TUNDU LISSU ATOA TAHADHARI KWA RAIS JAKAYA KIKWETE HUKUSU MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA.
MBIVU na mbichi kuhusu muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya Katiba zitajulikana leo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, itakapok
utana katika ofisi ndogo za Bunge Dar es Salaam.
Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya kamati hiyo zinaeleza kuwa pamoja na mambo mengine, muswada huo ni miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa.
Hata hivyo, Katibu wa Kamati hiyo, Yona Kirumbi, aliiambia NIPASHE jana kwamba Kamati itakutana kwa mambo yake ya ndani.
Wakati kamati hiyo ikitarajiwa kukutana leo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema itakubali kukaa kwenye meza ya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete iwapo atakuwa hajausaini muswada huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mnadhimu Mkuu wa Kambi hiyo, Tundu Lissu, alisema mtazamo wa Rais Kikwete, wa kusema kuwa madai ya wapinzani yanazungumzika, utakuwa na maana kama hatosaini muswada husika.
“Kama Rais atataka tumwamini asiusaini huo muswada, akiusaini atakuwa amesema tunaotaka muswada huu ujadiliwe upya hatuna maana, akisaini atakuwa ameendeleza mambo ya ki-CCM. Asisaini tutazungumza,” alisema Lissu.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), aliongeza kuwa: “Na kesho (leo), Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala inakutana, hapo ndipo tutajua haya aliyosema Rais yanazungumzika ama la.”
Alitahadharisha kuwa ni hatari kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhodhi mchakato wa Katiba na kwamba Watanzania hawatanyamaza ikiwa utavurugwa akisema nchi inaweza kuingia kwenye machafuko makubwa.
Aidha, alisema maandamano yaliyoandaliwa na vyama vya upinzani Oktoba 10, mwaka huu yapo pale pale na kusisitiza kuwa mgomo mkubwa pia utafanyika ndani ya Bunge.
Hata hivyo, wakati kukiwa na taarifa za Kamati hiyo kukutana leo, Mwenyekiti wake, Pindi Chana, aliiambia NIPASHE kwa njia ya simu jana kuwa yupo Ludewa mkoani Njombe na kwamba atarejea Dar es Salaam baada ya wiki moja.
“Nani kakuambia kamati inakutana? Mimi nipo Ludewa, nitarudi baada ya wiki moja,” alisema Chana.
LISSU AMJIBU JK.
Wakati huo huo; Lissu amemjibu Rais Kikwete akieleza kwamba taarifa za yeye (rais), kukiuka mapendekezo ya wadau wakati wa uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Katiba zilitolewa kwenye Kamati ya Katiba wakati wa vikao vya kamati za Bunge.
Alisema wawakilishi kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tec), Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste (CCT) na Shirikisho la Walemavu (Shivyawata), waliieleza kamati kwamba mamlaka ya Rais katika kuteua wajumbe yanamapungufu wakisema majina waliyopendekeza hayakuteuliwa bali aliteua mtu aliyemtaka.
“Kwa mfano Shivyawata wanasema hawakumpendekeza Al Shayma Kweigir kuwawakilisha kwenye tume, lakini ndiye aliyeteuliwa, kwa hiyo siwezi kuamini kwamba hawa waliokuja kwenye kamati walidanganya, hizi ni taarifa zilizotolewa kwenye kamati,” alisema.
Alisema inawezekana waliomweleza rais kuhusu alichokuwa amekisema bungeni wamempotosha kwa makusudi ilhali wakiujua ukweli wote.
Kuhusu ushiriki wa Zanzibar, alisema kamati ilipanga kufanya ziara ya siku tatu visiwani humo kwa nia ya kutembea, lakini akaibua hoja ya kwenda kukusanya maoni ya wadau kuhusu muswada huo na katika hali ya kushangaza, ziara hiyo ilisitishwa.
Alisema matokeo yake ni kwamba kamati ilikutana na takribani makundi 30 ya wadau kutoka Bara ambao walitoa maoni yao, lakini hakuna mdau kutoka Zanzibar aliyeshiriki.
