OFISI ya Rais Sekretarieti ya Ajira
katika Utumishi wa Umma imekamata jumla ya vyeti vya kughushi 677
ambavyo wahusika wanadai kuvipata kutoka Wakala wa Usajili, Vizazi na
Vifo (RITA), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na
Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Vyeti hivyo vimepelekwa katika taasisi
hizo ili kujiridhisha kabla ya kushitaki wahusika kutokana na ofisi hiyo
kutokuwa na mamlaka ya kushitaki wenye vyeti ambao hawakupata nafasi
hizo.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na
Msemaji wa Ofisi hiyo, Riziki Abrahamu ambaye aliongeza kuwa tangu
kuanza kazi kwa Sekretarieti ya Ajira, wameend
esha mchakato wa ajira kwa
waombaji 4,891 na kuwapangia vituo vya kazi.
Alisema kwa mujibu wa
sheria, mtu atakayethibitika kughushi nyaraka hizo atahukumiwa kifungo
cha miaka 20 jela au kulipa faini ya Sh milioni moja au adhabu zote
mbili kwa pamoja.
Pia alisema Sekretarieti inaandaa utaratibu wa
kutoruhusu kufanya usaili mwingine waombaji ambao hawatakwenda kuripoti
sehemu zao za kazi walizopangiwa bila sababu za msingi.
Alisema
kutoripoti katika vituo vya kazi ni kosa na kutaka waombaji wa fursa za
ajira kutochagua maeneo ya kazi, hususan waliopangiwa vituo na
Sekretarieti.
Abrahamu alisema Sekretarieti kwa
kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
ilipeleka muswada bungeni unaopendekeza kukasimu madaraka ya kuendesha
mchakato wa ajira, ili baadhi ya waajiri wakasimiwe madaraka hayo kwa
nia ya kurahisisha utendaji kazi katika kushughulikia mchakato wa ajira
kwa baadhi ya kada.
“Sekretarieti itaendelea kuhakikisha
kuwa jukumu hilo linaendelea kutekelezwa kwa ufanisi kwa kutumia kitengo
cha udhibiti na ubora kinachosimamia uhakiki wa taarifa za mhusika
ikiwa ni pamoja na vyeti,” alisema Abrahamu.
Aliongeza kuwa nafasi za kazi
zitakazotangazwa na mchakato kukasimiwa ni pamoja na kada za wasaidizi
wa ofisi, wahudumu wa afya, madereva, maofisa watendaji wa kata, mtaa,
kijiji, wapishi, walinzi na madobi.
Alisema wengine ni wasaidizi wa kutunza
kumbukumbu na makatibu muhtasi walio chini ya cheo cha mwendesha ofisi
au kada zingine ambazo katibu wa Sekretarieti ataona inafaa kukasimu.
Aidha, alitumia fursa hiyo kushauri
wanafunzi shuleni na wanaotarajia kuingia vyuoni kuchukua masomo au kozi
za fani ya afya, elimu, mifugo na kilimo, akisema maeneo hayo bado yana
fursa nyingi za ajira serikalini na wahitimu hupangiwa vituo vya kazi
moja kwa moja bila mchakato wa ajira kwenye Sekretarieri.
Aligusia pia mtindo ulioibuka wa
watumishi wa sekta binafsi kuiba na kisha kuomba kazi Utumishi wa Umma,
akisema wameandaa utaratibu wa kuweka matangazo ya wizi kama kumbukumbu
ili wahakikishe wanaajiri watumishi wa Serikali wenye weledi na maadili
mema.
“Tunachofanya ni kukusanya kumbukumbu
kwa waliotuhumiwa na kuwafuatilia wakileta maombi ya kazi kama
walisingiziwa au kushitakiwa na tatizo kumalizika, kwa lengo la
kutoingiza katika ajira watu wenye tuhuma,” alisisitiza.
Kuhusu wananchi kupata taarifa kwa
haraka juu ya ajira katika utumishi wa umma, alisema ili kuendana na
mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano nchini na
duniani, Sekretarieti ilianzisha tovuti yake ( HYPERLINK
“http://www.ajira.go.tz” www.ajira.go.tz) ambayo tangu kuzinduliwa
Aprili imetembelewa na wadau zaidi ya milioni 3.1.
Abrahamu alisema pia wameanzisha
kanzidata za aina tatu ambazo ni za wahitimu wa vyuo, waliofaulu usaili
na waliopangiwa vituo, ili kuwezesha mara nafasi ikitokea ya waliofaulu,
bila kupangiwa vituo wapangiwe bila mchakato mpya.
“Jambo lingine ni kuwa Sekretarieti iko
katika hatua za awali za mchakato wa kuwezesha waombaji wa fursa za
ajira, kuwasilisha maombi ya kazi kwa mfumo wa kielektroniki kwa nafasi
zitakazotangazwa,” alisema.
Abrahamu alisisitiza kuwa hiyo itasaidia
kupunguza mlolongo wa uendeshaji mchakato wa ajira ulivyo sasa,
kupunguza gharama za kutuma maombi, kurahisisha uhakiki wa vyeti na
utoaji taarifa. CHANZO HABARILEO.
0 comments:
Post a Comment