MATUKIO YA KISIASA.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto.
UMOJA wa Afrika unalitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo kupiga kura kuahirisha kwa mwaka mmoja kesi ya uhalifu wa kibinaadamu dhidi ya viongozi wa Kenya katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC.
Ili liweze kupitishwa, azimio hilo linahitaji kupigiwa kura na wanachama tisa, lakini hata hivyo, linaweza kupingwa kwa kupigiwa kura ya turufu na mataifa kama vile Uingereza na Ufaransa, yanayoiunga mkono kwa kiasi kikubwa Mahakama ya ICC, iliyoko The Hague.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda
Marekani bado haijajiunga na mahakama hiyo kupitia mkataba wa Roma, lakini inaunga mkono malengo yake.Umoja wa Afrika unasema kwamba kuahirishwa kwa kesi hiyo, kutaipa Kenya muda wa kuimarisha usalama wake katika kukabiliana na vitendo vya kigaidi, baada ya mashambulizi ya kigaidi ya mwezi Septemba mwaka huu.
Shinikizo lilitokana na shambulizi la kigaidi
Shinikizo la kuahirishwa kwa kesi hiyo limeongezeka baada ya kutokea mashambulizi hayo ya kigaidi yaliyosababisha mauaji ya watu 67 na wengine kadhaa kujeruhiwa. Hata hivyo, wanadiplomasia wa mataifa ya Magharibi na wanaharakati wanaiona hatua hiyo kama kampeni ya kisiasa.
Mahakama ya ICC imewafungulia Kenyatta na Ruto mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu kwa kuhusika kwao na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, ambazo zilisababisha zaidi ya watu 1,000 kuuawa.
Kenyatta anashtakiwa kwa ubakaji na vitendo vingine vya ukatili vilivyofanywa na kundi la kihalifu linalojulikana kama Mungiki, ambalo linadaiwa lilikuwa chini yake.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki MoonAma kwa upande mwingine, kura ya maoni iliyoendeshwa nchini Kenya, imeonyesha kuwa asilimia 67 ya Wakenya wanataka Rais Kenyatta ahudhurie kesi dhidi yake huko ICC, ili akajibu shutuma zinazomkabili.
Utafiti huo uliofanywa na shirika la Ipsos Synovate, unaonyesha kuwa asilimia hiyo ya raia 2,060 wa Kenya walioulizwa, waliona ni bora Rais Uhuru aende ICC kujibu kesi dhidi yake. DW

0 comments:
Post a Comment