Na Juma Mtanda, Morogoro.
TIMU ya soka ya Mawenzi Market Sport Club imendeeleza ubabe katika ligi daraja la nne kufuatia kutoa kipigo kikali kwa timu ya Msamvu Terminal katika mchezo wa kusaka nafasi tatu za kucheza ligi daraja tatu ngazi ya mkoa kuitandika bao 4-0 katika ligi hiyo inayoendelea kwenye uwanja wa Sabasaba Manaispaa ya Morogoro.
Kutokana na ubabe huo timu ya Market Sport Club tayari imekusanya pointi 13 kutokana na ushindi wa michezo minne kufuatia kushuka dimbani mara tano na kutoa sare mchezo mmoja huku ikiwa na pointi 13 na mabao ya kufunga 16 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne.
Mawenzi Market ilianza kampeni hiyo kwa kuifunga timu Mazimbu Market kwa ushindi wa bao 3-2 ikaongeza dozi katika mchezo wa pili ambapo waibuka na ushindi wa bao 5-0 dhidi ya Compassion, ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na You
ng Boys, ikashinda bao 7-1 kwa Sultan Rangers kabla ya kuibuka na ushindi wa bao 4-0 dhidi ya Msamvu Terminal.
Katika mchezo huo kati ya Market Sport Club dhidi ya Msamvu Terminal ilipata mabao matatu katika kipindi cha kwanza ambapo mshambuliaji, Haji Mfaume aliandikia timu yake bao la mapema la dakika tisa, kabla ya kupachikwa bao la pili dakika ya 17, Asley Elias huku mshambuliaji, Mrisho Said akitumbukiza mabao mawili pekee yake likiwemo la dakika ya 42 na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa ushindi wa bao 3-0.
Kipindi cha pili vijana hao wa Market Sport waliendelea kulikasaka lango la wapinzani wao na kumpa mwanya Mrisho Said kufumania nyavu dakika ya 59 baada ya ngome ya ulinzi ya Msamvu Terminal kushindwa kuhimili kasi ya washambuliaji wa Market Sport na kufanya mchezo huo kumalizika kwa ushindi wa bao 4-0.
Ligi hiyo iliyoanza kutimua vumbi April 11 mwaka huu imekuwa na ushindani wa hali ya juu timu ikiwa na lengo la kuwania nafasi tatu za juu za kucheza ligi daraja la tatu mkoa wa Morogoro msimu wa mwaka 2013/2014.

0 comments:
Post a Comment