Alisema Rais Kikwete amemshambulia bila kujua ukweli wa kina kuhusu kile kilichokuwa kimetokea bungeni.
Wapinzani wataka rais asisaini muswada huo kwa sababu una mapungufu makubwa ikiwamo Zanzibar kutoshirikishwa kwenye mchakato wa kukusanya maoni kabla haujawasilishwa bungeni na pia Rais apunguziwe mamlaka ya kuteua wajumbe 166 wa Bunge la Katiba.
Kifungu kingine kinacholalamikiwa ni kile cha ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kinachotaka tume hiyo ikishawasilisha Rasimu kazi yake iishie hapo.
Badala yake, wadau wanataka kazi ya tume iishe wakati wa kupiga kura ya maoni ili wakati wa mjadala kwenye Bunge la Katiba, iweze kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali.
Akihutubia Taifa mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Kikwete pamoja na mambo mengine, alisema madai ya upinzani yanazungumzika na kuwataka kusitisha maandamano na badala yake wayape mazungumzo nafasi.
Pia alisema Zanzibar ilishirikishwa kwa kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa maoni na kwamba madai ya kutozingatia majina yaliyopendekezwa na wadau wakati wa uteuzi siyo ya kweli kwa kuwa hakuwahi kufanya hivyo.
WADAU WAMPONGEZA JK
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, akizungumza na NIPASHE jana alimpongeza Rais Kikwete kwa kutoa wito wa kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ikiwa ni pamoja na wale wa Kamati ya Ufundi ya Ushirikiano inayojumuisha vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi kwa madai kwamba una nia nzuri.
Dk. Bana alisema Rais Kikwete ameonyesha nia njema na hivyo kuvitaka vyama vyote kutokumshinikiza kwa kumpa rais muda kwa kuwa halazimishwi na kwamba hayo siyo mawazo ya Watanzania wote.
“Vyama vyote na siyo vitatu tu, vikubaliane na kauli ya Kikwete na siyo kutoa mashinikizo ili mchakato wa katiba uweze kwenda kwa maelewano na kujenga nchi bora,” alisema Dk. Bana na kuongeza.
“Kauli ya Rais ni njema kwa kuwa inaelekea katika kupatikana muafaka, hivyo kamati hiyo ya ufundi pamoja na vyama vingine vya siasa nchini visionekane kuhodhi mchakato wa kupatikana katiba mpya kwa kuonekana kuwa wao ndiyo wanawasemea Watanzania.”
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Helen Kijo Bi-Simba, alisema mahali ulipofikia mchakato wa katiba siyo pazuri hivyo vyama vya siasa viwe tayari kukaa pamoja na Rais, ili waweze kumsikiliza.
Alisema vyama vya upinzani visipokubali kukaa chini kuzungumzia suala hilo, haiwezekani kufikia hatima nzuri wanayoitaka.
“Kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu, Joseph Warioba, vyama vya siasa naomba vitambue kwamba, mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya siyo wa kwao pekee bali ni wa Watanzania wote hivyo wakubali kukaa chini, wamsikilize, waangalie na kukipima kile atakachozungumza kwani mahali tulipofikia sasa siyo pazuri,” alisema.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaad Mussa, alisema uamuzi wa Rais Kikwete wa kufungua milango ya kukutana na wapinzani kujadili kasoro za mchakato wa katiba, ni jambo, ambalo linaonyesha kuwa ni ukomavu wa kisiasa.
Alisema mbali na ukomavu wa kisiasa, pia linaonyesha Rais Kikwete ni kiongozi asiyekuwa mwoga, anayejiamini na kujali maslahi ya watu wake.
Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), David Mwasota, alisema uamuzi huo wa Rais Kikwete ni wa kizalendo, kwani utasaidia kuondoa dukuduku la wapinzani na kuiacha nchi katika hali njema.
Hata hivyo, alimshauri kufanya kweli kwa kuonyesha dhamira hiyo kwa vitendo. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment