BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

‘MAZINGAOMBWE' YA UGAIDI.

MKAKATI mahususi wa kuwashughulikia baadhi ya wanasiasa maarufu hapa nchini walio katika kambi ya upinzani wanaodaiwa kutiliwa shaka na duru za kiusalama kuhusu mienendo yao ya kisiasa na hata ile ya binafsi, unaratib
iwa nyuma ya kivuli cha ugaidi.
 






















Utekelezaji wa mkakati huo, unadaiwa kuwahusisha makachero waliobobea katika fani hiyo walio nje ya mfumo rasmi wa kikachero, wakishirikiana kwa karibu na taasisi zote za ulinzi na usalama hapa nchini.

Taarifa zilizolifikia MTANZANIA Jumatano kutoka vyanzo vyake mbalimbali zimedai kuwa, uchunguzi wa muda wa makachero wa taasisi mbalimbali za ulinzi na usalama hapa nchini, uliokuwa ukitafiti chanzo cha kuibuka ghafla kwa vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyohusisha utekaji na utesaji watu maarufu hususan wakosoaji wa Serikali, ulibaini kuwa nyuma ya matukio hayo, wapo wanasiasa wanaowania kushika mamlaka ya dola.


Afisa mmoja wa jeshi aliyezungumza na gazeti hili, alidai kuwa taasisi za usalama zimefanya uchunguzi wa kina na kubaini kuwa vitendo vya utekaji na utesaji raia, vinafanywa na mkusanyiko wa kikundi cha watu ambao ni wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa, wakiwa na baraka za viongozi wao wa kisiasa.

Alidai, licha ya kugundulika kwa ukweli huo, Serikali imekuwa ikisita kuwachukulia hatua stahiki za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani kwa kuhofia kuzua mtafaruku miongoni mwa wafuasi wao ambao kutokana na uelewa wao mdogo, wamejengewa imani yenye muelekeo wa kuwaabudu ndani ya mioyo yao.

Taarifa zaidi zilizokusanywa na timu ya MTANZANI Jumatano, zinaeleza kuwa Serikali imeamua kuanza kuchukua hatua za taratibu za kuufahamisha umma jinsi baadhi ya wanasiasa wanavyojihusha na matukio ya uvunjifu wa amani, mojawapo ikiwa kuwafikisha mahakamani wale ambao uchunguzi umewabaini kuhusika.

Zinaeleza kuwa mwenendo wa baadhi ya kesi zinazowahusu wanasiasa wanaodaiwa kushiriki kupanga na kutekeleza mipango ya uvunjifu wa amani, unaashiria kuwepo kwa mkakati wa makusudi wa kuvishughulikia vyombo vinavyodaiwa sasa kuchukua mkondo wa kihalifu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kisiasa.

Madai haya yanaungwa mkono na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kapteni Sambwee Shitambala, ambaye katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumatano ya hivi karibuni, alieleza kuwa baadhi ya makachero ambao wako nje ya mfumo rasmi wa Serikali wa kikachero wamepewa jukumu la kuvishughulikia vyama korofi na wana siasa ambao nyendo zao zinatiliwa shaka.

Shitambala ambaye pia ni mwanasheria, alimtaja moja kwa moja Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, Mabere Marando, kuwa mmoja wa mashushushu aliyepandikizwa katika vyama vya siasa vya upinzani, kwa lengo la kuchunguza mwenendo wa vyama hivyo na hata viongozi wake.

Alisema, Marando ni mmoja wa makachero walio nje ya mfumo rasmi wa kikachero, aliyepewa jukumu la kufanya kazi za kikachero ndani ya vyama vya siasa vya upinzani.

“Mfano mzuri angalia tukio la kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, ambaye awali alituhumiwa kupanga ugaidi. 


Jiulize aliyekamatwa ni Lwakatare au Chadema? Hivi kwanini wanasheria kama Marando na Profesa Safari wamejiingiza wote kwenye kesi hiyo?

“Hivi unaweza kuamini kuwa ni kweli Marando anaweza kujitokeza hadharani akaingilia mwenendo wa kesi iliyo mahakamani, kwa kutaja orodha mpya wa watuhumiwa wa ugaidi na kutaja namba zao za simu huku akijua kuwa ni kosa?

“Kama mtu ana akili atagundua alichokuwa anafanya Marando, alikuwa anakimaliza Chadema bila wenyewe kujua, ni shushushu yule sasa kwa akili ya kawaida kabisa, jiulize ni kweli alipokuwa anakwenda mahakamani baada ya kutangaza yale majina alikuwa anakitetea chama au mteja wake ?.


 Yeye kama wakili ina maana amewaaibisha mawakili wengine kuwa alikuwa haelewi alichokuwa anakifanya kwa sababu katika hali ya kawaida, alipaswa apeleke yale majina mahakamani kama ushahidi lakini si kwa mtindo alioufanya,” alisema Shitambala.

Alieleza zaidi kuwa, Marando hatetei Chadema bali alikuwa anaongeza idadi ya watuhumiwa kwa mtindo aliotumia kutaja majina.

Alitoa mfano mwingine unaoonyesha mashaka kuhusu mwenendo wa Marando kuwa ni kuchanganya namba ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini na ile ya Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa kuwa ni tendo la makusudi lililolenga kuifanya taarifa kutoaminika.

“Marando ni shushushu, hawa jamaa huwa hawaachi kazi, ana uzalendo kwa nchi yake hivyo hata haya anayoyafanya sasa akiwa upinzani ni kwa sababu ya usalama wa taifa hili,” alisema.

Katika hatua nyingine, Shitambala aliwashutumu waandishi wa habari kuwa baadhi yao wamenunuliwa na wanatumika kuipotosha jamii na watu wenye tamaa ya madaraka.

Aliwataka wa andishi wajue kuwa wanajitoa kafara bila wao kujua, kwa kuwa wanatumika kirahisi kwa kuwapamba watu wasio na mapenzi mema na taifa kwa kuandika habari zao ambazo wakati mwingine hazina ukweli.

“Waandishi wa habari baadhi yenu mnaifanya jamii iamini vitu ambavyo havipo, kiujumla baadhi yenu waandishi mnapotosha, ningekuwa ‘president’ leo nahisi ningefunga magazeti yenye kuwalisha sumu wananchi na kupamba watu wenye tamaa ya madaraka kwa gharama ya chochote.”

Alieleza kushangazwa na tukio la Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis Msaki kutajwa kwenye mkanda aliorekodiwa Lwakatare, kwamba atatekwa na kuuawa lakini hakuna chombo cha habari kilichohoji na kulaani.

“Msaki ni mwandishi wa habari, lakini hakuna chombo cha habari kilicholalamika au kulaani kuwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema anapanga mipango ya kumdhuru, waandishi jitazameni upya kwa sababu ya kwenu tena ya hatari mnayanyamazia, lakini mengine hata ya kipuuzi mnayakimbilia bila hata kufanya uchunguzi wowote.

Kauli hii ya Shitambala imekuja huku kukiwa na tetesi za kuwepo mikanda mingine zaidi ya ule aliorekodiwa Lwakatare inayowaonyesha baadhi ya viongozi wa kisiasa, wakikiri kufanya njama za kuwadhuru watu maarufu.

Hata hivyo, mikanda hiyo bado haijawekwa wazi na inadaiwa kuwa iko mikononi mwa makachero ambao wanaendelea kuichunguza.

CHANZO  http://www.mtanzania.co.tz
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: