BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KABURI LA MTOTO ALIYEKUFA MIAKA MITATU ILIYOPITA LAFUKULIWA CHINI YA ULINZI MKALI CHINI MKOANI GEITA.

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg_3HweD9SxX7162OTpT98rNEGi-YTyTjInFyPKBTy6rVxUk9gTh_lFBXZvGh_7BjG691tTPu-QS2Idsx6KPrmhn7V0VlNtNTOmhRB2IIObnLXEwvSzHPn9IQ3us9l7C4Yg5VQZTOzIJYbY/s1600/1.JPGKATIKA hali isiyokuwa ya kawaida kaburi ambalo alizikwa mtoto Shabani Maulidi (15), ambaye anadaiwa kufariki dunia miaka mitatu iliyopita na kuonek
ana akiwa hai hivi karibuni, jana lilifukuliwa na viungo vya mwili wake kukutwa ndani.

Kazi hiyo iliyofanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi pamoja na Mtafiti wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza, Lucas Ndungulu, ilizua taharuki kwa umati wa watu waliokuwa eneo hilo, baada ya nyumba ya jirani lilipo kaburi hilo, Masanja Marwa, kubomoka ghafla wakati ufukuaji huo ukiendelea, huku mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara moja naye akianguka na kuzirai.
 Mama mzazi wa mtoto Shabani menye kilemba kichwani akiwa amepigwa bumbuazi  maeneo ya hospitali siku alipomuona mwanaye. 
 
Kwa sasa mtoto huyo ambaye alionekana hai, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uangalizi wa kitaalamu.
Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Ndungulu alisema kuwa wameamua kufukua kaburi hilo ili kupata sehemu ya viungo vya mwili kwa ajili ya vipimo.PICHA YA MAKTABA.

“Lengo la kufukua kaburi hili ni kutaka tupate kiungo chochote cha mwili wa marehemu ili tufanye utafiti wa kitaalamu ili tujue kama ni kweli huyu anayedaiwa kuwa ni mtoto wao ndiye,” alisema.

Alisema kuwa ufukuaji huo umemalizika na kwamba wamepata baadhi ya viungo vya mwili wa marehemu na kuchukua baadhi ya mifupa ya mapaja yote mawili ambayo itapelekwa katika hospitali ya rufaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Kwa mujibu wa Ndugulu, majibu ya vipimo hivyo yatatolewa baada ya wiki mbili kama hakutakuwa na tatizo lolote la kukatika kwa umeme.

Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Adamu Sijaona, alisema kuwa pamoja na kuchukua viungo hivyo, pia watachukua damu ya wazazi na mtoto mwenyewe.

“Tumechukua pia damu ya mama na baba wa Maulidi mwenyewe ili tukapime vinasaba (DNA) na kama alivyosema mtafiti, majibu yatatoka baada ya wiki mbili,” alisema.

Akizungumza baada ya kazi ya ufukuaji kumalizika, baba mzazi wa mtoto huyo, Maulidi Shabani, alisema kuwa endapo majibu yatakuja tofauti au vile wanavyokusudia, wapo tayari kuyapokea na kwamba ikigundulika huyo aliyeonekana ni Maulidi, pia watampokea na kuendelea kumtunza.

“Lakini nina imani kuwa huyu aliyeonekana ni mwanangu Maulidi kabisa, kwa sababu anazo alama zote,” alisema mzazi huyo.
Mtoto Maulidi aliyefariki dunia miaka mitatu iliyopita na kufanyiwa matanga, alionekana akiwa hai baada ya kukutana na mama yake ana kwa ana mapema wiki hii asubuhi wakati akienda kwenye shughuli zake za biashara.

Ilidaiwa na wazazi wake kuwa Maulidi alitoweka ghafla na kushindwa kurudi nyumbani kwao Januari mosi 2011, wakati alipokuwa amewapeleka mbuzi malishoni na mwili wake kuonekana baada ya siku tatu akiwa amefia kwenye kisima cha maji.

Kwa mujibu wa baba yake, Maulidi hakurudi nyumbani siku hiyo, ambapo waliendelea kumtafuta bila mafanikio na ndipo baada ya siku tatu walimkuta akiwa amefia ndani ya kisima cha maji kilicho maeneo ya Kijiji cha Nyankumbu, Kitongoji cha Mwembeni.

Tukio hili ni la tatu kutokea mkoani hapa ambapo wilayani Kasamwa, mwanamke aliyefariki dunia miaka mitano iliyopita alionekana hai na kutambuliwa na ndugu yake. Tukio la pili lilitokea Wilaya ya Chato, wakati kijana aliyefariki dunia miaka miwili iliyopita alionekana akiwa hai. TANZANIA DAIMA.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: