Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Luteni (mstaafu) Chiku Gallawa kulia akimjulia
hali askari aliyejeruhiwa na mapanga wakati wa vurugu zilizotokea
wilayani Lushoto mkoani Tanga hivi karibuni kushoto.
VURUGU kubwa zimetokea katika kijiji cha Viti kata ya Shume Wilaya ya Lushoto
mkoani Tanga ambazo zimesababisha Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai
wilayani humo (OCCID), Ufoo Maanga, kucharangwa mapanga na wananchi naye
kujih
ami kwa kumuua mmoja na kumjeruhi mwingine kwa kuwapiga risasi.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Majid Mwanga, alithibitisha kutokea kwa tukio
hilo lililotokea usiku wa kuamkia juzi wakati askari ambao idadi yao
haijajulikana walipokwenda usiku wa manane kwa ajili ya kumkamata
mtuhumiwa mmoja kijijini hapo katika mgogoro wa ardhi.
Mwanga ambaye hakueleza kwa undani juu ya tukio hilo, alisema upelelezi
wa tukio hilo umeanza ili kubaini chanzo chake na kuwataka wananchi
kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mikononi.
“Polisi walikwenda pale kufanya kazi yao ya kumkamata mtuhumiwa katika
kesi ya mgogoro wa ardhi, walipofika kijijini hapo wakapokewa kwa
kushambuliwa kwa mapanga na wanakijiji,” alisema Mwanga.
Aliyeuawa kwa kupigwa risasi katika tukio hilo amefahamika kwa jina la
Khamis Seif na aliyejeruhiwa ni Athumani Abdallah Mngazija ambaye
amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Lushoto akiendelea na matibabu.
Aidha, OCCID aliyejeruhiwa kwa kucharangwa mapanga na wanakijiji
kichwani na kwenye vidole alihamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Bombo kutoka
Hospitali ya Wilaya ya Lushoto alikokuwa amelazwa awali.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe,
alisema kufuatia tukio hilo mtu mmoja amekamatwa na kwamba uchunguzi
zaidi wa tukio hilo unaendelea.
Hata hivyo, Kamanda Massawe, hakumtaja kwa jina mtuhumiwa aliyetiwa mbaroni.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Viti, Samuel Shelukindo, akizungumza na NIPASHE
kwa simu, alisema juzi askari kadhaa walifika kijiji hapo mapema
asubuhi na baadaye walikwenda kijiji cha Mtae.
Alisema ilipofika usiku saa 5:00 askari hao wakiongozwa na OCCID
walifika kijijini hapo bila kutoa taarifa kwa viongozi wa kijiji,
kitongoji wala kata na kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa katika kesi ya
mgogoro wa ardhi aliyetajwa kwa jina la Mohamed Khamis na kumgongea
mlango ili afungue.
Mohamed Khamisi ameshitakiwa na Athuman Rajabu maarufu kwa jina la Komba
katika Baraza la Ardhi Wilaya ya Korogwe katika kesi namba 189/2013.
Komba alipotafutwa katika simu yake hakupatikana.
Mwenyekti huyo alisema Khamis (mtuhumiwa) alikataa kufungua mlango wa
nyumba yake na ndipo askari hao waliamua kuuvunja na kuingia ndani na
watu waliokuwa wamelala ndani ya nyumba hiyo walipiga kelele kuomba
msaada kutoka kwa majirani.
Shelukindo alisema baadaye majirani walitoka na kwenda katika nyumba
hiyo na ndipo zikazuka vurugu ambazo zilisababisha OCCID kufyatua risasi
kutoka katika bastola yake kujihami na kuua mtu mmoja na kujeruhi
mwingine.
Alisema waliopigwa risasi ni Khamis Seif na Athuman Mngazija ambao usiku
huo Mtendaji wa Kata ya Shume, Jamar Karanga, akisaidiana na wanakijiji
waliwapeleka majeruhi hao katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto.
Hata hivyo, usiku huo mmoja wa majeruhi hao ambaye ni Khamis Seif
alifariki dunia akiwa hospitali kutokana na kuvuja damu nyingi.
Shelukindo alisema wanakijiji hao baada ya kuona wenzao wamepigwa risasi
walipandwa na hasira na kuanza kumjeruhi OCCID kwa kumpiga ambaye
aliokolewa na askari wenzake waliomchukua na kumwingiza katika gari yao
na kuondoka kijiji hapo.
Aliongeza kuwa majeruhi katika tukio hilo ambaye bado anaendelea na
matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto yupo chini ya ulinzi wa
polisi na amefunga pingu ingawa hali yake bado ni mbaya.
Shelukindo alisema kitendo cha polisi kuvamia kijiji bila kutoa taarifa
kwa viongozi wa kijiji husika siyo kizuri kwani wananchi wanategemea
walindwe na polisi lakini kama wao ndio wanageuka kuwa wauaji siyo
kitendo kizuri
“Mimi kama kiongozi wa kijiji nalaani kitendo cha polisi, watu
wanategemea polisi kulinda raia na mali zao, lakini wao ndio wanaua,”
alisema Shelukindo.
Mwenyekiti huyo alisema katika hali ya kushangaza Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya ya Lushoto haijafika kijijini hapo tofauti na matukio
mengine.
Shelukindo alisema katika vurugu hizo mtu mmoja ambaye inadaiwa ndiye
alikwenda polisi kulalamika amechomewa nyumba zake nne na wananchi wenye
hasira.
Taarifa ambazo zimeifikia NIPASHE jana jioni zilieleza kuwa OCCID
aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa Bombo ameruhisiwa baada ya
hali yake kuimarika. CHANZO:
NIPASHE
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment