Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba.
KWA mliotaka msimamo wangu juu ya kauli ilinukuliwa
jana tarehe 18 Julai 2013 na Gazeti la Majira kwamba Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba kwamba “Mnyika anaangalia
upepo unakoelekea, akiona watu wanalalamika ndipo anaongea namsihi aache
kufanya siasa katika jambo hili”, naomba kutumia mtandao huu kutoa majibu ya
ujumla kwa maswali na masuala yote kama ifuatavyo.
Nieleze kwamba sitaacha kufanya siasa kwenye jambo
hili mpaka kodi hiyo itakapofutwa kuwawezesha wananchi wa kip
ato cha chini
kubaki na fedha walau kidogo kwa maendeleo.
Sitaacha kufanya siasa kwa sababu ndio kazi yangu
ambayo wananchi walinichagua kuifanya ya kuwawakilisha na kuisimamia Serikali
ambayo yeye Makamba ni sehemu yake. Sitaacha kufanya siasa kwa sababu Mwalimu
Nyerere alisema ili nchi yetu iendelee inahitaji watu, ardhi, siasa safi na
uongozi bora.
Ambacho sitafanya ni siasa chafu kama hizo ambazo
Makamba amefanya za kusema uongo, kwa kuwa naamini anafahamu kabisa kwamba
sijaanza kuongea kuhusu suala hili baada ya malalamiko ya wananchi bali jambo
hili nilianza kulishughulikia bungeni mara baada ya Waziri wa Fedha kuwasilisha
jedwali la marekebisho la kuanzisha kodi lukuki za simu ikiwemo hii.
Katika
mchango wangu bungeni, nieleza kwamba muswada huo wa sheria ya fedha kwa
kupandisha kodi kwenye mafuta na simu ni ‘muswada wa majanga ya kuwaongezea
mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.
Aidha, sikuishia kusema tu kwa niaba ya wananchi
bali nilichukua hatua kwa mujibu wa kanuni za Bunge nami kuwasilisha jedwali la
marekebisho ya kupinga kodi ya umiliki wa kadi za simu pamoja na kodi nyingine
zote zenye kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi sio kwenye sekta ya
mawasiliano bali pia kwenye sekta zingine ikiwemo sekta ndogo (sub sector)
nyeti ya mafuta.
Mlioniuliza kwa SMS katika simu na kwenye mitandao
ya kijamii sasa ni wakati wa Makamba kuhojiwa kwa njia hizo hizo kwa kuwa yeye
ni sehemu ya Serikali na Serikali ndiyo ambayo iliingiza suala hili kwa mara ya
kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge kupitia hotuba ya Bajeti Serikali na ikalirudia
kuliingiza kupitia jedwali la marekebisho ya Sheria ya Serikali; ni wakina nani
hasa kwa majina ndani ya Serikali na Bunge walioingiza kodi hii? Na ni wakina
nani hasa waliopigia kura ya ndio kuipitisha ?.
Aidha, amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la leo
tarehe 19 Julai 2013 akieleza kwamba hakubaliani na suala hili na kupita kwake
ilikuwa na kuzidiwa nguvu.
Hivyo, ataje kwa majina hayo waliozidi nguvu
serikali kinyume na matakwa yake. Amenukuliwa akisema pia kwamba anajua kuwa
suala hili haliwezi kutekelezwa na kwamba ni lazima litabadilishwa kwa
kuangalia eneo lingine la kutoza kodi.
Ni vizuri akahojiwa, ikiwa huo ni
msimamo wa Serikali; mwenye mamlaka ya kusitisha kodi hiyo ni nani na kwanini hajitokezi
kutoa agizo la kusitisha wakati maandalizi yakiendelea ya kupeleka muswada
bungeni wa kuifuta kabisa kodi hiyo katika mkutano ujao ?.
Wakati Naibu Waziri akisema hayo, Waziri wa Fedha Dk
William Mgimwa katika Serikali hiyo hiyo yeye ametoa kauli tofauti siku hii hii
ya leo ambapo kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania amewataka watumiaji wa mitandao
ya simu nchini na watanzania kwa ujumla kuwa na subira kuhusu tozo ya sh 1000
kwa mwezi kwa kila laini ya simu za kiganjani.
Na kwa kuwa amesema kwamba Serikali inaendelea
kupokea maoni kutoka kwa wadau, natoa mwito kwa wananchi kumtumia maoni kupitia
namba zake za simu za mkononi 0754/0684-765644.
Aidha, ni vizuri aeleze subira hiyo ivutwe mpaka
lini? Na ni wakina nani hasa kwa majina waliomfanya akaingiza kodi hiyo katika
kitabu cha Hotuba yake aliyosoma bungeni kuhusu bajeti ya Serikali na wakina na
hasa kwa majina waliomfanya arejeshe kodi hiyo ya kadi za simu kwenye jedwali
la marekebisho ya muswada wa sheria ya fedha alilowasilisha bungeni.
Nasisiza kuwa kauli za ujumla za Serikali bila
kuwataja kwa majina wahusika ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko
ya wananchi kuhusu kodi hii na nyinginezo kwa kuhamisha mzigo huo kwa wabunge.
Ni muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu wabunge, Rais ama kiongozi
mwingine mwenye mamlaka ajitokeze kusitisha kutozwa kwa kodi hiyo na kuanzisha
mchakato wa muswada wa kufuta kodi hiyo kuwasilishwa katika mkutano wa Bunge
unaotarajiwa kuanza tarehe 27 Agosti 2013.
Majina ya wahusika yasipotajwa au mamlaka zinazohusika
zisipotoa kauli katika mkutano wa hadhara nitakaoshiriki jumapili tarehe 21
Julai 2013 katika Uwanja wa Sahara kata ya Mabibo kuanzia saa 8 Mchana mpaka
saa 11 Jioni nitatoa mrejesho kuhusu yaliyojiri katika mkutano uliopita wa
Bunge na kueleza hatua zaidi zinazopaswa kuchukuliwa kuwezesha majina ya
wabunge hao kutajwa hadharani na hatua za kuondoa kodi hiyo kuchukuliwa.
Uongozi bora na uraia mwema wenye uwajibikaji ni
chimbuko na chachu ya ukuaji endelevu wa uchumi wa nchi na ustawi wa maisha ya
wananchi. Twende kazi.
John Mnyika (Mb)
19 Julai 2013
0 comments:
Post a Comment