MAWAZIRI WANEE WA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE WAKANYAGA KAA LA MOTO.
WABUNGE wameungana bila kujali itikadi za vyama vyao na kutaka kwa pamoja Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mawaziri watatu wanaowajibika na Operesheni Tokomeza Ujangili, kuwajibika, kutokana na operesheni hiyo kudaiwa kusababisha vitendo vya kikatili na mauaji kwa wananchi.
Mawaziri hao watatu wanaolengwa ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Aidha, wabunge hao wengi walitaka Kamati Maalumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Mazingira, iwataje wanasiasa wanaodaiwa kuhujumu operesheni kwa majina ambao pia wanatajwa kuwa katika mtandao wa ujangili.
Kamati hiyo iliwasilisha bungeni hapo, kupitia Mwenyekiti wake, James Lembeli, taarifa ya uchunguzi kuhusu tathmini ya matatizo yaliyotokana na Operesheni Tokomeza, ambapo pamoja na mambo mengine, ilibainisha vitendo vya kikatili vilivyofanywa na watendaji wa umma, ikiwemo tuhuma za baadhi ya wanasiasa kushiriki kwenye vitendo vya ujangili.
“Rais Jakaya Kikwete, ni lazima amwondoe Waziri Mkuu, la sivyo nitakuwa mtu wa kwanza kuwasilisha maoni ya kura ya kutokuwa na imani naye bungeni,” alisema Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola.
Lugola, katika mchango wake kuhusu mjadala huo, alisema anashangaa kwa nini zilitumika operesheni za kijeshi dhidi ya wananchi wanaoishi katika maeneo ya hifadhi na wafugaji.
“Siamini kabisa kwa nini operesheni hii imehusisha Jeshi, ni kama vile lengo lake si kupambana na majangili bali kupambana na wafugaji,” alisema.
Maoni hayo ya Lugola, yaliungwa mkono na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Mbunge wa Longido, Lekule Laizer (CCM).
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM) alitaka maofisa wote waliotajwa kuhusika katika taarifa hiyo ya Kamati wachukuliwe hatua, kwa kuwa pamoja na watu wengi kupoteza maisha, wengi wamebaki vilema na masikini kwa kupoteza mifugo yao.
“Ni lazima sheria ifuate mkondo wake, hatuwezi kuruhusu watu wachache ndani ya Serikali kuacha watu wauawe na kisha wasiadhibiwe,” alisema Nkumba.
Nkumba ndiye mbunge aliyetoa hoja binafsi katika mkutano wa Bunge la 13, ya kutaka operesheni hiyo isitishwe na kuundwa kamati maalumu ya kuchunguza matukio ya udhalilishaji na unyanyasaji yanayofanyika kupitia operesheni hiyo.
Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah (CCM), ambaye alikuwa ni mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo maalumu, alisema viongozi wote watatu waliokuwa wakisimamia operesheni hiyo lazima waadhibiwe.
Awali baada ya kuwasilishwa kwa taarifa hiyo, hali ya amani bungeni humo ilivurugika na wabunge kutishia kususa mkutano huo, baada ya kubaini kuwa muda wa kujadili taarifa hiyo ni mchache nusu siku na kutaka ijadiliwe angalau kwa siku mbili.
Mbunge Laizer, alisema ni bora mjadala huo ufanyike kwa siku mbili kutokana na ukubwa wa tatizo lililoainishwa na kamati na ikiwezekana hata wabunge wafanye mjadala huo bila posho.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Lugola, Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina (CCM), Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), na Zitto ambao wote walitaka muda wa mjadala uongezwe.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliahirisha kwa muda Bunge hilo na kuitisha Kamati ya Uongozi ya Bunge ili iweze kupanga ratiba ya Bunge hilo.
Baada ya Kamati hiyo kukutana, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, alitangaza rasmi kuwa muda wa mjadala wa Bunge umeongezwa kutoka saa nne hadi saa saba na kuwa saa nne hadi saa nane na jioni ambako ilizoeleka kuwa bunge hilo linaanza saa 11 jioni hadi saa mbili kasoro usiku jana lilianza saa 10 jioni hadi saa tatu usiku.
Wakati huo huo, Kamati Maalumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imependekeza baadhi ya watendaji wakuu akiwamo Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa wawajibishwe kutokana na kuchangia kuhujumu Operesheni hiyo.
Operesheni hiyo kwa mujibu wa Lembeli alisema Kamati ilikutana na watu mbalimbali wakiwamo wabunge, na kufanya ziara maeneo ilikofanyika operesheni hiyo, na ilimhoji Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi.
Alisema kamati hiyo kwanza ilibaini kuwa washiriki wa Operesheni hiyo, walikuwa ni wanajeshi 885 kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), askari 480 kutoka Jeshi la Polisi, askari 440 kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU), askari Wanyamapori 383 na kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Wengine ni askari 99 kutoka Wakala wa Huduma za Misitu TFS, askari Wanyamapori 51 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Waendesha Mashitaka 23 na Mahakimu 100.
Alisema baada ya kamati hiyo kukutana na waathirika, mawaziri, washiriki na kutembelea maeneo hayo ilibaini kuwa katika utekelezaji wa operesheni hiyo, kulikuwa na changamoto mbalimbali vikiwamo vifo vya askari sita na wananchi 13.
Alisema pia kamati hiyo ilibaini kuwepo kwa mamluki miongoni wa washiriki wa operesheni hiyo akitolea mfano kukamatwa kwa polisi na askari wanyamapori wakisindikiza gari lenye meno ya tembo, kwa kutumia gari la Serikali ikiwa ni pamoja vyombo vya habari kutumika kuvuruga operesheni kwa kueneza propaganda.
Alisema pia katika hali ya kutisha, Kamati ilibaini baadhi ya wananchi wakiwemo viongozi, madiwani na wenyeviti wa vijiji na vitongoji na watumishi wa Serikali walikamatwa na kudhalilishwa mbele ya wananchi wanaowaongoza.
Alisema pia Kamati ilibaini kuwa baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walidai kudhalilishwa mbele ya wanafamilia kwa kupewa adhabu wakiwa uchi na wanawake kushikwa sehemu za siri bila ridhaa yao. Aidha, alisema baadhi ya akina mama walidai kubakwa na kulawitiwa. HABARILEO.
0 comments:
Post a Comment