SIMBA YANUSURIKA KUSHUKA DARAJA TENA 1988
John Bosco, Kipa wa Simba.
Na Daniel
Mbega.
SIMBA,
siyo tu kwamba iliokoka na kuteremka daraja msimu huo ukiwa ni msimu wa pili
mfululizo kunusurika, bali ushindi wao wa magoli 2-1 dhidi ya mahasimu wao
wakubwa, Yanga Jumamosi Julai 23, 1988 mwaka huo kwenye Uwanja wa Taifa
uliifanya ilinde hadhi yake.
Mchezo huo ulikuwa ni wa marudiano wa Ligi Daraja
la Kwanza Tanzania Bara, ambapo katika mchezo wa kwanza timu hizo zilifungana
1-1.
Kwa
Coastal Union kuchapwa magoli 2-0 na African Sports siku hiyo, Yanga ilihitaji
sare tu ili iweze kutetea ubingwa wake, lakini timu ya Tanga pamoja na kipigo
hicho ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa tofauti ya idadi ya
magoli ya kufunga. Yanga na Coastal zilikuwa na pointi 26 kila moja, lakini
Coastal ilikuwa na magoli 27 na Yanga ilikuwa na magoli 24.
African
Sports ilishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 26 pia lakini ilikuwa na magoli
23 ya kufunga. Timu hii, hata hivyo, iliingia kwenye Ligi Kuu ya Muungano na
kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Tanzania nzima mwaka huo. Simba ilikuwa ya tatu
kutoka mwisho ikiwa na pointi 20.
Baada ya
John Makelele kufunga goli la ushindi mapema katika kipindi cha pili, Yanga
ilishindwa kuuvunja ukuta wa Simba. Mashabiki wa Simba walikuwa na furaha kubwa
jioni hiyo, kwani kwa msimu wote hawakuwa na imani kama timu yao ingeweza
kunusurika isishuke daraja.
Siku hiyo
vijana hao wa Msimbazi walionyesha mpira mzuri na ari ya ushindi ilikuwepo
tangu mwanzo. Yanga ilichanganyikiwa sana siku hiyo baada ya kutamba kwamba
wangeifunga Simba kwa kuwa timu hiyo msimu huo ilikuwa dhoofulhali, lakini
wakajikuta wakiwa katika wakati mgumu sana.
Hadi
mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana 1-1, kama walivyofanya katika mchezo
wa kwanza Aprili 30, mwaka huo. Kama ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza, Edward
Chumila tena ndiye aliyeanza kufunga goli la Simba katika dakika ya 21. Malota
Soma alimhadaa mlinzi wa Yanga kwenye wingi ya kulia na krosi yake ilisogezwa
kidogo tu na walinzi wa Yanga na hivyo kumwezesha Chumila kufunga kirahisi
baada ya kufumua shuti kali mara mpira ulipodunda.
Dakika
tisa baadaye mwamuzi Msafiri Mkeremi aliinyima Simba penati ya wazi baada ya
Godwin Aswile wa Yanga kuunawa mpira huo ndani ya eneo la hatari. Badala yake
Mkeremi akaamuru ipigwe ‘free - kick’ kuelekea goli la Simba, huku mashabiki wa
Simba wakiwa hawaamini.
Mpaka
wakati huo Yanga haikuonyesha kama ilikuwa inajiamini na mara nyingi ilikuwa
ikitumia mbinu za kuotea kuwavunja nguvu washambuliaji wa Simba. Katika dakika
ya 36 Yanga ilifanikiwa kusawazisha goli hilo kupitia kwa nahodha Issa Athumani
aliyemzidi ujanja Mkandawire kabla ya kuunganisha wavuni kwa kichwa krosi ya
Athumani China. Mkandawire akabaki chini amelala asiamini yanayotokea langoni
mwake.
Bao hilo
liliwapa imani Yanga na mchezo ungeweza kuwa hivyo kama siyo makosa ya kipa
Sahau Kambi wa Yanga yaliyowapa ushindi Simba katika dakika ya 58. Kambi
aliuona mpira wa kichwa wa Malota Soma hauna madhara sana, akaudharau, lakini
ghafla akatokea Makelele aliyeukwamisha wavuni kabla haujamfikia kipa huyo.
Pamoja na
jitihada zote, ngome ya Simba ikawa makini zaidi kulinda bao lake. Mwamuzi
Msafiri Mkeremi kutoka Tabora hakuweza kutoa hata kadi moja katika mechi hiyo.
Mgeni
rasmi katika pambano hilo alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Salim Ahmed Salim. Viongozi wengine waliohudhuria
ni pamoja na Spika wa Bunge, Chifu Adam Sapi Mkwawa, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Utamaduni na Michezo, Zahra Nuru na Mwenyekiti wa Baraza la
Michezo (BMT), Hamza Kasongo. Jumla ya watazamaji 30,000 walihudhuria pambano
hilo.
YANGA: Sahau Said Kambi, Fred Felix/Yusuf Bana,
Kenneth Mkapa, Godwin Aswile, Lawrence Mwalusako, Athumani China/Abdallah
Burhani, Justin Mtekele, Said Mwamba ‘Kizota’, Issa Athumani, Dennis Mdoe na
Celestine Mbunga.
SIMBA: John Bosco, Raphael Paul, Twaha Hamidu, Deo
Njohole ‘OCD’, Pazi Ally, Daniel Muhoja, John Makelele, Adolf Kondo/Francis
Mwikalo, Edward Chumila na Augustine Haule.
0 comments:
Post a Comment