RAIS Jakaya Kikwete, anaweza kutangaza mabadiliko katika baraza lake la mawaziri wakati wowote kuanzia sasa.
Hatua hiyo inafuatia uteuzi wa mawaziri watatu kutenguliwa, mmoja kujiuzulu na mwingine kufariki dunia.
Desemba 20, mwaka jana, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliwasilisha bungeni taarifa ya uchunguzi kuhusiana na athari zilizojitokeza katika Operesheni Tomokeza Ujangili iliyositishwa na serikali wakati wa Mkutano wa 13 wa Bunge kufuatilia malalamiko ya wananchi, wabunge na wadau.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli, alisema uchunguzi wao ulibaini kuwa operesheni hiyo iliendeshwa bila kufuata taratibu na matokeo yake kusababisha mateso kwa raia, vifo na upotevu wa mali hususani mifugo.
Baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa, wabunge walichachamaa na kushinikiza mawaziri ambao wizara zao zilihusika katika utekelezaji wa operesheni hiyo wawajibike kisiasa au wawajibishwe.
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, aliamua kujiuzulu wakati mjadala ukiendelea na siku hiyo baadaye Rais Kikwete, alikubaliana na mapendekezo ya wabunge kwa kutengua uteuzi wa mawaziri watatu, Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi); Mathayo David Mathayo (Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT).
Januari Mosi, mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini na kuzikwa kijijini kwake Magunga, Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa Jumatatu wiki hii.
Licha ya nafasi hizo tano kuwa wazi, pia kumekuwapo na shinikizo la kutaka mawaziri kadhaa waondolewe kutokana na utendaji wao kulalamikiwa kuwa haufikii viwango na kwamba ni mizigo.
Mawaziri hao walilalamikiwa na wananchi kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, wakati wa ziara yake ya wiki kadhaa kuanzia Novemba, mwaka jana katika mikoa ya Njombe, Mbeya na Ruvuma.
Miongoni mwa mawaziri waliolalamikiwa ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima.
Kutokana na malalamiko hayo, Kinana aliahidi kuwa angewasilisha taarifa hizo katika kikao cha Kamati Kuu ili mawaziri hao waitwe na kujieleza.
Aidha, wakati wa mkutano wa 14 wa Bunge, wakati wa kujadiliwa kwa ripoti ya mwaka ya hoja za kamati kuhusu hesabu zilizokaguliwa na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2012, baadhi ya wabunge walimshambulia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, kwa kushindwa kudhibiti wizi wa fedha katika halmashauri pamoja na kuwalinda watendaji wanaovurunda kazi kwa kuwahamishia sehemu nyingine.
Wakati mkutano huo wa Bunge ukiendelea, Kamati Kuu ilikutana mjini Dodoma na kuwahoji baadhi ya mawaziri hao, lakini hatma yao inasubiri uamuzi wa Rais Kikwete, ambao wengi wanaamini kuwa anaweza kuwaondoa katika baraza lake.
Habari zinaeleza kuwa huenda wakati wowote mwishoni mwa wiki hii au mapema wiki ijayo, Rais Kikwete atatangaza mabadiliko katika baraza lake kwa kujaza nafasi tano ambazo ziko wazi pamoja na kuwaondoa mawaziri wanaolalamikiwa kwa utendaji mbovu unaosababisha CCM ilalamikiwe na wananchi.
Mmoja wa maofisa waandamizi serikalini, aliliambia gazeti hili kuwa wakati wowote katika mwisho wa wiki hii au mapema wiki ijayo, Rais atatangaza mabadiliko ya mawaziri ili kuruhusu shughuli za serikali ziende kama inavyotakiwa.
Alisema Rais atakuwa amepata muda wa kutosha kushauriana na washauri wake wakiwamo waliokuwa wamekwenda katika mapumziko ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Miongoni mwa waliokuwa katika mapumziko ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye ni mshauri muhimu wa Rais katika uteuzi wa mawaziri akiwa ndiye kiongozi wa shughuli za serikali bungeni na kwa kuzingatia kuwa mawaziri wanatokana na wabunge.
KAULI YA IKULU
NIPASHE lilipomuuliza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, jana kuhusiana na mchakato wa kutangaza mabadiliko ya mawaziri, alisema Baraza hilo litatangazwa Rais atakapokuwa tayari.
Balozi Sefue alisema kwa ufupi: “Mheshimiwa Rais akiwa tayari atatangaza, hatuwezi kulipangia muda.”
Mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri yatakuwa ya nne kufanywa na Rais Kikwete tangu alipoingia madarakani mwaka 2005.
MABADILIKO YA KWANZA
Rais Kikwete aliunda upya baraza lake la mawaziri Februari, 2008 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na kashfa ya kuipa Kampuni ya Richmond Development Company LLC ya Houston, Texas nchini Marekani zabuni ya kufua umeme wa dharura wa megawati 100 kwa upendeleo.
Lowassa alijiuzulu sambamba na waliokuwa mawaziri wawili Dk. Ibrahim Msabaha (Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Nazir Karamagi (Nishati na Madini).
Karamagi na Dk. Msabaha, wote walikuwa wameiongoza wizara ya Nishati na madini kwa nyakati tofauti.
Hatua ya kujiuzulu kwa Lowassa na wenzake, ilitokana na ripoti ya Kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, iliyowasilishwa bungeni baada ya kukamilisha kazi ya uchunguzi kujiridhisha kuhusiana na uhalali wa kampuni hiyo ndani na nje ya nchi.
Kamati hiyo pia iliundwa na Stella Manyanya (Viti Maalum), Mohamed Mnyaa (Mkanyageni-CUF), aliyekuwa Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM) na Herbert Mntangi (Muheza-CCM), ambao wal;ibaini kuwa kampuni hiyo ilikuwa feki.
MABADILIKO YA PILI
Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya pili katika baraza lake Mei, 2008 baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge.
Chenge alichukua uamuzi huo baada ya kubainika kuwa anamiliki akaunti iliyokuwa na Dola za Marekani milioni moja (wakati huo Sh. bilioni 1.2) katika benki moja katika kisiwa New Jersey, nchini Uingereza.
Akaunti hiyo ilibainiwa na wapelelezi wa Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Ufisadi ya Uingereza (SFO) na kuhusishwa na fedha za kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi ambayo Tanzania iliinunua kutoka Uingereza wakati huo Chenge akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mapema miaka ya 2000. Ilidaiwa kuwa huenda Chenge alipata fedha hizo kutokana na rada hiyo kununuliwa kwa bei ya juu kuliko thamani yake.
Baada ya Chenge kujiuzulu, nafasi yake ilichukuliwa na Mbunge wa Bagamoyo, Dk. Kawambwa huku Rais Kikwete pia akibadilisha mawaziri kadhaa.
MABADILIKO YA TATU
Mei 2012, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya tatu katika baraza lake la mawaziri baada ya kuwaondoa mawaziri sita kufuatia ripoti
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG), na kubaini mawaziri hao kwa nyakati tofauti walikiuka maadili ya utumishi wa umma na kushindwa kuwajibika kisiasa kusimamia mali za umma.
Katika mabadiliko hayo, waliondolewa ni wa Mustafa Mkulo (Fedha); William Ngeleja (Nishati na Madini); Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii); Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii); Omari Nundu (Uchukuzi) na Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara).
Wengine waliotimuliwa ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Athumani Mfutakamba na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Lucy Nkya. Dk. Mponda na Dk. Nkya waliponzwa na mgomo wa madaktari.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment