MAITI YA KICHANGA YAZUA BALAA, NDUGU WATWANGANA MAKONDE MKOANI KATAVI.
Gari la kubeba maiti.
MTAFARUKU mkubwa umetokea msibani katika Mtaa wa Kawajense Madukani, Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi baada ya ndugu wa pande mbili kugombania kuuzika mwili wa kichanga, Junia Bacho mwenye mwaka mmoja na nusu aliyefariki juzi, katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda.
Tukio hilo ambalo lilivuta hisia za watu wengi, lilitokea juzi katika mtaa huo baada ya mtoto huyo kufariki akiwa amelazwa katika hospitali ya wilaya ambako alikuwa akiuguzwa na shangazi yake, Evelyne Komba.
Baada ya mtoto huyo kufariki, kulitokea kutoelewana baina ya ndugu wa baba wa mtoto, Joseph Bacho na ndugu wa mama aitwaye Anna Kizo.
Upande wa ndugu wa baba ulidai ndio wenye haki na jukumu la kuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka nyumbani kwa mama mzazi wa baba wa marehemu aitwaye Ted Francis anayeishi katika Mtaa wa Madukani mjini hapa.
Ndugu wa mama wa marehemu nao walidai hawako tayari kuona msiba huo unakwenda kwa baba wa mtoto kwani hakuwa na uhalali wa kuuchukua kwa kile walichodai kwamba alikuwa hajatoa mahari na hivyo wao hawamtambui.
Hali hiyo iliwafanya ndugu wa pande hizo mbili kuanza kutupiana shutuma ambapo wale wa baba mtoto walidai mama yake alishindwa kumuhudumia wakati akiwa mgonjwa, na kwamba muda wote baba alipokuwa akifika nyumbani, alikuwa hamrusu kumwona mwanae.
Kwamba mtoto huyo alipochukuliwa na baba yake Juni 18 kwa ajili ya kushughulikia matibabu ya ugonjwa wake wa ukosefu wa lishe (kwashakoo), mama hakuwahi kufika kumwangalia, hali iliyolazimu aangaliwe na shangazi na bibi yake.
Pamoja na maelezo hayo, ndugu wa upende wa mama wa marehemu waliendelea na msimamo wao wa msiba kuwa kwao, ingawa baada ya mabishano ya muda mrefu pande hizo ziliamua kuuacha mwili hospitali.
Baada ya kurudi nyumbani kila upande uliweka msiba, hali iliyofanya kuwepo na misiba sehemu mbili katika mtaa mmoja.
Siku iliyofuata, wazee wa mtaa waliingilia kati kwa kufanya kikao na pande hizo zilizokuwa zikivutana, kisha kufikia uamuzi wa kupeleka msiba huo nyumbani kwa baba wa marehemu.
Kufutia uamuzi huo, shangazi wa marehemu, Evelyne aliongoza ndugu kwenda kuuchukua mwili wa marehemu tayari kwa ajili ya mazishi yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kwenye makaburi ya Kawanjense Msufini.
Hata hivyo, wakati shughuli za mazishi zikitarajia kuanza, ndugu wa baba wa marehemu walipata taarifa kuwa kaburi walilochimba kwa ajili ya kuzikia mwili wa mtoto huyo limefukiwa.
Ndugu hao, walipofika makaburini walikuta mama mkubwa wa marehemu aitwaye Jane Kiza na wenzake wakiwa wanamalizia kulifukia kaburi hilo.
Jane na kundi lake walipoulizwa kwanini wamefukia kaburi hilo, walianza kufoka na kisha kundi la ndugu wa mama wa marehemu walitokea na kuanza kuwashambulia kwa kipigo ndugu wa baba.
Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiongozwa na SSG Bahati walifika eneo hilo na kutuliza ghasia kisha walielekea msibani na kuamuru mwili huo urudishwe kuhifadhiwa hospitali hadi hapo ufumbuzi utakapokuwa umepatikana.TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment