BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

LISSU: CCM IMEINGILIA MCHAKATO WA KATIBA.

ADAI FEDHA ZILIZOOMBWA KWA AJILI YA TUME NI KUFURU.http://www.freemedia.co.tzMbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu.
 
MSEMAJI Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu amedai kuwa matumizi ya fedha zilizoombwa kwa ajili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni kufuru.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, alitoa kauli hiyo wakati akitoa maoni ya kambi ya upinzani kwa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka ujao wa fedha 2013/2014.

Alisema katika mwaka wa fedha 2013/14, Bunge linaombwa kuidhinisha sh bilioni 33.944, sawa na kiasi kile kile kilichoidhinishwa mwaka wa fedha uliopita.

Lissu alisema kiasi hicho ni pamoja na sh bilioni 12.193 kwa ajili ya kulipia posho za vikao kwa wajumbe wa tume 34 na sekretarieti 160, sh bilioni 1.728 kwa ajili ya posho ya kujikimu kwa wajumbe na sekretarieti wanaposafiri nda
ni ya nchi kikazi na sh bilioni 1.650 kwa ajili ya kulipa gharama za nyumba za wajumbe na sekretarieti wanaotoka nje ya Dar es Salaam.

Akichanganua matumizi ya tume hiyo, inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, Lissu alisema kuna sh milioni 18 zinazoombwa kwa ajili ya kugharamia chakula kwa wajumbe wa tume na sekretarieti watakaopata maambukizi ya ukimwi.

“Kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka Serikali ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kama kuna uhalali wowote wa kutumia fedha za wananchi ili kununua ‘chakula maalumu’ kwa ajili ya wajumbe na sekretarieti ya tume watakaopata ukimwi kwa sababu ya kuendekeza ngono zembe na starehe zao binafsi,” alisema.

Lissu alisema wajumbe hao ambao wengi ni wazee, wanatakiwa wafanye kazi ya tume vinginevyo Bunge lielezwe kwa ufasaha ni kwa namna gani mchakato huu wa Katiba mpya unatazamiwa kusababisha maambukizi ya ukimwi kwa wajumbe hao.

Kwa mujibu wa Lissu, pia kuna sh milioni 60 kwa ajili ya usafiri wa ndani, sh milioni 50 kwa ajili ya gharama za malazi kwa wajumbe wa tume na sekretarieti wanaposafiri kikazi, sh milioni 423 kwa ajili ya chai na vitafunwa na sh milioni 50 kwa ajili ya wahudumu wanaosaidia kazi za tume wakiwa mikoani wakati wa kushiriki kwenye mabaraza ya katiba na shughuli za upigaji kura ya maoni.

Lissu alisema vile vile, Bunge limeombwa kuidhinisha sh milioni 60 ya kulipia maji kwa matumizi ya ofisi za tume, sh milioni 30 kwa ajili ya kulipia gharama za usafiri wa basi na teksi kwa wajumbe na sekretarieti watakaposafiri ndani ya nchi kikazi na sh milioni 103 kwa ajili ya kulipia gharama za simu za mkononi.

Akiendelea kuanika matumizi ya tume hiyo, Lissu alisema Bunge linaombwa kuidhinisha posho na ulaji zaidi ya huu kwa ajili ya wajumbe na sekretarieti ya tume.

Alisema ulaji huu mwingine unajumuisha sh milioni 604 kwa ajili ya posho kwa wajumbe wa tume na sekretarieti wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.

Alisema maelezo ya tume yamejaribu kuhalalisha matumizi ya fedha hizi za ziada kwa kuzibatiza jina la ‘posho ya mazingira magumu’, wakati vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vitafanyika jijini Dar es Salaam au Dodoma.

Lissu aliongeza kuwa zipo sh milioni 266 zinazoombwa kwa ajili ya chakula na viburudisho wakati wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, sh milioni 12 nyingine kwa ajili ya huduma za chakula na viburudisho kwa shughuli zinazohusiana na tume na sh milioni 185 kwa ajili ya kulipia usafiri wa basi na teksi.

Aidha, alisema kuna sh milioni 30 za utengenezaji wa fulana na kofia kwa wajumbe wa tume na sekretarieti wakati wa kushiriki kwenye uhamasishaji kuelekea upigaji wa kura ya maoni, sh milioni 40 nyingine kwa ajili ya utengenezaji wa sare wakati wa maadhimisho mbalimbali ya kitaifa na sh milioni 12 kwa ajili ya posho za kujikimu kwa watumishi wa tume watakaohudhuria kwenye maadhimisho mbalimbali ya kitaifa.

