KWA miaka mingi, watu wenye ulemavu wa kuona, wasioona kabisa na
wale wenye uono hafifu, wengi wao wamekuwa wakitumia fimbo maalumu
(white cane) kwa ajili ya kutambua vitu vilivyo mbele yao.
Hata hivyo, mwanasayansi Dk Stephen Hicks wa Chuo
Kikuu cha Oxford nchini Uingereza, amegundua teknolojia mpya ya miwani
inayowawezesha watu wenye ulemavu wa kuona kutambua vitu vilivyo mbele
yao, maandishi kwenye mabango na majina ya mitaa kupitia miwani maalumu
iliyopewa jina la ‘Smart Glasses.’
Kwa mujibu wa Dk Hicks, teknolojia hiyo mpya
inafuatia teknolojia nyingine ya miwani, ambayo humwezesha mtu mwenye
ulemavu wa kuona, kupata picha ya vivuli ya vitu vilivyo jirani naye,
ikiwemo binadamu.
NOOR SHIJA.
NOOR SHIJA.
Hata hivyo, Dk Hicks amekuja na uvumbuzi mwingine
wa ‘Smart Glasses’ inayomsaidia mtumiaji kujiongoza mwenyewe katika
maeneo ambayo hayafahamu kwa kusoma vibao vya maelekezo, kama vile
majina ya mitaa na vituo vya basi.
Dk Hicks anasema kuwa miwani hiyo inamfanya mtu
mwenye ulemavu wa kuona kuweza kujitegemea kwa kiwango kikubwa, ikiwemo
kufahamu maneno yaliyoandikwa kwenye mabango ya matangazo, mitaa na
orodha ya vyakula hotelini.
Kwa mujibu wa teknolojia hiyo ya Dk Hicks, miwani
hiyo imetengenezwa kwa kuwekwa kamera ambazo zinarekodi picha, yakiwemo
maandishi na kuyatambulisha kwa sauti kwa mtumiaji. Mfano, orodha ya
vyakula hoteli, miwani hiyo inarekodi maneno na kuyatamka kwa sauti kwa
mtumiaji.
Dk Hicks anasema kuwa miwani hiyo itasaidia maelfu
ya watu wenye ulemavu wa kuona kuweza kumudu kufanya shughuli zao bila
utegemezi wa watu wengine, ikiwemo kufahamu maelekezo yanayotokana na
mabango ya barabarani, hasa majina ya mitaa na vituo vya mabasi.
Zaidi ya miaka mitatu, Dk Hicks amekuwa
akitengeneza miwani hiyo aliyoweka kamera na programu inayomsaidia
mtumiaji kubaini kitu na miwani hiyo inamtamkia kwa maneno.
Ulemavu wa macho ni hali ya kukosa kuona kutokana
sababu zinazohusiana na mishipa, kuna viwango mbalimbali vimetengenezwa
ili kuelezea kiwango cha kukosa kuona, ambapo upofu kamili ni ukosefu
kamili wa kuona maumbo na mwanga na hurekodi kliniki kama NLP, kifupishi
cha “No Light Perception” au kukosa kuona mwanga.
Hata hivyo, kwa mujibu wa wataalamu wa macho, watu
wenye ulemavu huo ambao macho yao bado hayajaharibika, wanaweza
kutambua kukiwa na mwanga ingawa hawaoni kwa ukamilifu. Ishara za mwanga
za lengo hili husafiri kupitia njia ya ‘retinohaipothalamia,’ kwa hivyo
mishipa ya jicho iliyoharibika kupita mahali ambapo njia ya
‘retinohaipothalamia’ hutokea kwenye jicho siyo kizuizi.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO),
zinaeleza kuwa visababishi vya upofu wa kawaida duniani kote katika
mwaka 2002 vilikuwa mtoto wa jicho asilimia 47.9, glakoma asilimia 12.3,
kuzorota kwa seli kunakohusiana na umri asilimia 8.7, konea kutopitisha
nuru asilimia 5.1 na kuharibika kwa retina kunakosababishwa na ugonjwa
wa kisukari asilimia 4.8, pia upofu tangu utotoni asilimia 3.9, trakoma
asilimia 3.6 na onkoseresiasisi asilimia (0.8).
Kulingana na suala la maambukizi ya upofu duniani,
idadi kubwa ya watu katika nchi zinazoendelea na uwezekano mkuu wao
kuathiriwa unamaanisha kuwa visababishi vya upofu katika maeneo hayo ni
muhimu zaidi kiidadi. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment