoro zinapozuka.
Maendeleo ya kilimo:
Mpango utakaofadhiliwa na wahisani na mashirika ya kimataifa ni pamoja na kuboresha kilimo, kuwawezesha watu kupata misaada ya fedha na kuchukua hatua ili kuwasaidia watu wa Darfur kujisimamia wenyewe chini ya uongozi wa mfumo wa serikali ya jimbo hilo ,unaofanyakazi kwa ufanisi zaidi.
Mkakati wa maendeleo ya jimbo la Darfur,unasisitiza kwamba wakati wa kuchukua hatua ni sasa, kwani kuchelewa kutasababisha mchakato huo uwe mgumu.
Hata hivyo wakati mikasa mibaya ya umwagikaji wa damu imeshapita, waasi na wanajeshi wa serikali wanaendelea kupambana,sambamba na mapambano baina ya jamii za kiarabu.
Wakati mgumu lakini hapana kushika tama
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo,UNDP Bwana Kuhnel amekiri kwamba hizi ni nyakati ngumu duniani kukusanya fedha.Lakini amesema litakuwa kosa kubwa kutoitumia fursa iliyopo duniani.
Ameeleza kwamba kinachohitajika ni kuanza juhudi na kupata kiasi cha fedha kitakachojenga imani ya mkakati unaokusudiwa kutekelezwa.
Usalama kwanza nyumbani:
Wakati huo huo wakimbizi wa ndani katika jimbo la Darfur,katika kambi kadhaa, walifanya maandamano kabla ya mkutano wa Doha kuanza kusisitiza ulazima wa kulipa kipaumbele suala la usalama.
Watu hao wamesema kuwa hawatarejea kwenye vijiji vyao kabla ya amani kurejea.
Justice and Equality Movement:
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alisema mapema mwaka huu kwamba kukataa kwa makundi muhimu kuutia saini mkataba wa Doha kumepunguza hatua za utekelezaji wa mkataba huo.
Kundi moja lililojitenga na chama cha "Justice and Equality" hapo jana(Jumamosi) lilikuwa kundi la pili kujiunga na mkataba wa Doha. Lilitiliana saini mjini Doha "makubaliano ya mwisho" na serikali ya Sudan.
0 comments:
Post a Comment