DAR ES SALAAM.
KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo inaanza kikao chake cha siku mbili ikitarajiwa kujadili masuala mazito, hasa misukosuko iliyokikumba katika siku za karibuni.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Habari
na Uenezi wa Chadema, John Mnyika ilisema kikao hicho kitakachofanyika
Dar es Salaam kitapokea, kujadili na kufanya uamuzi wa masuala
mbalimbali ikiwamo hali ya siasa na ripoti ya fedha.
“Suala mojawapo litakuwa kujadili mihutasari ya
mikutano iliyopita na yatokanayo na mikutano hiyo, taarifa ya hali ya
siasa na ripoti ya fedha,” ilisema taarifa hiyo ya Mnyika, ambaye yuko
ziara ya kikazi huko Uturuki.
Pia utajadili mchakato na maudhui ya mabadiliko ya
katiba, taarifa ya utekelezaji wa Programu ya Chadema ni Msingi na
shughuli za kanda na taarifa ya utekelezaji wa Mpango Mkakati kuhusu
maboresho.
Chadema katika mawimbi makali
Miongoni mwa mambo ambayo yanatarajiwa kujadiliwa
katika kikao hicho ni mustakabali wake katika kipindi hiki ambacho
kinapita katika mawimbi makali kutokana na kuibuka kwa malumbano ya
waziwazi baina ya viongozi wake waandamizi na pia kusimamishwa kwa
baadhi ya viongozi wa mikoani.
Matukio ya karibuni yanajumuisha malumbano kati ya
Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
kuhusiana na masuala ya posho, kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Chadema
wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kuvunjwa kwa uongozi wa Mkoa wa Mara
na pia kuondolewa kikaoni kwa Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda.
Wafuatiliaji wa mambo ya siasa watakuwa
wanakitazama kikao hiki kama fursa ya kuweka sawa mambo ili kiendelee
kutoa ushindani kwa chama tawala.
Alipoulizwa kama matukio ya hivi karibuni
yatajadiliwa katika kikao hicho, Mnyika alikataa kuingia kwa undani na
badala yake alisema taarifa zitatolewa baada ya kikao.
“Niko nje ya nchi, mengine utapewa majibu kesho
(leo) kwa yale ambayo yatakuwepo katika taarifa zitakazowasilishwa. Yale
ambayo hayatakuwepo utajulishwa pia iwapo hayatajadiliwa,” alisema
Mnyika.
Zitto na Lema
Zitto na Lema waliingia katika vita ya maneno mwanzoni mwa Novemba kuhusiana na masuala ya posho ya vikao.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment