ZAIDI ya wanafunzi 600 wa Shule ya Msingi Kikoo iliyopo Kata ya Kitomondo, wilayani Mkuranga, Pwani, wanasoma kwa kukaa chini ya miembe.
Hayo yalibainishwa na Diwani wa Viti Maalumu, Daima Utanga (CCM), katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika wilayani humo katika ukumbi wa Parapanda, kilichokuwa kinajadili shughuli za maendeleo ya wilaya.
Alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa madawati, hali inayosababisha wanafunzi hao kusoma chini ya miembe.
Alisema shule hiyo tangu kuanzishwa kwake hadi sasa ina wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tano, na ina madarasa mawili tu.
“Serikali naiomba iangalie tatizo hili kwa jicho la tatu ili iwajengee wanafunzi madarasa, iwapatie vifaa vyote muhimu kama kweli tunategemea kupata ‘Matokeo Makubwa Sasa’.
“Mpango wa serikali kutegemea ‘Matokeo Makubwa Sasa’ katika Shule ya Kikoo hayatakuwepo kama serikali haitafanya jitihada za kuondoa mazingira mabovu kwa wanafunzi wa shule hiyo,” alisema. Diwani huyu. TANZANIA DAIMA.
0 comments:
Post a Comment