SHIRIKA la Transparency International linasema mtu mmoja katika kila
wawili duniani anaamini ufisadi umeongezeka ndani ya kipindi cha miaka
miwili hii, ingawa watu wengi wanaamini wanaweza kubadilisha hali ya
mambo.
Asilimia 27 ya walioulizwa, walisema wamewahi kutoa rushwa kwa ajili ya kupata huduma za kijamii ndani ya miezi 12 iliyopita, hali inayomaanisha kwamba hakuna maend
eleo yoyote inapolinganishwa na muda kama huu mwaka jana, pale ripoti ya mwisho ilipotolewa.
Hali inaonekana kuzidi kuwa mbaya katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, hasa nchini Tanzania na Uganda, ambako matokeo ya utafiti huo, yanaonesha kuwa huduma muhimu za kijamii zimeendelea kupatikana kwa rushwa.
"Kwenye eneo la Afrika ya Mashariki tuna takwimu ambazo zinaogofya sana, kama vile Uganda au Tanzania, ambako takribani asilimia 70 ya watu wanaamini kuwa ufisadi umeshamiri.
Ni jambo la kuogofya zaidi kuona kwamba huduma kama vile elimu ni miongoni mwa maeneo matano yaliyoathiriwa sana na ufisadi, na hilo linayaathiri moja kwa moja maisha ya watu, maana fikiria kwamba unalazimika kutoa rushwa kutibiwa hospitalini." Amesema Lucas Olo Fernandes, afisa wa Transparency International kwa kanda hiyo ya Afrika.
Taasisi za kupambana na rushwa haziaminiwi
Ufisadi wazidi kusambaa duniani badala ya kupungua.
Kwa mfano, watu katika mataifa 36 wanawaona polisi kuwa mafisadi wakubwa kabisa, kwani katika nchi hizo kiasi cha asilimia 53 ya watu walishawahi kuombwa rushwa na polisi.
Hali inafanana na hiyo kwenye taasisi za mahakama, ambapo asilimia 30 ya watu kutoka nchi 20 walishawahi kutoa rushwa mahakamani na hivyo wanaamini kuwa mfumo wa sheria umejaa ufisadi.
Hata hivyo, la kutia moyo ni kwamba, watu 9 katika kila 10 walioulizwa walisema wangelichukua hatua dhidi ya ufisadi na robo ya wale walioombwa rushwa walikataa kutoa.
Matokeo haya yanaelezea haja ya serikali, asasi za kiraia na sekta ya biashara kufanya mengi zaidi katika kuwashirikisha watu kwenye mapambano dhidi ya ufisadi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Transparency International, Huguette Labelle, serikali zinapaswa kukibeba kilio hiki cha raia dhidi ya ufisadi kwa umakini mkubwa na kuchukua hatua madhubuti kuleta uwazi na uwajibikaji.
Kimsingi, serikali zimeonekana kutokufanya ya kutosha kupambana na ufisadi ndani na nje yake.
0 comments:
Post a Comment