Na Rajab Mkasaba, PEMBA.
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Serikali
haitomvumilia mtu/kundi lolote, litakalojiingiza kwenye siasa, kwa
kutumia mrengo wa dini na kutishia kuvurugika kwa amani nchini.
Dk. Shein alieleza hayo, huko uwanja wa mpira Makombeni, mara baada
ya kulifungua tawi la kisasa la CCM Makombeni, na baadae kuzungumza na
WanaCCM na wananchi wengine, kwenye mkutano wa hadhara.
Alisema, katika siku za hivi karibuni, kumeibuka makundi yakitumia
vibaya, fursa ya kutangaaza dini na kuchukua baadhi ya vipengele vya
siasa na kuwababaisha wananchi, jambo ambalo halileti taswira nzuri
katika taifa kama hili, lililotawala amani na utulivu.
Makamu Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa kamwe Serikali kwa
kushirikiana na vyombo vyake, haitoyavumilia makundi hayo, kwani
yamekuwa yakiitumia fursa hiyo vibaya.
Alieleza kuwa ndani ya Serikali
ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa,
hakuna sababu ya kurejeshana kule taifa lilikotoka, na badala yake ni
vyema fursa za kujikusanya na kuhutubia zikawa zinahubiri umoja, amani
na mshikamano.
“Kundi lolote likigundulika linatumia vibaya fursa ya kutangaza dini,
na kujikita kwenye mambo ya kisiasa kwa lengo la kuwagawa wananchi na
kuvuruga amani na utulivu uliopo halitovumiliwa,”alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, alieleza kuwa, Serikali inayoongozwa na CCM tayari imeanza
mchakato wa kuifanya hospitali ya Abdallah Mzee ya Mkoani, kuwa ya Mkoa
kama ilivyoahidiwa wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.
“Wakati tulipokuwa tukipita katika kuomba ridhaa ya kuongoza nchi,
tulisema kuwa mkituchagua tutafanya mengi, ikiwa ni pamoja na kuifanya
hospitali hiyo kuwa ya Mkoa, sasa mambo yameanza katika kuitekeleza
ahadi hiyo,” alifafanua.
Kuhusu dhana zilizoibuka hivi karibuni, kwamba vyama vya upinzani
vitamuondoa Dk. Shein madarakani, kutokana na wingi wa kumiliki
vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, hao alisema wamechelewa. Alieleza
kuwa, yeye hawezi kung’olewa madarakani kwa wingi wa vitambulisho hivyo
vinavyomilikiwa na wafuasi wa chama fulani, kwani kinachohesabiwa siku
ya uchaguzi mkuu, ni kura na sio vitambulisho.
Alizidi kufafanua kuwa, wenye ndoto hizo wamechelewa na wamekuwa
wakiota ndoto za mchana, ambazo hukosa jawabu makini na kubaki
wakitapatapa. Akieleza kuhusu Katiba ya Zanzibar, alisema kila mmoja
anawajibu wa kuifuata kwa vitendo, maana hakuna mtu wala kundi la watu
lililojuu ya katiba ya nchi.
Katika hatua nyengine Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar,
aliwataka vijana, waache tabia ya kukimbilia nje ya nchi kwa kutafuta
kazi, na badala yake watulie nchini ili kujikusanya pamoja kwenye
vikundi vya ushirika.
Alifafanua kuwa, Serikali imekuwa mbioni kila siku kuhakikisha vijana
wake wanawezeshwa kupitia vikundi vya ushirika, kwani Serikali haina
uwezo wa kuajiri kila mmoja. Mapema Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM
Zanzibar aliwakabidhi kadi za CCM wanachama wapya 291wakiwemo wa Jumuia
za CCM, mara baada ya kulifungua tawi jipya la kisasa la CCM Makombeni.
Awali dk Shein na ujumbe wake, ulitembelea tawi la CCM la Mizingani
na ambapo yeye mwenyewe peke yake aliahidi kuchangia shilingi milioni 2
ambapo viongozi wengie aliofuatana nao katika harambee iliyofanywa hapo
hapo waliahidi kuchangia shilingi milioni 5.4 kwa ajili ya ujenzi wa
matawi ya kisasa ya CCM ya Mizingani na Chambani.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
alisema tayari CCM imeshajipanga vyema kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa
Jimbo la Chambani.
“Sisi CCM tunasema kuwa tuko tayari kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa
ubunge wa Jimbo la Chambani, na hatuendi kushiriki tunaenda kushindana,”
alisema Vuai.
0 comments:
Post a Comment