“Kwa ujumla, Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha jumla ya sh bilioni 19.039 kwa ajili ya posho za aina mbalimbali na malipo mengine yanayowahusu wajumbe na sekretarieti ya tume kwa mwaka wa fedha 2013/14. 

Hii ni zaidi ya asilimia 56 ya bajeti yote inayoombwa kwa ajili ya tume,” alisema.

Kwa mahesabu hayo, Lissu alisema wajumbe wa tume, katibu na naibu katibu pamoja na wakuu wa vitengo saba vya tume na madereva wao, kila mmoja atalipwa wastani wa sh milioni 16.756 kwa mwezi huo mmoja, au sh 558,547 kama posho ya kujikimu kwa kila siku moja.

“Mheshimiwa Spika, katika nchi ambayo wauguzi katika hospitali za umma wanalipwa mshahara wa kuanzia takriban sh 360,000 kwa mwezi na walimu wa shule za msingi wanaanzia sh 250,000 na wale wa sekondari sh 325,000 kwa mwezi, malipo haya kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yana uvundo na harufu mbaya ya rushwa kwa wajumbe wa tume,” alisema Lissu.

Mabaraza ya Katiba.
Lissu alisema Februari mwaka huu, tume ilichapisha mwongozo kuhusu muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake.

Alisema mwongozo huo ulisainiwa na Mwenyekiti wa Tume Jaji Warioba na ulianza kutumika Machi Mosi, mwaka huu.

Alisema ingawa tume imedai kwamba mwongozo huo ulitolewa kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kambi hiyo inaamini kwamba ulitolewa kinyume na matakwa ya sheria hiyo na kwa lengo la kuinufaisha CCM na washirika wake.

Kwa maana hiyo, alisema mikutano ya uchaguzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya kwa upande wa Tanzania Bara imeendeshwa na makada wa CCM wakati kwa upande wa Zanzibar imeendeshwa na viongozi waliochaguliwa na wananchi walioshiriki katika mikutano hiyo bila kujali itikadi au uanachama wao katika vyama vya siasa.

Alisema ndiyo maana karibu nchi nzima wananchi wengi wasiokuwa wanachama wa CCM ambao walipata kura nyingi katika kura za mikutano ya uchaguzi ya vijiji na mitaa walienguliwa kwenye michujo iliyofanyika katika kamati za maendeleo za kata zilizowekwa kwa mujibu wa mwongozo wa tume.

Lissu alisema hata mahali ambapo wananchi wasiokuwa wanaCCM walifanikiwa kupenyeza katika chekeche la kamati za maendeleo za kata (WDC) wamefanyiwa mizengwe na wanaCCM ili waondolewe katika orodha ya wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya.

Alisema mfano mzuri ni Beatus Kipeya aliyechaguliwa mjumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Arusha Mjini kwa kupitia Kata ya Sombetini.

Alisema mara baada ya Kipeya kuchaguliwa kwenye kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Sombetini cha tarehe 8 Aprili, 2013, siku hiyo hiyo Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha, Allan G. Kingazi alimwandikia Mkuu wa Wilaya ya Arusha kumlalamikia juu ya kuchaguliwa kwake.

Alisema ukiacha Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Arusha, watu wengine wote walionakiliwa barua ya malalamiko ya Katibu wa CCM Kingazi ni makada wa CCM.

“Wote hawa hawahusiki kisheria kwa namna yoyote ile katika mchakato wa uundaji wa mabaraza ya katiba ya wilaya. Chombo pekee ambacho kinahusika kisheria na mchakato wa kuunda mabaraza hayo na ambacho kilitoa mwongozo wa namna ya kuyaunda, yaani tume, haikuandikiwa wala kunakiliwa barua ya malalamiko ya Katibu wa CCM Kingazi,” alisema.

Lissu aliongeza kuwa endapo serikali itashindwa kutekeleza ahadi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi yake, na endapo muswada utakaoletwa hautakidhi matakwa ya kuboresha mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, basi CHADEMA itahamasisha Watanzania kuikataa rasimu ya katiba mpya kwenye kura ya maoni.

“CHADEMA itawaalika wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania nzima, pamoja na taasisi za kiraia na za kidini, vyama vya siasa na Watanzania wote wenye nia njema na taifa hili kuhamasisha Watanzania kuikataa rasimu ya katiba mpya kwenye kura ya maoni,” alisema.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: