BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KISHINDO KIZITO RASIMU KATIBA MPYA.

MTANZANIA.
HATIMAYE Tanzania imeandika historia mpya, baada ya kutangazwa kwa rasimu ya Katiba mpya ambayo imetoa mapendekezo maz
ito.

Akitangaza kwa mara ya kwanza rasimu hiyo mjini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Jaji Joseph Warioba, alisema miongoni mwa mapendekezo mazito yaliyotolewa ni pamoja na kuanzishwa kwa Serikali za Shirikisho, Tanzania Bara na Mapinduzi Zanzibar. 


Alisema rasimu hiyo, imependekeza Spika wa Bunge na naibu wake kutokuwa wabunge wala viongozi wa vyama vya siasa.

Katika rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema imependekeza Rais aunde serikali ndogo iliyo na mawaziri wasiozidi 15 na mawaziri hao wasiwe wabunge. Alisema mawaziri hao, hawatahudhuria vikao vya Bunge, isipokuwa endapo watahitajika kutoa ufafanuzi kwenye kamati za Bunge tu.


IDADI YA WABUNGE

Jaji Warioba, alisema rasimu hiyo imependekeza jumla ya wabunge wawe 75, ambapo 50 watatoka Tanzania Bara, 20 Tanzania Visiwani na watano watatoka kundi maalum ambao watateuliwa na Rais kwa ajili ya kuwatetea walemavu.

BUNGE

Alisema kwa upande wa wabunge, watakuwepo wa aina mbili, wa kuchaguliwa na wachache wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha watu wenye ulemavu.

Alisema kama ikitokea mbunge atafukuzwa na chama cha siasa, atabaki kuwa mbunge, lakini akihama chama atapoteza ubunge wake.

Alisema ukomo wa ubunge, unapendekezwa uwe vipindi vitatu vya miaka mitano mitano, hata hivyo wananchi wanaweza kumuondoa mbunge wao kabla ya mwisho wa kipindi chake.

Katika rasimu hiyo, pia imependekezwa kusiwepo na uchaguzi mdogo, isipokuwa kama nafasi yake ni ya mgombea binafsi na kama ni ya chama cha siasa, basi nafasi hiyo ijazwe na mtu kutoka chama chake.

MGOMBEA BINAFSI

Katika jambo ambalo lilikuwa likisubiriwa na Watanzania wengi, la mgombea binafsi, Jaji Warioba alisema imependekezwa kila mwananchi awe huru kugombea nafasi ya ngazi yoyote, hata ya urais kwa nafsi yake.

Alisema tume yake, inapendekeza mgombea urais awe na umri wa miaka 40 na kuendelea.

Alisema uchaguzi wa Rais, utakuwa kama ilivyo sasa na kuendelea, yaani mgombea urais atakuwa na mgombea mwenza na atatangazwa na Tume huru ya Uchaguzi, baada ya kupata kura zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa.

Alisema matokeo ya uchaguzi wa Rais, yanaweza kulalamikiwa mahakamani, lakini siyo kila mtu anayeweza kufungua kesi, bali wanaoruhusiwa ni wagombea urais na Mahakama ya Juu pekee ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza malalamiko hayo na iamriwe ndani ya mwezi mmoja.

Rais aliyeshinda ataapishwa siku 30 tangu alipotangazwa kuwa mshindi au kuthibitishwa na mahakama.

KINGA YA RAIS

Kuhusu kinga ya Rais, Jaji Warioba alisema imependekezwa Rais abaki na kinga kama ilivyo sasa na anaweza kushtakiwa na Bunge kama ilivyo Katiba ya sasa.

MADARAKA YA RAIS

Kwa upande wa madaraka ya Rais, Jaji Warioba alisema yataendelea kubaki kama ilivyo sasa, kwa uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu, pia ashirikiane na taasisi na vyombo vingine katika uteuzi.

Mfano uteuzi wa mawaziri na manaibu,Rais atateua na Bunge litathibitisha.

Kuhusu Jaji Mkuu na naibu wake, Rais atawateua kutokana na majina ya watu waliopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama, baada ya hapo Bunge litathibitisha.

ULINZI NA USALAMA

Jaji Warioba, alisema Tume imependekeza kianzishwe chombo kipya kitachoitwa Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa, ambalo kati ya majukumu yake, itakuwa ni kumshauri Rais kuhusu uteuzi wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Makatibu Wakuu

Alisema rasimu ya Katiba mya, imependekeza Rais aendelee kuwateua makatibu wake na manaibu wake kutokana na mapendekezo ya utumishi wa umma.

TUME YA UCHAGUZI

Katika kipengele hicho, Jaji Warioba alisema tume imependekeza jina la Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), libadilishwe na iitwe Tume Huru ya Uchaguzi.

Kutokana na hali hiyo, wajumbe wa tume hiyo sifa zao ziwekwe kwenye Katiba na majina ya waombaji wa nafasi hizo yatachambuliwa na kamati ya uteuzi ambayo Mwenyekiti wake atakuwa Jaji Mkuu na wajumbe wengine sita.

Pia tume hiyo iwe huru isimamie masuala ya uchaguzi kura ya maoni, usajili wa vyama vya siasa.

MAHAKAMA

Rasimu hiyo, imependekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court), majaji wa mahakama ya juu na mahakama ya rufani watateuliwa na Rais, baada ya kupendekezwa na tume ya utumishi wa mahakama.

MUUNDO WA MUUNGANO

Jaji Warioba, aliongeza kuwa orodha ya Mambo ya Muungano yawe saba badala ya 22 yaliyopo sasa. Yaliyopendekezwa ni pamoja na Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya siasa, Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya Kodi yatakonayo na mambo ya Muungano.

IBARA

Alisema Katiba ya sasa ina ibara 152, lakini tume imepokea mapendekezo Katiba ijayo iwe na ibara 240.

MISINGI MIKUU YA TAIFA

Uhuru, haki, udugu na amani, hivyo tume imependekeza misingi mingine mitatu na kufanya misingi hiyo kuwa saba, ambapo iliyoongezwa ni pamoja na usawa, umoja na mshikamano.

TUNU ZA TAIFA

Katiba ya sasa haina sehemu inayoelezea tunu za taifa (National Values), tume imependekeza tunu zifuatazo ziwe kwenye Katiba ijayo, ambazo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha yetu ya taifa ya Kiswahili.

MALENGO YA KITAIFA

Tume ilipozunguka nchi nzima wananchi walilalamikia malengo ya taifa na walitaka katiba ijayo ioneshe dira ya taifa. Rasimu hiyo inaelezea malengo ya serikali yatakuwa ni mwongozo kwa serikali, bunge, mahakama, vyama vya siasa, taasisi na mamlaka nyingine na kwa kila mwananchi katika matumizi au kutafsiri masharti ya katiba au sheria nyingine za nchi.

MAADILI YA VIONGOZI

Jaji Warioba, alisema tume yake imependekeza Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na miiko ya viongozi yawekwe kwenye Katiba, Sekretarieti ya Maadili ya Umma, ikipendekezwa kubadilishwa jina na tume yenye mamlaka makubwa ya kusimamia maadili ya viongozi wanaovunja miiko ya uongozi.

URAIA

Alisema tume, imependekeza kwa kutaja raia wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na haki zake.

MFUMO WA UTAWALA

Imependekezwa Tanzania iendelee kuwa na mfumo wa Jamhuri, kwa maana ya nchi inayoongozwa na rais mtendaji ambaye ni mkuu wa nchi, kiongozi wa serikali na amiri jeshi mkuu.

BAADHI YA MAMBO AMBAYO HAYAMO KWENYE RASIMU

Serikali ya Majimbo, Mahakama ya Kadhi, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Serikali za Mitaa na Uraia wa Nchi mbili.

MAMBO YALIYOTUPWA
MAJIMBO
Jaji Warioba, alisema Tume imependekeza jimbo litakuwa na wabunge wawili, yaani mwanamke na mwanamume, ili kuleta usawa katika jamii.

Tume imetupilia mbali maombi ya serikali za majimbo, baada ya kuchambua kwa undani na kuona athari zake.

Alisema iliona baada ya kupendekeza muundo wa Muungano wa Serikali Tatu, ilionekana kuongeza ngazi nyingine ya serikali ingeleta gharama kubwa.

Alisema katika ziara zao mikoani, Tume ilibaini malalamiko ya upendeleo baadhi ya maeneo, ukabila, ukanda, udini, hivyo kuzigawa rasilimali za taifa kikanda na hivyo kuleta tofauti kubwa ya maendeleo katika nchi.

MAHAKAMA YA KADHI

Akitoa mfano, Jaji Warioba alisema Tume imeona Mahakama ya Kadhi ya Zanzibar ilivyo na si suala la Muungano.

Alisema suala hilo, litashughulikiwa na washirika wa Muungano na kupendekeza kuwa inaweza ikaendelea kuwepo nchini, lakini isiingizwe kwenye katiba kama ilivyo visiwani Zanzibar.

“Hii ndiyo mchakato wa rasimu yetu ya Katiba ijayo, nawashukuru wananchi, kwani ilikuwa siyo rahisi kufanya kazi hiyo, jumla ya wananchi 1,365,337 walijitokeza katika mikutano yetu ambapo wananchi 333,537, makundi maalum 160 na viongozi 43 walitoa maoni,” alisema Jaji Warioba.

DK BILAL

Akizindua rasimu hiyo, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, aliipongeza tume hiyo kwa kazi ngumu waliyofanya kwa uadilifu kufanikisha mchakato huo hatua ya awali.

Alisema ni vyema wananchi wakajitokeza kwa wingi katika Mabaraza ya Matiba na kuichambua rasimu hiyo, kisha kuondoa kasoro zilizojitokeza.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: