WAJIPANGA KUKWAMISHA BAJETI YA KILIMO,
MAIGE, LEMBELI WAONGOZA MASHAMBULIZI
MAIGE, LEMBELI WAONGOZA MASHAMBULIZI
http://www.mtanzania.co.tz. 
Waziri wa Kilimo na Ushirika, Christopher Chiza.
Dalili hizo zilionekana jana, wakati wabunge hao walipokuwa wakiijadili baada ya kuwasilishwa na Waziri wa Wizara hiyo, Christopher Chiza.
Aliyekuwa wa kwanza kuikataa bajeti hiyo ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli, ambaye alisema haiungi mkono kwa kuwa haionyeshi nia ya kutatua kero za wakulima.
Kutokana na hali hiyo, alisema kama ataiunga mkono, hatakuwa amewatendea haki wananchi wa Jimbo la Kahama na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.
Alisema kwamba, katika Jimbo lake la Kahama, kuna kata tano zinazolima tumbaku ambayo imekuwa ikiliingizia taifa pato la Sh bilioni 15 kila mwaka.
“Lakini wananchi hawa Mheshimiwa Spika, nimewapigia kelele sana, Mkuu wa Wilaya amepiga kelele sana, Mkuu wa Mkoa amepiga kelele na amezunguka sana kusikiliza kero za wananchi, lakini Serikali haisikii.
“Wakulima wa tumbaku katika jimbo langu wanaibiwa macho macho na Serikali ipo, wakulima wa tumbaku wanabambikiziwa madeni makubwa, yaani utashangaa, matokeo yake mwishoni mwa mwaka hawalipwi.
“Nimepiga kelele sana, nimemuomba ndugu yangu Mheshimiwa Waziri aje wilayani kwangu, lakini hataki, sijui ameweka nini kwenye masikio.
“Matokeo yake, viongozi wa vyama vya ushirika wamekuwa ni tatizo katika jimbo langu, hivi Ofisa Ushirika wa Wilaya ya Kahama yuko pale kwa maslahi ya nani?
“Huyu ndiye kinara wa kuchonga wizi, ndiye anayepitisha malipo yote ya vyama vyote vya msingi, ndiye anayepitisha viongozi wote wabovu ambao kila siku wanawaibia wakulima wa tumbaku, lakini Serikali iko kimya, siungi mkono hoja.
“Ninajua haya ninayoyasema kuna watu wengine wataudhika, lakini siungi mkono hoja kwa sababu mimi si kazi yangu kuwafurahisha watu, bali niko hapa kuzungumzia yanayowasibu wananchi,” alisema Lembeli.
Kutokana na kile alichosema ni Serikali kutowajali wakulima, alisema wakulima mwaka huu hawatalipwa fedha zao, kwa kuwa vyama vya ushirika vimekopa fedha benki kwa ajili ya kulipa madeni ya nyuma.
“Pia nauliza, ni kwa nini tumbaku yenyewe inauzwa kwa Dola, lakini wakulima wamekuwa wakilipwa kwa shilingi za Kitanzania?
“Hii ni biashara ya wapi, ni wizi mtupu, mkulima hajui kama tumbaku yake imeuzwa kwa Dola 1.26, kama kweli mnataka kumsaidia mkulima, kwa nini mkulima asiruhusiwe kufungua akaunti mbili, moja ya Dola na nyingine ya shilingi.
“Mheshimiwa Spika, nasema siungi mkono hoja hii kwa sababu nikiunga mkono hoja, wakulima wa kule Kahama wanaolima pamba na tumbaku, nitakuwa siwatendei haki.
“Yaani wakulima wa pamba ni masikini, wakulima kwa sababu ukilima eka moja ya pamba kipato chake hakizidi shilingi 200,000, lakini ni mwaka wa tatu sasa, Serikali inasema imekuja na rasimu ya kuwakomboa wakulima.
“Nasema siungi mkono hoja hadi hapo Serikali itakaposema imejiandaa vipi kufidia jasho la wakulima,” alisema Lembeli.
Katika maelezo yake, alizitaja kata ambazo wakulima wake wametapeliwa kuwa ni Kata anayotoka iitwayo Bulungwa, ambako kuna Vyama vya Msingi vya Mtaganya, Namatutu, Migamba na Mweli.
Kata nyingine ni Ulowa ambako kuna chama kiitwacho Twende na Wakati na Kata ya Uyogo ambako kuna chama kiitwacho Nsungansabi na Uyogo.
Kata nyingine ni Usheta vilipo vyama vya Kidanha, Nyeyela na Mihama pamoja na Kata ya Bukomela ambako kuna Chama cha Msingi cha Bukomela.
MAIGE APIGILIA MSUMARI
Naye Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, alisema haungi mkono bajeti hiyo na kwamba atashangaa kama wabunge wanaotoka Mkoa wa Shinyanga wataiunga mkono.
Maige ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema tatizo la wakulima wa pamba katika Mkoa wa Shinyanga ni kuporomoka kwa bei ya pamba na kwamba baada ya bei kushuka mwaka jana kutoka Sh 1,100 hadi Sh 600 kwa kilo, alitegemea Serikali katika bajeti yake ingekuja na mfuko maalum kwa ajili ya kukabiliana na anguko la bei.
“Kwa maana hiyo, bei ikiporomoka mwaka huu, wakulima watakula hasara tena kwa sababu hamjaleta mkakati wa kuhimili bei ya pamba kama ikishuka.
“Ili nikubaliane na bajeti hii, ninategemea mambo matatu, la kwanza, nategemea kuona fedha zimetengwa kwa ajili ya mfuko wa mhimili wa bei, pili, nione mkakati wa kutosha kwa ajili ya kufufua angalau viwanda vya kuchakata pamba, na la mwisho, iwepo mipango ya kutangaza na kusaidia wakulima wa pamba ili kuongeza tija.
“Mheshimiwa Waziri ni rafiki yangu, lakini wananchi wa Shinyanga ni marafiki zangu zaidi kuliko Mheshimiwa Waziri, nasema siungi mkono hoja,” alisema Maige.
Kuhusu njaa mkoani Shinyanga, alisema haridhishwi ya kasi ya kusambaza chakula cha njaa kwa kuwa kinapelekwa kwa wananchi baada ya muda mrefu.
RAMO MAKANI
Kwa upande wake, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani (CCM), naye alisema haungi mkono bajeti hiyo hadi hapo atakapoona kuna sababu za msingi za kuiunga.
Katika mchango wake, alitaka wakulima wa korosho walipwe bei nzuri inayokwenda sambamba na iliyoko katika Soko la Dunia.
Kwa mujibu wa Makani, baadhi ya watu wamekuwa wakitumia Soko la Dunia kuwaibia wananchi, jambo ambalo asingependa liendelee kuwapo.
SAID NKUMBA
Wakati wabunge hao wa CCM wakionyesha msimamo huo, Mbunge mwenzao wa chama hicho, Said Nkumba (Sikonge), aliiunga mkono na kusema pamoja na Serikali kufanya mazuri, bado kuna changamoto zinazotakiwa kufanyiwa kazi katika sekta ya kilimo.
CHIBULUNJE JE!
Mbunge wa Chilonwa, Ezekiah Chibulunje (CCM), aliitaka Serikali kuwasaidia wakulima ili wapate soko la zabibu, kwa kuwa Kiwanda cha Kusindika Mvinyo cha Stawico, kinanunua zabibu kwa bei ndogo.

0 comments:
Post a Comment