Mkazi wa Kichangani, Yuster Manasa (40)
akipalilia mahindi huku akiwa na mtoto mgongoni katika shamba lake lililopo kata ya Kinglwira Manispaa ya Morogoro. PICHA MAKTABA MTANDA BLOG
RAIS Jakaya Kikwete amesema ni aibu kwa
Serikali kudaiwa na wakulima na amewahakikishia wakulima wa Wilaya ya
Ludewa Mkoa wa Njombe, kuwa watalip
wa haraka iwezekanavyo fedha zao
wanazodai kwa kuiuzia Serikali mahindi yao.
Aidha, Rais Kikwete amethibitisha kuwa
meli ambazo Serikali yake iliahidi kununua kwa ajili ya usafiri katika
Maziwa Makuu ya Tanzania, zinajengwa na zitazinduliwa kabla ya mwaka
2015.
Amesema zinaweza kuwa meli mbili, badala
ya moja, kwa kila moja ya maziwa ya Nyasa, Tanganyika na Victoria. Rais
alisema hayo juzi, alipozungumza kwa nyakati tofauti katika Wilaya ya
Ludewa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi kukagua na kuzindua
miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Njombe.
Rais Kikwete aliwaambia wakazi hao wa
Ludewa kwenye mkutano wa hadhara kuwa ni kweli Serikali yake inadaiwa
kiasi cha Sh bilioni 17 ikiwa ni deni la wakulima wa mikoa mbali mbali
nchini, ambao waliuza mahindi yao ya msimu uliopita kwa Wakala wa Taifa
wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Suala hilo lilijirudia tena wakati Rais
Kikwete alipokuwa anapokea Ripoti ya Maendeleo ya Wilaya ya Ludewa,
ambako aliambiwa kuwa wakulima wa wilaya hiyo pekee, walikuwa bado
wanaidai Serikali Sh bilioni 3.115 ambayo ni thamani ya mahindi ya tani
6,231, ambayo wakulima hao waliiuzia NFRA.
Aliambiwa kuwa mpaka sasa wakulima wa Wilaya ya Ludewa, wamelipwa Sh bilioni 2.839 kutokana na tani 5,679 za mahindi.
NFRA ilikuwa imelenga kununua kutoka kwa
wakulima wa Wilaya ya Ludewa tani 13,000, lakini mpaka sasa imeweza
kununua tani 11,911 tu, na sehemu kubwa ya kiasi hicho, haijalipiwa na
Serikali. “Hii ni aibu. Serikali haiwezi kudaiwa na wakulima. Hizi fedha
zitalipwa tu,” alisema Rais Kikwete.
Alielezea hatua ambazo amezichukua
binafsi katika siku mbili kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao. Pia,
alisema Serikali yake itaangalia uwezekano wa kununua tani 2,972 za
mahindi ya msimu uliopita, zilizobakia mikononi mwa wakulima wa wilaya
hiyo.
“Naambiwa kuwa bado NFRA inahitaji kiasi
cha tani 40,000 hivi ili kukamilisha shehena ya idadi ya kiasi cha tani
250,000 za mahindi kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa mwaka huu. Nitawaambia
waangalie kama wanaweza kununua kiasi hiki kilichobakia mikononi mwa
wakulima wa Ludewa”, alisema.
Kuhusu maombi ya wananchi wa Ludewa
kununua meli ya kuchukua nafasi ya Mv. Mbeya iliyozama katika Ziwa Nyasa
ili kurahisisha usafiri ndani ya ziwa hilo, ambalo linapakana na Wilaya
ya Ludewa, Rais alisema Serikali yake inanunua meli hiyo.
“Tunajua kuwa meli ya Mv. Mbeya ilizama
katika Ziwa Malawi na kwa kweli meli zimezama katika maziwa mengine
makubwa ya Tanganyika na Victoria, na mimi kwenye Kampeni niliahidi kuwa
nitanunua meli moja kwa kila ziwa,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza: “Tumeagiza meli tatu kutoka
Korea Kusini, zinajengwa. Tumeagiza meli nyingine tatu kutoka Denmark.
Nazo zinajengwa. Hivyo, tunaweza kupata siyo meli moja bali meli mbili
katika maziwa yote matatu. Ni matumaini yangu kuwa nitaweza kuzizindua
meli hizo kabla ya kumaliza kipindi changu cha uongozi, mwaka 2015.” HABARILEO.
0 comments:
Post a Comment