Sasa ni
dhahiri kuwa maisha ya kiongozi wa zamani wa nchi hii, Nelson Mandela
yamo hatarini kutokana na kwamba anaishi kwa msaada wa mashine,
imethibitishwa na mmoja wa wazee wa ukoo wa kiongozi huyo.
Binti yake mkubwa Makaziwe naye amethibitisha hilo, akisema hali ni mbaya na chochote chaweza kutokea.
"Naweza kusisitiza hilo, kwamba Tata (baba) hali yake ni mbaya sana,
chochote chaweza kutokea, lakini nataka nisisitize tena, kwamba ni Mungu
tu ndiye anajua muda wa kuondoka,” alikiambia kituo cha utangazaji cha
SAFM jana.
Hali hiyo inayotia mashaka imesababisha hata Rais Jacob Zuma afute
safari yake ya Msumbiji ambako alipanga kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Ndiyo, anatumia mashine kupumua,” Mzee Napilisi Mandela aliiambia
AFP muda mfupi baada ya kumtembelea Mandela hospitalini juzi. “Hali ni
mbaya, lakini tutafanyaje.”
Zuma alifuta safari yake iliyokuwa ifanyike jana baada ya “kubaini,
kwamba kiongozi huyo wa zamani hali yake bado ni mbaya,” taarifa kutoka
Ofisi ya Rais ilisema.
Wakati huo huo, kiongozi wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu Ban Ki-moon
alisema juzi kwamba dunia yote inamwombea Mandela wakati huu ambapo
anapigania maisha yake.
Ban alimwita Mandela “mmoja wa mashujaa wa karne ya 20” katika hafla
ya kuadhimisha miaka 50 ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU (sasa Umoja
wa Afrika-AU) iliyofanyika New York, Marekani, ambao uliongoza
mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.
“Najua fikra na maombi yetu viko na Nelson Mandela, familia yake na
wanaompenda, Waafrika Kusini wote na watu wote duniani ambao wamekuwa
wakivutiwa na matendo yake maishani na kuwa mfano wa kuigwa,” alisema
Ban.
“Hebu nasi leo tuoneshe dhamira ya uwajibikaji wa dhati katika
kuhakikisha tunaboresha maisha na fursa za Waafrika wote,” alisema
Katibu Mkuu wa UN.
Zuma alimtembelea Mandela hospitalini juzi saa nne usiku na kumkuta
akiwa bado na hali mbaya, msemaji wa Rais, Mac Maharaj alisema.
“Rais Zuma alizungumza na madaktari ambao bado wanaendelea kufanya
kila linalowezekana kuokoa maisha yake ... ameamua kufuta safari yake ya
Maputo kesho (jana), ambako alitakiwa kuhudhuria Mkutano wa Uwekezaji
katika miundombinu kwa nchi za Kusini mwa Afrika wanachama wa SADC.”
Mandela (94) alilazwa katika hospitali ya moyo ya Medi-Clinic iliyoko
hapa Juni 8 kutokana na kuibuka upya kwa matatizo ya mapafu yake.
Katika hatua nyingine, mjukuu wake, Mandla Mandela, amekanusha kuwapo
kwa mvutano kati yake na shangazi yake, Makaziwe, kwa mujibu wa taarifa
zilizotolewa jana.
Magazeti yaliripoti juzi kwamba anadaiwa alijitoa kwenye kikao cha familia kilichofanyika Qunu Jumanne.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, anadaiwa kuhamisha makaburi ya watoto
watatu wa Mandela kutoka Qunu hadi Mvezo mwaka 2011, bila hata
kushauriana na familia.
Iliripotiwa pia kuwa familia hiyo ilikuwa ikitaka watoto hao, Makgatho, Thembekile na Makaziwe, warudishwe Qunu.
“Chifu Zwelivelile (Mandla) hana suala lolote na mtu mwenye mamlaka
ya kurudisha Qunu kaburi lolote au makaburi yote,” msemaji wa Mandla,
Freddy Pilusa alikaririwa akiiambia The Star jana.
“Mvezo ndiko mahali ilikozaliwa familia ya Mandela na kimila ndiko
nyumbani kwao, na hivyo ndiko iliko historia ya familia hiyo.” Alisema
Mandla hawezi sasa kuzungumzia lolote kuhusu mipango ya maziko ya babu
yake.
Waganga wa jadi wa Limpopo jana walifanya matambiko katika ofisi za ANC zilizoko Polokwane kumwombea Mandela.
Mwenyekiti wa Timu kazi ya ANC Limpopo, Falaza Mdaka, alisema waganga
hao waliomba kufanyia tambiko lao katika ofisi hizo wakisema ndiko
kulikuwa ‘nyumbani’ kwa Mandela na kuongeza kuwa alikuwa mtu wa aina
yake na dunia bado inamhitaji.
Waganga hao waliimba nyimbo za mapambano na kuchoma ubani, wakiwaomba
wahenga kumponesha kiongozi huyo anayependwa na nchi nzima.
“Mandela
anahitaji msaada wa wahenga,” alisema mmoja wa waganga hao, Sylvester
Hlathi.
About mtanda blog
Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
0 comments:
Post a Comment