KWA UFUPI
Ni bahati mbaya kwamba wabunge bado wanaendekeza itikadi za vyama badala ya kujadili hoja kwa uzito wake kwa lengo la kuweka mbele masilahi ya taifa badala ya matakwa ya vyama wanavyoviwakilisha bungeni.Waziri wa Mambo ya Ndani,Emmanuel Nchimbi
BUNGE jana lilipitisha Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo liliidhinisha jumla ya Sh741 bilioni, huku Sh579 bilioni zikiwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh163 bilioni kwa miradi ya maendeleo. Hatua hiyo ya Bunge ilifuatia mjadala wa hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani na ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Hotuba hizo mbili zilizua malumbano makali kati ya wabunge wa chama tawala na wale wa upinzani, huku kila upande ukibeza fikra na mawazo ya upande wa pili pasipo kuangalia uzito wa hoja hizo. Tunaweza kusema kwamba malumbano hayo yaliegemea hasa katika itikadi za kisiasa, hivyo kudhoofisha au kuzima hoja za msingi zilizowasilishwa na baadhi ya wabunge wa kambi hizo mbili.
Ni bahati mbaya kwamba wabunge bado wanaendekeza itikadi za vyama badala ya kujadili hoja kwa uzito wake kwa lengo la kuweka mbele masilahi ya taifa badala ya matakwa ya vyama wanavyoviwakilisha bungeni.
Hii ni kansa inayoendelea kulitafuna Bunge letu, kwani wabunge wanaposhindwa kutenganisha hoja zenye masilahi kwa taifa na zile zenye masilahi kwa wanasiasa wanakuwa hawawatendei haki wananchi hata kidogo.
Tunazungumzia suala hili kwa uchungu mkubwa kutokana na unyeti wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ambayo pia inalisimamia Jeshi la Polisi. Kwa sababu jeshi hilo ni roho ya nchi, tungetegemea wabunge wa kambi hizo mbili kuweka kando tofauti zao na kuupa mjadala wa hotuba zote mbili z
a Bajeti ya wizara hiyo uzito unaostahili.
Ni vigumu kuamini kwamba wabunge wengi hawajatambua kuwa, kutokana na matukio makubwa ya kihalifu yanayoikumba nchi yetu hivi sasa, tunalihitaji Jeshi la Polisi pengine kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya taifa letu.
Amani iliyokuwa imetamalaki kiasi cha dunia kuiona nchi yetu kama kisiwa cha amani sasa inatikiswa na maadui wa ndani wakishirikiana na washirika wao kutoka nje. Tukio la bomu jijini Arusha mwishoni mwa wiki, ambapo watu kadhaa walikufa na wengine kujeruhiwa ni kielelezo cha hali hiyo.
Hivyo, tunalishangaa Bunge kutoona umuhimu wa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuliimarisha jeshi hilo ambalo ni dhaifu. Hali tuliyomo inatulazimu kuajiri askari wasiopungua 50,000 badala ya 3,000 waliotangazwa katika hotuba ya Waziri juzi. Askari mmoja bado anahudumia watu 1010 badala ya 450 kwa kiwango kinachokubalika sasa.
Kuendeleza lawama kwa jeshi hilo hakutatusaidia iwapo haitakuwapo dhamira ya kuliimarisha na kuhakikisha lina askari wenye weledi, waliopewa elimu na mafunzo stahiki.
Matumizi ya FBI kwa matukio ya uhalifu sio mkakati endelevu, badala yake jeshi hilo lifundishwe kupambana na wahalifu, lipewe vifaa vya kutosha na vya kisasa. Serikali iwe na dhamira ya kuondoa unyonge kwa askari wetu kwa kuwapa makazi mazuri, usafiri, bima ya maisha na mishahara stahiki.
Hayo yote yamo ndani ya uwezo wetu, kinachohitajika ni utashi tu wa kisiasa.
Ili kuhakikisha kwamba jeshi hilo na vyombo vingine vya dola vinakuwa huru na adilifu, Katiba Mpya itakayoundwa itamke bayana kwamba jeshi hilo na Idara ya Usalama wa Taifa ni vyombo vya umma, hivyo visifungamane na upande wowote. Hatua hiyo itavikomboa vyombo hivyo kutoka katika makucha ya wanasiasa.
0 comments:
Post a Comment