BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UHUSIANO TANZANIA NA RWANDA SASA WAZIDI KUINGIA DOA, NI BAADA YA RWANDA KUTANGAZA KUACHA KUTUMIA BANDARI YA DAR ES SALAAM,

UHUSIANO wa Tanzania na Rwanda, umezidi kuingia doa, baada ya nchi hiyo kutangaza kutotumia Bandari ya Dar es Salaam, kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu, kupitisha mizigo ya wafanyabiashara wake. 

Uamuzi wa Rwanda umekuja huku kukiwa na mgogoro wa chini chini unaoendelea kufukuta, baada ya Rais Jakaya Kikwete kumshauri Rais Paul Kagame, kukaa meza moja na waasi wa kundi la FDLR, ambao wanadaiwa kuendesha mapig
ano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Uamuzi huo, ulibainika mjini Dar es Salaam jana, wakati wa kikao cha pamoja kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, chini ya Mwenyekiti wake, Andrew Chenge na Umoja wa Wasafirishaji wa Mizigo kwa njia ya barabara Tanzania (TATOA).


Katika kikao hicho, TATOA ilieleza namna nchi za Rwanda na Uganda zilivyokusudia kuachana na mipango yao ya kupitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam.

Msemaji wa TATOA, Elias Lukumay, alisema kupanda kwa gharama za ushuru, kodi na nyinginezo, ni sababu kuu ya nchi hizo kujitoa kutumia bandari hiyo.

“Tunaelewa ufinyu wa bajeti ya Serikali, lakini sekta ya usafirishaji kwa sasa inaelemewa, baadhi ya vitu vilivyopanda na hivyo kuongeza gharama za uendeshaji ni leseni za barabarani, kodi ya mafuta, malipo ya bima, ghala la kuhifadhia mizigo, ada ya Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na nyinginezo.

“Gharama kubwa za uendeshaji katika usafirishaji na kuweka gharama nyingi za ziada kutaathiri uchumi ambapo wateja wa nchi jirani watatafuta njia mbadala, wakati ilitugharimu kuwaleta kwetu na wengine watatafuta shughuli mbadala na kuachana na usafirishaji,” alisema.

Alisema mkutano wa maazimio hayo ulifanyika Julai 19, mwaka huu, nchini Rwanda, ambapo mjadala ulikuwa ni kutotumia Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu Tanzania haina uamuzi wa haraka katika mambo yake kwa upande wa biashara.

“Kama TATOA, tulipata barua ya mwaliko wa mkutano huo, lakini hatukuhudhuria, sababu kubwa wenyewe wanasema hatueleweki na hatuna uamuzi wa haraka.

“Jambo hili pia, limechangiwa na mgogoro uliopo baina yetu na Rwanda, umechangia kwa kiasi kikubwa, kwani mkutano huo pia ulifanyika wakati Rais wa Marekani, Barrack Obama, akiwa nchini kwetu kwa ziara ya siku mbili,” alisema Lukumay.

Katika barua iliyoandikwa Julai 16, mwaka huu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Sekta Binafsi wa Rwanda, Hannington Namara na MTANZANIA kupata nakala yake, iliwataka wanachama wa usafirishaji katika nchi hizo kukutana ili kujadili utekelezaji wa ushuru wa pamoja wa orodha.

Sehemu ya barua hiyo ilisema: “Mkutano huo unarejea mazungumzo ya pande tatu yaliyofanyika mjini Kampala, Uganda, baina ya wakuu wa nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, ambapo madhumuni yake ni kujadili kwa kina masuala yanayohusu biashara ya upakuaji na upakiaji mizigo kuendana na utekelezaji wa ushuru wa pamoja wa forodha.”

Moja ya uamuzi uliofikiwa katika mkutano huo ilikuwa kuimarisha eneo la ushuru wa pamoja wa forodha na utekelezaji wake, ambapo kodi zitakusanywa katika maeneo ya mipaka kama Mombasa, Mpondwe na Oluhura.

TATOA waliomba sekta ya usafirishaji ipunguziwe kodi, ihamasishwe na kuwezeshwa ili itoe mchango zaidi kwa pato la taifa kwa mamlaka husika kutenga maeneo ya maegesho na kusitisha ukamataji wa magari unaoendelea.

Tanzania yaipuuza Rwanda

Katika hatua nyingine, Tanzania imesema haiko tayari kuendelea na vita ya maneno na Serikali ya Rwanda, licha ya vyombo vya habari vya nchi hiyo kuichafua familia ya Rais Jakaya Kikwete.

Kauli hiyo imetolewa ikiwa ni siku chache tu baada ya kuwapo taarifa za vyombo vya habari vya Rwanda kuichafua familia ya Rais Kikwete, kwa kuihusisha na undugu uliopo kati ya mke wake, Salma Kikwete na Rais wa zamani wa nchi hiyo, Juvenal Habyarimana.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ali, alisema Tanzania haihitaji kupoteza pumzi kuzungumzia masuala yasiyo na mantiki.

“Hatuhitaji kusemewa na tunadhani tutapoteza muda na pumzi kuendelea na vita ya maneno… Hivi watu wako kwenye duru ya mitandao, hatuna mantiki hata kidogo.

“Unaweza kujibu… lakini inategemea watu wenyewe wanaongea kitu gani, lakini hicho walichoongea kila mtu anao uwezo wa kutafakari,” alisema Ali.

Mtandao wa Rwandanews ambao ni maarufu nchini Rwanda, umeandika kuwa wabaya wa Kagame wanaotajwa kuwa na undugu wa damu na Salma Kikwete ni Wahutu, ambao ni wapinzani wa serikali ya sasa ya Rwanda.

Mtandao huo umeandika kuwa hiyo ndiyo iliyomfanya Rais Kikwete kugeuka kuwa kiongozi pekee duniani anayewaonea huruma waasi wa kundi la FDLR wa Mashariki mwa Kongo tangu mwaka 1994.

Kwa mujibu wa mtandao huo, taarifa za Salma Kikwete kuhusishwa na Habyarimana, zilibainika baada ya kurushwa kwenye mtandao huo Mei 5, 2005 na mtu aliyetajwa kwa jina la Shabyna Stillman, ambaye ni Mwanadiplomasia Mwandamizi katika Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: