BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS AMWANGA UGALI WA MAWAZIRI WANEE, NI WALE WALIOGUSWA NA OPEREHENI YA TOKOMEZA UJANGILI.

Sizitaki Mbichi Hizi: Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki alikuwa wa kwanza kujiengua, alipotangaza nia yake ya kujiuzulu kwenye hotuba aliyotoa muda mfupi kabla Waziri Mkuu hajazungumza. PICHA | EMMANUEL HERMAN 


RAIS Jakaya Kikwete, ametengua uteuzi wa Mawaziri wanne, akikubaliana na kilio cha Wabunge cha kuwawajibisha mawaziri hao kutokana na makovu mabaya yaliyotokana na Operesheni Tokomeza. 




Operesheni hjiyo ilikuwa na lengo la kukabiliana na wimbi kubwa la ujangili. Operesheni hiyo inadaiwa kusababisha vitendo vya kikatili, unyanyasaji na mauaji dhidi ya wananchi na wanyama. 



Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dk David Mathayo na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki ambaye alitangaza kujiuzulu Bungeni. 



Akizungumza bungeni jana jioni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema Rais Kikwete alichukua uamuzi huo, baada ya kuwasiliana naye na kumueleza msingi wa tukio hilo na uamuzi wa wabunge ambao Rais naye aliuridhia. 



“Baada ya kulisikia jambo hili na kwa uzito wake nilimueleza Rais Kikwete, naye ameungana na wabunge kwa sehemu kubwa na kusisitiza angependa matokeo ya tume itakayoundwa isichukue muda mrefu na watendaji wote bila kujali ni akina nani nao lazima wawajibike,” alisema Pinda. 



Kutokana na kauli yake hiyo alitengua uteuzi wa mawaziri hao wote wanne , ingawa alisisitiza kuwa hakuna hata mmoja aliyehusika moja kwa moja na matendo hayo lakini kwa kuwa wao ni wasimamizi lazima wawajibike. 



“Mawaziri hawa hawakutenda kitu chochote lakini tatizo walikabidhiwa sekta hiyo kusimamia, na suluhu ya kisiasa ni wao kuachia ngazi,” alisema. 



Alisema kilichowalisilishwa bungeni hapo na Kamati maalum ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na picha zilizowasilishwa na kuonyeshwa bungeni hapo zinasikitisha. 



Alisema operesheni hiyo ilisimamiwa na wizara tatu, ya ulinzi, mambo ya ndani na maliasili. 



“Nimesikiliza kwa makini kuna vitendo vimeonyeshwa havikubaliki, mauaji, ubakaji, iko mifugo imeuawa, haya yote hayakubaliki, naelewa nia nzuri ya operesheni hii, ilikuwa ni dhamira ya Serikali tuwakamate majangili ila tatizo ni namna operesheni hiyo ilivyotekelezwa na kusimamiwa,” alisema. 



Alisema ni lazima wizara zione jambo hilo ni sehemu ya usimamizi na sehemu ya jukumu lao. 



Akielezea zaidi alisema: “Ndio maana kabla ya kuja humu ndani niliwaita mawaziri wote wanne kuwataka wenyewe waone uzito wa hili na wao wenyewe wabebe dhamana,”alisema katika mazungumzo hayo mawaziri wote, walikubali kuwa jambo hilo ni zito na linastahili kupewa uzito kwa upande wa Serikali. 



Alisema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa vyombo vilivyohusika viko chini yao, Mathayo amejieleza kwa maana ya kuwa yeye katika operesheni tokomeza hakuwa na chombo chochote kilichosimamia zoezi hili. 



Waziri Mkuu Pinda alisema aliwahakikishia watanzania kuwa suala hilo halitoishia hapo na kwamba hatua za kiutawala, zitachukuliwa, kwa kuwa kuna uvunjifu wa sheria.



“Tutaunda tume itakayojumuisha watu wenye kaliba nzuri, ili tupate wale wote waliohusika, naomba muda wa mwezi mmoja na tutawasilisha ripoti hiyo bungeni,” alisema. 



Awali kabla ya kuzungumza Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Khamis Kagasheki, aliamua kujiuzulu mwenyewe kutokana yaliyojiri kwenye ripoti hiyo. 



“Mimi ni mtu mzima, nimesikia hisia nyingi sana zilizotolewa na wabunge, wengine wamesema mimi ni lazima nichukue uamuzi wa kisiasa, nasema Rais Dk Kikwete, aliponiteua katika wadhifa huu ilikuwa ni kwa furaha yake,” alisema. 



Alisisitiza kuwa “Naamini anaaamini kuwa ningeweza kufanya kazi hii kadri nilivyoweza, kutokana na operesheni hii yametokea yaliyotokea, na uhakika utaratibu utafanywa ili kujua hali halisia, naomba nijiuluzu,” alisisitiza nitachukua hatua inayostahiki ili kufuata utaratibu. 



Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo, alitumia fursa hiyo kujitetea huku akidai kuwa taarifa hiyo haijamgusa mahali popote na tuhuma anazotupiwa hazina uhusiano na wizara yake. 



“Ripoti nzima sikuonekana ila nimeonakana kwenye mistari ya mwisho kwamba nijipime hakuna tuhuma zozote dhidi yangu. 



Sikuitwa sehemu yeyote na kamati hii. Watu wanasema mpare anauza ng’ombe kwa kesi ya kuku, hiyo ni kwa sababu anataka haki, yaliyosemwa yote ipo mipango ya kuyatekeleza. Tatizo kubwa lipo katika ardhi, wizara yagu haihusiki na kupima ardhi,”. “Katika hili naonewa, nawashukuru sana, jambo lingine tatizo lililopo ni uhaba wa fedha mbayo wizara inapatiwa ndio maana mambo mengine yanashindwa kutekelezeka,” alisema. 


Naye Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema, aliunga mkono kamati hiyo na kuahidi kuwa itaundwa Tume ya Uchunguzi ya kimahakama. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na Tume ya aina hiyo yenye lengo la kumaliza mzizi wa fitina. 



Awali Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema, alianza kutoa hoja kwa kuunga mkono, akisema ni jambo hili linafungua milinago ya kuchukua hatua za kikatiba. 



Jaji Werema alisema kwamba Msingi wa hatua hiyo ni taarifa ya kamati kuhusu operesheni hiyo ambayo ilianza kwa jambo jema la kutokomeza ujangili. 



Jaji Werema pia alisema kwamba Operesheni za aina hii zimeshawahi kufanyika na kutumia JWTZ, akisisitiza kuwa jeshi hilo si la vvita tu bali la ulinzi na usalama. 



Aidha alifafanua zaidi kwamba kwa mujibu wa ibara ya 147 na 148 amiri jeshi anaweza kuamuru jeshi hilo kutumika na kusaidia raia. Hata hivyo alisema kwamba katika operesheni za aina hiyo inawezekana kikafanya kitu cha pamoja kwa ajili ya kusaidiana, kutumiwa na mahakimu ili utaratibu wa utoaji haki ufanyike. 



“Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya kamati kuna mambo ya uhalifu, yako mengine yanahitaji uchunguzi wa kina na wa kimahakama, ninashauri na hili halihitaji azimio la Bunge, nakubaliana na wabunge kuwa Serikali ichukue hatua.”Alisema jaji Werema. 



Alisema:”Nashauri kwamba wakati muafaka ukifika, iko sababu ya msingi ya kutumia sheria yetu ya uchunguzi wa kimahakama. Ambapo Rais atashauriwa aunde tume ya uchunguzi ambayo ama itaongozwa na Jaji wa mahakama Kuu au ya rufani.” 



Jaji Werema alisema kwamba anakubaliana na waziri Kivuli Tundu Lissu juu ya umuhimu wa kulinda Katiba yetu ambapo watendaji wanapaswa kufanya vitu kisheria. “ Tunahitaji kurudi nyuma na kuangalia mfumo wetu wa elimu na nidhamu.” Alisema Werema na kuongeza kuwa tatizo la kufanya vitu na kudharau sheria limekomaa na hivyo serikali lazima ichukue hatua. HABARILEO.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: