BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BUNGE LIBEBE LAWAMA TOZO YA KODI YA LINE ZA SIMU


Utamaduni wa taasisi nyingi hapa nchini wa kukataa kuwajibika pale makosa yanapofanyika, badala yake lawama zikaelekezwa mahali pengine pasipohusika, sasa unaonekana kama jambo la kawaida. Ni utamaduni hasi wa kutokubali kuwajibika kwa jambo lolote linalokwenda kombo, badala yake kuwanyooshea vidole watu wengine, tena ambao hawahusiki katika kusababisha matatizo hayo.

Ni utamaduni huo ambao umefifisha dhana ya uwajibikaji katika nchi yetu. Ni utamaduni unaojenga mazingira ya mtu kutaka sifa pale mambo yanapokwenda vizuri, hata kama hukuchangia lolote katika kuleta hali hiyo ya mafanikio. Yanapotokea matatizo, hulka ya wengi ni kuruka kimanga na kusema sio wao.

Tunaweza kusema kwamba hakuna chombo kilichoathiriwa na utamaduni huo hapa nchini kama Serikali. Mhimili huo wa dola ndio umefanywa kama gunia la kufanyia mazoezi ya ndondi kwa kugeuzwa kisingizio cha kila tatizo linalojitokeza. Hapana ubishi kwamba yapo matatizo yanayosababishwa na mhimili huo.

Lakini, aghalabu mhimili huo umekuwa hautendewi haki, kwani hata watendaji wake wanapohusika kufanya uamuzi fulani, wanakuwa wa kwanza kuelekeza lawama kwa mhimili huo pindi uamuzi walioufanya unatoa matokeo yasiyokubalika.

Mifano ni mingi, lakini kutokana na ufinyu wa nafasi katika safu hii, tutatoa michache tu ya matukio ya hivi karibuni. Hatua ya chama tawala (CCM), ambacho juzi kilitoa taarifa ya kuilaumu Serikali kwa kuweka tozo ya Sh1,000 kwa kila laini ya simu ya kiganjani imewaacha wananchi wengi wakiwa midomo wazi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba chama hicho kilikuwa nyuma ya Serikali katika kufanya uamuzi wa kuweka tozo hiyo. Baada ya tozo hiyo kupingwa na wananchi ndipo chama hicho kilipoamua kuruka kimanga kwa malengo ya kisiasa.

Yafaa tukumbuke hapa kwamba tozo hiyo ilipitishwa na Bunge katika kikao cha Bajeti mwezi uliopita wakati pia liliporidhia Sheria ya Fedha. Serikali ilipeleka mapendekezo kuhusu tozo hiyo na ilikuwa juu ya Bunge kuyakubali au kuyakataa. Zaidi ya theluthi mbili ya wabunge wanatoka CCM na ukweli ni kwamba ndio haohao waliopitisha Bajeti ya Serikali na mapendekezo yake kuhusu tozo ya laini za simu. Hatua ya chama hicho kuilaumu Serikali baada ya tozo hiyo kupingwa na wananchi ni kutoitendea haki katika kutaka kujinusuru kisiasa.

Utamaduni wa kutowajibika wakati matatizo yanapotokea pia jana ulidhihirishwa na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba aliposema wizara yake haikubaliani na tozo hizo. Inashangaza kuona viongozi wa wizara hiyo wanapingana na dhana ya uwajibikaji wa pamoja, kwani tozo hiyo imewekwa na Serikali ambayo wao ni watumishi wake. Ni mwendelezo wa utamaduni wa kuruka kimanga hata kama nao walishiriki katika chombo kilichoamua kuanzisha tozo hiyo inayopingwa na wananchi.

Ni utamaduni ambao sasa umejikita katika jamii yetu. Undumilakuwili huo tunaoshuhudia katika suala la tozo ya laini za simu ndio tulioshuhudia katika matukio mengi huko nyuma, likiwamo la Sheria ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii ambayo ilipitishwa na Bunge kwa msukumo wa idadi kubwa ya wabunge wa CCM, lakini wakaruka kimanga kwa malengo ya kisiasa baada ya sheria hiyo kupingwa kila kona ya nchi. Ndio maana tunasema katika hili la tozo ya laini za simu, Bunge ndilo libebe lawama badala ya Serikali.

Source:Mwananchi
Share on Google Plus

About Anonymous

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: