HABARILEO.
RASIMU ya Katiba imetolewa na Tume ya
marekebisho ya katiba na miongoni mwa mambo yanayopendekezwa ni kuundwa
kwa Serikali tatu pamoja na kuruhusiwa kwa mgombea binafsi. Uzinduzi wa
rasimu hiyo ya katiba umefanyika jana, Dar es Salaam na kwa uamuzi huo
wa tume sasa Tanzania itakuwa na mara
is watatu ambao ni rais wa serikali
ya shirikisho, rais wa Tanzania Bara na rais wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (SMZ).
Muundo wa Muungano sasa Alisema tume
yake inapendekeza serikali tatu, kwani wananchi ambao walitoa
mapendekezo hayo ni wengi kuliko makundi ya waliotaka serikali moja,
serikali nne, muungano wa mkataba na serikali mbili.
“Sababu zao zilikuwa nzito lakini pia
kulikuwa na changamoto nyingi na nzito.Pamoja na maoni ya wananchi, tume
ilirejea sababu za kupendekeza muundo huu zilizotolewa na tume
zilizopita na tafiti zilizofanywa na tume kuhusu aina mbalimbali za
muungano,” alisema Warioba.
Alisema pamoja na maoni ya wananchi,
tume ilirejea sababu za kupendekeza muundo huo zilizotolewa na tume
zilizopita na tafiti zilizofanywa na tume kuhusu aina mbalimbali za
muungano.
“Baada ya yote hayo tume hatukuwa na
jinsi zaidi ya kufikia uamuzi wa kupendekeza mfumo wa serikali tatu,
yaani serikali ya shirikisho, serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar,” alisema Warioba.
Hivyo kutakuwa na serikali ya muungano,
serikali ya Tanzania Bara, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Shughuli
za Muungano zitatekelezwa na kusimamiwa na serikali ya muungano, Bunge
la Jamhuri ya Muungano na mahakama yake.
Kutokana na uamuzi huo wa tume, muundo,
madaraka na mambo mengine ya kiuendaji yahusuyo serikali ya Bara na ile
ya Zanzibar yataainishwa katika katiba za washirika hao wa muungano.
Katika rasimu hiyo serikali ya muungano
itakuwa ndio chombo chenye mamlaka ya utendaji, Bunge litakuwa na
mamlaka ya kutunga sheria kwa mambo ya muungano na mahakama kitakuwa
chombo cha kutoa haki katika muungano huo.
Kwa mujibu wa rasimu hiyo, serikali ya
Bara itakuwa na mamlaka juu ya mambo yasiyo ya muungano yanayohusu eneo
hilo na SMZ, pia itakuwa na mamlaka ya juu yasiyo ya muungano yaliyoko
eneo lake. “Washirika wa muungano watakuwa na hadhi na haki sawa ndani
ya muungano na watatekeleza.”
Washirika hao wanaruhusiwa kuanzisha
mahusiano au ushirikiano na jumuiya au taasisi yoyote ya kikanda au
kimataifa kwa mambo yaliyo chini yake kwa mujibu wa katiba yake. Katika
eneo hilo inapendekezwa kuwa mshirika wa muungano anaweza wakati wa
kutekeleza majukumu yake kuomba ushirikiano kutoka serikali ya muungano
kwa ajili ya kufanikisha uhusiano na jumuiya au taasisi za kimataifa au
kikanda na serikali ya muungano inaweza kutoa ushirikiano kwa mshirika
huyo kwa namna itakavyohitajika.
Inapendekezwa kila mshirika wa muungano
atateua waziri mkazi atakayeratibu na kusimamia uhusiano baina ya
serikali za washirika na kati ya serikali ya mshirika na serikali ya
muungano, mawaziri hao wakaazi watafanya kazi zao na ofisi zao zitakuwa
makao makuu ya serikali ya muungano na watakuwa kiungo kati ya serikali
ya muungano na serikali mshirika Tume hiyo pia imepunguza mambo ya
muungano kutoka 22 hadi saba ambayo ni katiba na mamlaka ya Jamhuri ya
muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama wa Jamhuri, uraia na uhamiaji,
sarafu na benki kuu, mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa, ushuru wa
bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya muungano.
Katika muundo huo serikali ya muungano
itapata mamlaka yake kutoka kwa wananchi wa pande zote na serikali za
serikali washirika nazo zitachaguliwa na wananchi kupitia uchaguzi wa
kidemokrasia utakaosimamiwa na tume za uchaguzi za nchi zao. Viongozi
wote hao wanalazimishwa na katiba hiyo kulinda na kuimarisha muungano.
Mgombea binafsi Jaji Joseph Warioba
alisema tume yake imezingatia maoni ya wananchi ambao walipendekeza haki
zote ziimarishwe na kusiwe na vikwazo vya lazima. Kutokana na maoni
hayo, Warioba alisema tume yake inapendekeza kwamba vikwazo vilivyowekwa
kuzuia mgombea huru viondolewe, kwa maana nyingine tume inapendekeza
mgombea binafsi aruhusiwe.
Kwenye rasimu hiyo ya katiba, pia haki
mpya zimeingizwa ambazo ni haki ya mtoto, haki za watu wenye ulemavu,
haki za wanawake, haki za wazee, haki za makundi madogo katika jamii,
haki ya elimu na kujifunza, haki ya kupata habari, haki na uhuru wa
habari na vyombo vya habari. Mfumo wa utawala Rais wa shirikisho ndiye
atakayekuwa amiri jeshi mkuu na yeye atakuwa na makamu mmoja.
Rais huyo atakuwa ndiye taswira ya Muungano wa Tanzania. Pia kutakuwa na Bunge la Muungano, na mahakama ya Muungano.
Makamu wa Rais ndiye atakayekuwa
msaidizi mkuu wa Rais.
Tume hiyo imependekeza umri wa kugombea urais
uendelee kuwa miaka 40 kwa vile idadi kubwa ya watu waliotoa maoni
walipendekeza umri huo. Kwenye mapendekezo hayo, Warioba alisema mgombea
wa nafasi ya rais atatangazwa kuwa mshindi iwapo atakuwa amepata kura
zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa.
Inapendekezwa kuwa uchaguzi wa rais
itakuwa kama ilivyo sasa isipokuwa tume hiyo imependekeza mgombea urais
aweza kupendekezwa na chama cha siasa au kuwa mgombea huru.
Katika rasimu hiyo tume hiyo
imependekeza kuwa matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kulalamikiwa
mahakamani. ‘lakini sio kila mtu anaweza kufungua kesi, wanaoweza
kufungua kesi ni wagombea urais.’
Pia tume hiyo imependekezwa kuundwa kwa
mahakama ya juu (supreme court) ambako wagombea urais wanaweza kufungua
kesi na ni mahakama hiyo tu itakuwa na mamlaka na uwezo wa kusikiliza
malalamiko kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais na shauri lazima liamuliwe
ndani ya siku thelathini.
“Rais aliyeshinda ataapishwa siku 30
tangu alipotangazwa kuwa mshindi au kuthibitishwa na mahakama,” alisema
Warioba. Madaraka ya Rais Warioba alisema katika eneo hilo tume
imependekeza rais abaki na madaraka ya uteuzi wa viongozi wa ngazi za
juu. Lakini imependekezwa rais ashirikiane na taasisi na vyombo vingine
katika uteuzi huo.
Alisema uteuzi wa mawaziri na manaibu
waziri Rais atateua na Bunge lithibitishe, lakini kuhusu jaji mkuu na
naibu jaji mkuu ambaye tume imependekeza cheo hicho kiwepo, majina ya
watu waliopendekezwa na tume ya utumishi wa mahakama na baada ya hao
bunge litathibitisha.
Kwa upande wa makatibu wakuu watateuliwa na rais
kutokana na mapendekezo ya tume ya utumishi wa umma.
Kwa upande wa wakuu wa vyombo vya ulinzi
na usalama, inapendekezwa kuwa kianzishwe chombo kipya kitakachoitwa
baraza la ulinzi na usalama wa taifa ambalo kati ya majukumu yake
itakuwa ni kumshauri rais kuhusu uteuzi wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na
usalama.
Kinga ya rais imependekezwa na tume hiyo
ibaki na anaweza kushtakiwa na Bunge kama ilivyo katiba ya sasa. Idadi
ya mawaziri Katika mapendekezo hayo imependekezwa kuwa rais aunde
serikali ndogo iliyo na mawaziri wasiozidi 15 na mawaziri hao wasiwe
wabunge.
Mawaziri hao hawatahudhuria vikao vya
Bunge isipokuwa watahitajika kutoa ufafanuzi kwenye kamati za Bunge.
Bunge Kwa upande wa Bunge, Warioba alisema inapendekezwa wabunge wa aina
mbili.
Yaani kutakuwa na wabunge wa kuchaguliwa
na wabunge wachache wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha watu wenye
ulemavu. Tume imependekeza mbunge akifukuzwa na chama cha siasa abaki
kuwa mbunge lakini akihama chama atapoteza ubunge wake.
Katika eneo hilo pia rasimu inapendekeza
kuwepo ukomo wa ubunge ambao ni vipindi vitatu vya miaka mitano mitano
lakini wananchi wanaweza kumwondoa mbunge wao kabla ya mwisho wa kipindi
iwapo hawaridhiki na utendaji wake wa kazi.
Pia imependekezwa kusiwepo na uchaguzi
mdogo isipokuwa kama nafasi inayokuwa wazi inatokana na mbunge huru
ndipo uchaguzi mdogo kujaza nafasi hiyo utafanyika, “lakini kama nafasi
ikiwa wazi kutokana na mbunge wa chama cha siasa basi nafasi hiyo ijazwe
na mtu kutoka chama hicho.”
Kwa upande wa spika na naibu spika,
inapendekezwa wasitokane na wabunge na wasiwe viongozi wa vyama vya
siasa. Tume ya uchaguzi Jaji Warioba alisema tume yake imefanya
uchambuzi wa maoni ya wananchi katika eneo hilo na imependekeza jina la
tume liwe Tume Huru ya Uchaguzi.
Tume pia imependekeza sifa za wajumbe
wa tume hiyo huru ziwekwe kwenye katiba na watapatikana kutokana
miongoni mwa watu wenye sifa zilizoainishwa ndani ya katiba kwa kuomba.
Alisema majina ya waombaji
yatachambuliwa na kamati ya uteuzi ambayo mwenyekiti wake atakuwa jaji
mkuu na wajumbe wengine sita ambao ni majaji wakuu wa nchi washirika,
spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano na maspika wa mabunge ya nchi
washirika na mwenyekiti wa tume ya haki za binadamu.
Alisema kamati hiyo itapendekeza majina
ya watu wnaofaa kwa rais ambaye atateua mwenyekiti, makamu mwenyekiti na
wajumbe wengine.
“Bunge litathibitisha uteuzi wao,
wabunge na viongozi wengine wa kisiasa hawatakuwa na sifa za kuwa
wajumbe wa tume ya uchaguzi.” Katika eneo hilo imependekezwa kuwa tume
huru ya uchaguzi isimamie masuala ya uchaguzi, kura ya maoni na usajili
wa vyama vya siasa.
Kuhusu mahakama imependekezwa kuwa
majaji wa mahakama ya juu (supreme court) na mahakama ya rufaa
watateuliwa na rais baada ya kupendekezwa na tume ya utumishi wa
mahakama.
Benki Kuu Kwa kuwa tume imependekea
muungano wa shirikisho, kutokana na uzito wa maoni ya wananchi, hivyo
kutakuwa na benki kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayokuwa na
wajibu wa kusimamia masuala ya sarafu na fedha za kigeni na benki za
washirika wa muungano.
Pia inapendekezwa kuwepo na benki
zitakazokuwa na jukumu la kutunza akaunti ya fedha za serikali za kila
mshirika wa Muungano na kuzisimamia benki za biashara katika mamlaka
zao. Baraza la mawaziri Katiba inapendekeza makamu wa rais atatoka
upande mwingine wa muungano ambako hatoki rais wa muungano.
Mgombea binafsi anaruhusiwa kumteua
makamu wa rais hata kama mtu huyo alishashika wadhifa wa urais wa
Zanzibar au wa Tanzania bara.
Ikitokea rais wa bara au wa SMZ
akateuliwa kuwa makamu wa rais atalazimika kuacha wadhifa wake wa awali
ili ashike wadhifa huo wa juu katika Jamhuri.
Kwa muundo huo baraza la
mawaziri sasa litaundwa na makamu wa rais wa Jamhuri ya muungano,
mawaziri wa serikali ya muungano, mwanasheria mkuu wa serikali
atahudhuria vikao vya baraza hilo lakini hatakuwa na haki ya kupiga
kura.
Baraza hilo la mawaziri ndilo
litamshauri rais na bunge na mahakama havitakuwa na uwezo wa kuchunguza
jambo ambalo limepitishwa na baraza la mawaziri.
Mambo ya Jumla Katiba iliyopendekezwa
ina ibara 20 kutoka za sasa ambazo ni 153. Misingi mikuu ya taifa
iliyoko kwenye katiba hiyo ni saba kutoka minne ya awali ambayo ni
uhuru, haki, udugu, usawa, umoja, amani na mshikamano. Tunu za taifa
katika katiba hiyo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi,
uwajibikaji, na kiswahili.
Kwenye katiba hiyo pia kuna malengo ya
taifa ambayo yatakuwa ni mwongozo kwa serikali, bunge, mahakama, vyama
vya siasa, taasisi na mamlaka nyingine kwa kila mwananchi katika
matumizi au kutafsiri masharti ya katiba au sheria nyingine za nchi. Kwa
msingi huo, tume hiyo imependekeza malengo makuu ya taifa yapanuliwe
kwa mpango wa kuonyesha malengo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii,
kiutumaduni, kimazingira, na sera ya mambo ya nje.
Vyombo vya kikatiba katika rasimu hiyo
ni tume ya uhusiano na uratibu wa serikali, baraza la mawaziri, kamati
maalum ya makatibu wakuu na sekretarieti ya baraza la mawaziri, baraza
la ulinzi na usalama la taifa, tume huru ya uchaguzi, tume ya utumishi
wa mahakama, tume ya utumishi wa umma, tume ya maadili ya viongozi na
uwajibikaji na tume ya haki za binadamu na utawala bora.
Katika katiba hiyo inapendekezwa kuwa
maadili ya viongozi wa umma pamoja na miiko ya uongozi yawekwe kwenye
katiba na tume imependekeza sekretarieti ya maadili ibadilishwe kuw
atume yenye mamlaka makubwa ya kusimamia maadili ya viongozi wanaovunja
miiko ya uongozi.
0 comments:
Post a Comment