JIJI la Dar es Salaam bado linazizima kufuatia kifo cha aliyekuwa mwasisi wa Taasisi ya Moyo Tanzania (THI), Dk. Ferdinand Massau Magessa aliyefariki dunia, majira ya saa 12 jioni ya Mei 16, mwaka huu katika Hospitali ya Aga Khan, Dar, Ijumaa Wikienda lina mkasa wa kukutoa machozi.
“Kwa muda mrefu marahemu alikuwa akisumbuliwa na kidonda kwenye koo hali iliyomfanya aw
e anakula kwa kutumia mrija kwa sababu alikuwa akisikia maumivu wakati wa kumeza.
“Mbaya zaidi akiwa bado anasumbuliwa na tatizo hilo akapatwa malaria, tukampeleka Aga Khan ambako alifariki dunia,” alisema Mkama akiwa kwenye msiba nyumbani kwa marehemu, Mbweni Kwajumbe, jijini Dar.
Mwili wa marehemu uliagwa jana saa 5:00 asubuhi katika Hospitali ya Aga Khan na kusafirishwa leo kwenda Kijiji cha Murutunguru, Ukerewe, Mwanza kwa mazishi huku kifo chake kikiibua mengi.
YESU alitumwa na Mungu kwenda Israel kuwaambia Wayahudi neno lake ambalo linaokoa lakini watu hao walimkataa na kumuua, ndivyo inavyoweza kutafsiriwa kwa marehemu Dk. Massau aliyekuwa shujaa mzalendo.
Kwamba, kufuatia kuongezeka kwa magonjwa ya moyo nchini, aliamua kuacha kazi ya ‘mapesa mengi’ nchini Marekani ambako alilipwa mshahara mnono na kuleta ukombozi Tanzania kwa kufungua hospitali ya kutibu magonjwa ya moyo, lakini serikali ilionekana kumkataa.
Serikali ni kama ilimkataa kufuatia kitendo cha Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF kumnyang’anya jengo walilompangishia kufanyia kazi na kuwaondoa wagonjwa waliokuwa wamelazwa kwa madai ya kumdai kodi bila kujali kuwa alikuwa akitetea roho za Watanzania wenzake wanaoteswa na magonjwa ya moyo.
Kuanzia hapo, habari zinasema hali ya afya ya daktari huyo ilianza kubadilika ambapo watu wake wa karibu wanadai ‘stress’ au mawazo yalikuwa yakimchanganya kila kukicha.
Baadhi ya waombolezaji kwenye msiba nyumbani kwa marehemu, Mbweni Kwajumbe walisema dokta huyo alileta ukombozi kwa Watanzania lakini waliotakiwa kukombolewa wenyewe walikuwa hawako tayari (kama Wayahudi).
“Inauma sana! Jamaa aliipenda nchi yake ndiyo maana aliamua kuachana na nchi ya Marekani kuja kuanzisha taasisi yake nchini, lakini cha ajabu mizengwe ilikuwa mingi, alipigwa vita, mawazo yakamjaa.
“Kama uliwahi kumwona wakati anaanzisha THI mwaka 2005 afya yake ilikuwa imara, lakini ulipoanza mgogoro wa NSSF, alikongoroka sana,” alisema Magana aliyekuwa kwenye msiba huo.
Marehemu Dk. Massau alihitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tawi la Muhimbili mwishoni mwa miaka ya 80. Alipata mafunzo ya upasuaji wa moyo katika Chuo Kikuu cha Hubei nchini China.
Dk. Massau aliwahi kufanya kazi nchini Marekani katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Texas (THI) akiwa ameongeza ujuzi kwenye Chuo Kikuu cha Texas Medical.
Mwaka 1996 aliongeza ujuzi tena kupitia kwa Profesa Denton Cooley ambaye ndiye mwanzilishi na mpasuaji mkuu katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Texas, Marekani.
Baada ya kuona utendaji wake wa kazi ni wa hali ya juu, Dk. Cooley aliiandikia barua Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akitaka kumtambua Dk. Massau na uwezo wake wa kazi.
Hata hivyo, inasemekana serikali ilikaa kimya juu ya barua hiyo. Waziri wa afya alikuwa Dk. Aron Chiduo.
Mwaka 2000, Dk. Massau alirejea rasmi nchini na kufanya kazi katika Hospitali ya TMJ ambapo pia ilimsaidia kuanzisha taasisi yake.
NSSF WALIVYOMMALIZA.
Aprili 2012, NSSF kupitia amri ya Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi, iliifunga taasisi yake na kuwahamishia wagonjwa wote kwenye hospitali nyingine kwa kile kilichodaiwa ni taasisi hiyo kushindwa kulipa shilingi bilioni saba za pango.
Hadi Dr. Massau anafikwa na umauti alikuwa akiendelea na ujenzi wa jengo la taasisi yake huko Mbweni, Dar.
Marehemu ameacha mke na watoto watano. Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.
0 comments:
Post a Comment