NI WANAODAIWA KUJIHUSISHA NA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA, APUUZA TUHUMA, AMTAKA MBUNGE KUWASILISHA USHAHIDI.http://www.mtanzania.co.tz
WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA.
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewakingia kifua na kuwatetea baadhi ya mawaziri waliotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini. Pinda alitoa utetezi huo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF) katika kipindi cha maswali kwa waziri mkuu (papo kwa hapo).
Msingi wa swali la mbunge huyo ulijikita katika hoja iliyotolewa hivi karibuni na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) ambaye aliwatuhumu baadhi ya mawaziri kujihusisha na biashara hiyo haramu.
“Mheshimiwa waziri mkuu kuna kauli iliwahi kutolewa humu bungeni. Hivi karibuni Mbunge wa Mwibara alisema wapo baadhi ya mawaziri wanaojihusisha na biash
ara ya dawa za kulevya.
“Kauli hii ni nzito na inatia aibu Serikali, kama kweli mawaziri hawa wapo, je! ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na kauli hii?,” alihoji.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema hakuna taarifa inayoonyesha kama kuna waziri anayejihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Pinda Alisema taarifa hizo hazina ukweli na kumtaka Lugola kuwasilisha ushahidi wake kuhusiana na tuhuma hizo uweze kufanyiwa kazi na hatua ziweze kuchukuliwa.
“Mimi ni mtu mzima, naamini nanyi wabunge ni watu wazima, hivyo ni muhimu kauli zetu tunazotoa zipimwe kabla ya hatujazitoa,” alisema Pinda.
Pinda alisema uteuzi wa mawaziri hufanywa baada ya Rais kujiridhisha na mchahakato mkubwa kufanyika kabla ya uteuzi.
“Mimi kazi yangu ni kusema hakuna waziri yoyote anayejihusisha na biashara ya dawa za kulevya, Lugola alete ushahidi wake tuweze kumpelekea Rais.
“Naheshimu kauli za wabunge, lakini kauli hizi zinahitaji kupimwa kabla ya kutolewa. Kauli hii ni nzito na pia inashtua,” Alisema Pinda.
Katika swali lake la nyongeza, mbunge huyo alitaka suala hilo lishughulikiwe kwa kanuni kwa ushahidi huo kuwasilishwa bungeni kwanza kabla ya kufikishwa serikalini.
“Kama Naibu Spika (Job Ndugai) atatoa kauli ya kumtaka mbunge huyo awasilishe ushahidi huo bungeni atakuwa amenisaidia, lakini usinichukulie kwamba napiga chenga swali lako,” alisema Pinda.
Naye Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), aliuliza kwa nini kitengo cha maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu huchelewa katika maafa.
Akijibu swali hilo, Pinda Serikali imeweka mfumo mzuri unaowezesha shughuli za maafa kufikiwa kwa haraka tofauti na mbunge anavyohoji.
“Kila wilaya ina kamati ya maafa na mkuu wa wilaya ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo, kwa hiyo maafa yanapotokea mahala popote kamati ile inakuwa ya kwanza kufika, baadaye sisi tunapata taarifa kutoka kwenye ile kamati,” alisema.
Pinda alisema kitengo cha maafa katika ofisi yake hutoa msaada tatizo linapokuwa kubwa vingine kamati hiyo inalimaliza.
“Naomba ieleweke kuwa si kila maafa ofisi yangu inatoa msaada kwani misaada mingine hufanyika katika ngazi ya wilaya au mkoa kwa kushirikisha wadau mbalimbali,’’ alisema Pinda.
Akizungumzia Serikali kuhamia Dodoma, Pinda alisema bado haijabadili nia yake ya kuhamishia makao makuu ya Serikali mjini Dodoma.
Kuhamishia makao makuu ya nchi mjini hapa ni jambo la msingi lisilokwepeka ndiyo maana Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali, alisema.
Kwa mujibu wa Pinda, kukamilika kwa sheria hiyo kutaweza kuweka utaratibu mzuri wa kuhamia Dodoma ikiwamo kuainisha vivutio mbalimbali.
Pinda alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM) aliyetaka kujua ni lini Serikali itawasilisha bungeni muswada wa sheria ya kuhamisha makao makuu ya Serikali Dodoma.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF), alitaka kujua sababu za Serikali kufanya uamuzi wa kubadisha alama za ufaulu na kusababisha matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.
Sakaya alitaka kujua Serikali imechukua hatua gani kwa watumishi waliamua kubadili viwango vya madaraja na hivyo kusababisha matokeo hayo kufutwa.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema kwa sasa hawezi kusema chochote kwa vile tume iliyoundwa kuchunguza suala hilo haijamaliza kazi yake na kumtaka mbunge huyo kusubiri.

0 comments:
Post a Comment