KIONGOZI wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda ambaye alikuwa amelazwa katika Taasisi ya
Tiba na Mifupa (Moi), jana aliondolewa na kupelekwa katika Gereza la Segerea,
Dar es Salaam.
Kitendo hicho kimelaaniwa vikali na familia
yake na wafuasi wake, ambao wamep
anga kufanya maandamano makubwa leo.Daktari matatani
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro,
Faustine Shilogile amesema watamhoji daktari aliyemtibu Sheikh Ponda Mjini
Morogoro.
Hata hivyo, Kamanda Shilogile hakutaka kutaja jina la daktari huyo
akisema atakuwa anaingilia kazi ya Kamati ya Haki Jinai ambayo ndiyo
inayochunguza suala hilo.
Jeraha la Sheikh Ponda limezua utata baada ya
mwenyewe kusema kuwa limetokana na risasi aliyopigwa na askari wa jeshi hilo
huku polisi wakikana.Daktari huyo anaaminika kuwa ni miongoni mwa mashahidi
muhimu kwani anafahamu chanzo cha kidonda cha Sheikh Ponda.
Inaaminika kuwa alitibiwa katika zahanati ya
Al Jamih iliyoko Msamvu baada ya tukio hilo, Ijumaa iliyopita.
Hata
hivyo, Makamu wa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Rodrick Kabangira
alipinga kitendo cha daktari kuhojiwa akisema Baraza la Madaktari Tanzania
ndilo lilipaswa kumhoji.
“Tayari
kuna utata wa jeraha lenyewe na ukweli ni kwamba ripoti ya huyo daktari ni
muhimu kwa umma kwani ndiyo itathibitisha chanzo cha jeraha,” alisema.
Alisema
hakuna kosa lolote kwa daktari huyo kumhudumia Sheikh Ponda isipokuwa kama
atakuwa ameandika taarifa tofauti za jeraha hilo.
“Tatizo
kubwa ni kwamba Serikali imekuwa ikiruhusu uchunguzi kwa tume ambazo hazitoi
majibu halisi kwa wananchi. Ingetumika tume ya kimahakama au baraza ambalo lina
mamlaka hata ya kumfutia usajili wake kama atakuwa amedanganya,” alisema.
Msajili
wa Baraza la Madaktari Tanzania, Parot Luwena alisema madaktari hutakiwa
kufanya kazi kwa misingi ya taaluma zao wala siyo kwa shinikizo, hivyo kama
kuna masuala mengine ambayo polisi wanahitaji, wanapaswa kuzingatia sheria za
nchi.
Sheikh
Ponda, ambaye alisomewa shtaka la uchochezi akiwa kitandani na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Tumaini Kweka ilidaiwa kuwa alitenda kosa hilo
katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya Juni 2
mpaka Agosti 11, mwaka huu. Alisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi
wa Mahakama ya Kisutu, Hellen Liwa.
Jana, Polisi waliimarisha doria kwenye
Hospitali ya Taifa Muhimbili kuanzia saa 1:30 asubuhi. Magari matatu ya Kikosi
cha Kutuliza Ghasia(FFU) yaliyobeba askari wenye silaha yalionekana yakiranda
katika maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo.
Sheikh Ponda alitolewa wodini saa 4:20 asubuhi
chini ya ulinzi mkali wa askari baadhi yao wakiwa wamebeba silaha.
Alionekana akiwa ameshikiliwa na polisi
kutokana na kukosa nguvu ya kutembea.
Akiwa amevalia shati lenye rangi ya udongo,
kikoi cheupe na kandambili, Sheikh Ponda alipakiwa kwenye gari ndogo aina ya
Landcruiser nyeupe lililokuwa na vioo vya giza.Baada ya kupakiwa, safari ya
kuelekea Segerea ilianza saa 4:45.
Gari lililombeba lilitanguliwa na gari la
FFU lililokuwa na askari wenye silaha likifuatiwa na magari mengine mawili ya
FFU yaliyokuwa na polisi wenye sare na magari mengine mawili ambayo yalikuwa na
askari kanzu.
Wakili ashangaa, familia yaja juu.
Akizungumza baada ya tukio hilo jana, Wakili
wa Sheikh Ponda, Juma Nassoro alisema hakuwa na taarifa za kuondolewa hospitali
kwa mteja wake na kueleza kushangazwa na kitendo hicho akisema mteja wake
alikuwa mgonjwa akiwa anahisi maumivu makali ya kidonda tangu juzi.
“Nimepigiwa
simu mchana huu na mmoja wa wanafamilia, nimeshangaa sana kwa sababu nakumbuka
jana (juzi Jumatano) Sheikh alishindwa kufanyiwa mahojiano na polisi kutokana
na kuhisi maumivu na kizunguzungu,” alisema Nassoro.
Msemaji wa familia, Isihaka Rashid alisema
hawakuwa na taarifa ya Sheikh Ponda kupata ruhusa ya kutoka hospitali na kwamba
wakati anaondolewa alikuwapo mkewe na kijana mmoja kwani muda huo wanafamilia
wengine walikuwa kwenye kikao.“Nilifika hospitali asubuhi, hatukupewa nakala
yoyote ambayo inaonyesha Sheikh Ponda karuhusiwa.
Lakini baada ya tukio
tulipokwenda kuhoji tukaambiwa wamemruhusu tukapewa na karatasi ya kuthibitisha
kuwa ameruhusiwa,” alisema Isihaka.
Sheikh Ponda alifikishwa hospitalini hapo
Jumapili iliyopita, akiwa na jeraha ambalo linadaiwa kuwa ni la risasi
aliyopigwa na polisi katika mkutano wa Kongamano Mjini Morogoro. Rashid alisema
familia imepatwa hofu juu ya usalama wa maisha yake kwa kuwa hali yake bado
haijatengamaa kwani alikuwa amevimba mkono.
“Wamemchukua katika hali inayotia shaka kwa
sababu hata dawa zake hawakumchukulia, cheti cha ruhusa ya daktari pia
kimeachwa, gharama zake za matibabu yake ni Sh1.1 milioni.
Tumeambiwa tuchague
kama tunataka kulipia au vipi, kwetu tunaona kama wamemteka,” alisema Rashid.
Alisema kutokana na hali hiyo familia imeamua
kulirejesha suala la kufuatilia usalama wa maisha ya Ponda mikononi mwa
viongozi wa Jumuiya anayoiongoza ili walishughulikie na kwamba tayari
wamewajulisha kwamba watatoa tamko leo kwenye Msikiti wa Mtambani uliopo
Kinondoni.
Polisi waonya waandamanaji
Polisi imesema kwamba itadhibiti maandamano
yanayotarajiwa kufanyika leo kushinikiza kuachiwa kwa Sheikh Ponda.
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema jana
kuwa maandamano yoyote hayatavumiliwa na jeshi hilo.
“Tunapiga marufuku maandamano yoyote,
watakaoyafanya wafahamu kuwa jeshi litayadhibiti,” alisema.
Ubao wa matangazo ya Makao Makuu ya Polisi
limebandikwa tangazo la kuwataka polisi kuwa tayari kukabiliana na vurugu
zozote zitakazotokea.
Tangazo hilo limesema hali ya usalama siyo
nzuri na kwamba askari polisi wanatakiwa kujiandaa kukabiliana na vurugu. CHANZO :Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment