BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SERIKALI YAJIBEBESHA "MADUDU" YA IPTL.

http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/06/eskrow.jpg
DANADANA zinazopigwa na viongozi wakuu wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika kutafuta ukweli wa sakata la uuzwaji wa hisa za kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwenda kwa Kampuni ya PAP, zimeibua mzozo mkali Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.

Matamshi makali ya kuwashambulia watoa tuhuma za uchotwaji wa sh. bilioni 200 za akaunti ya Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yaliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi, yanatafsiriwa kama hatua ya serikali kujibebesha lawama ili kuwalinda watuhumiwa.

Wanaotuhumiwa kwa kashfa hiyo ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake Maswi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Benno Ndullu.

Baadhi ya wabunge wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kuzima hoja ya kutaka kuunda Kamati Teule ya Bunge na kulipeleka sakata hilo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Inaelezwa kuwa Serikali ya CCM inahofia uchunguzi wa sakata hilo kuwa unaweza kusababisha kutikisika kwa utawala, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na ule mkuu utakaofanyika mwakani.

Hoja kubwa wanayoijenga ni kuwa tume huru ya kuchunguza jambo hilo inaweza kuzaa makovu kama yale yaliyotokea mwaka 2008 ilipotokea kashfa ya Richmond iliyozusha makundi hasimu ndani ya CCM, yaliyosababisha matokeo mabaya kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Habari zinasema kuwa msimamo wa kukataa uundwaji wa Kamati Teule uliwekwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenye kikao cha ndani cha wabunge wa chama hicho kilichofanyika wakati wa mkutano wa Bunge la Bajeti lililomalizika jana.

Msimamo huo ndio uliochangia Spika wa Bunge, Anne Makinda, kukataa hoja ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) kuundwa kwa kamati hiyo na badala yake akaagiza suala hilo lipelekwe kwa CAG na TAKUKURU.

Spika Makinda, pia aliagiza Kafulila na wabunge wengine wenye ushahidi wa sakata hilo waupeleke kwenye vyombo vinavyoshughulikia jambo hilo.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa mvutano uliozuka siku chache zilizopita bungeni kati ya Jaji Werema na Kafulila, umefungua upya sakata hilo.

Werema alimuita Kafulila tumbili huku mbunge huyo akimuita mwanasheria huyo mwizi wa IPTL ambapo hitimisho la mzozo huo lilikuwa kwa Werema kumtishia maisha mbunge huyo.

Kafulila, Mnyika kumng’oa Pinda

Kutokana na sakata hilo kutopatiwa uzito unaostahili, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) na Kafulila wanapanga kuanza kukusanya saini za wabunge ili wamng’oe madarakani Waziri Mkuu, Pinda kwa kushindwa kusimamia wizara zilizo chini yake.

Wakizungumza na Tanzania Daima Jumapili, wabunge hao walisema jaribio hilo ni gumu kwa kuwa litahitaji kuungwa mkono na wabunge wengi wa CCM ambao chama chao hakitaki jambo hilo lishughulikiwe kikamilifu.

Hata hivyo, walisema wataendelea na mpango huo kwa kuwa historia inaonyesha kuwa ufisadi unaofichuliwa na wapinzani licha ya kupata wakati mgumu, lakini baadae hufanyiwa kazi.

Werema, Maswi wakaliwa kooni

Kufuatia kauli za matusi na vitisho za Jaji Werema na Maswi kwa wabunge Kabwe, Zitto (CHADEMA) na Kafulila (NCCR-Mageuzi) baada ya kulivalia njuga suala hilo, wachambuzi wa kisiasa wamesema kuwa serikali inapaswa kujitafakari upya kuhusu maadili ya viongozi wa umma.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema kauli hizo za viongozi wa serikali zinadhihirisha namna ilivyokosa uwajibikaji.

Alisema viongozi hao walipaswa wafanyie kazi taarifa walizopewa na kutoka hadharani na majibu ya kueleweka badala ya kutoa porojo zisizo na msingi.

“Mnakumbuka mwaka 2010 nilitoa tuhuma ya kuwepo kwa masanduku ya kura kabla ya wakati kule Tunduma… viongozi wa serikali tunaowalipa kodi zetu badala ya kufanyia kazi wakaja hadharani na madai kuwa mimi ni muongo na wengine wakaamua kututukana kabisa,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, wajibu wa serikali ni kutafuta taarifa za kweli na kuzitoa hadharani badala ya jukumu hilo kuachwa kwa mtu binafsi aliyeeleza kuwa anaweza kuwa na nusu ya ukweli unaopaswa kuanikwa na serikali kupitia vyombo vyake vya kichunguzi.

Zitto ambaye juzi alishambuliwa kwa tuhuma nzito na Maswi akiitwa mwizi na mshenzi, alisema viongozi hao wanachukulia madai hayo kama jambo la mzaha pasipo kujua kuwa litaondoka na watu.

Alisema badala ya Maswi kuweweseka, anapaswa ajibu hoja dhidi ya tuhuma zinazowakabili na kama ana madai mapya anapaswa kuyapeleka katika mamlaka husika yafanyiwe kazi.

“Nimemsikia kupitia video Maswi anasema vipeperushi vinasambazwa, napenda kuwaambia Watanzania kinachosambazwa ni barua ya Maswi kwenda kwa Gavana wa Benki Kuu kwa ajili ya kutolea fedha, pia ajibu tuhuma zinazomkabili na kama ana hoja mpya ya kutuhusisha na wizi aende maeneo husika tuchunguzwe,” alisema Zitto.

Aliongeza kuwa fedha zilizochotwa ni za umma na kwamba hata kama serikali ya sasa itashindwa kuwashughulikia watu waliochota fedha hizo, hawatasalimika katika serikali ijayo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alisema nchi imeingiliwa na nguvu kubwa ya mitaji kutoka nje na kwamba mabeberu hao wanawatumia watu wa ndani ya nchi kuingia katika sekta muhimu za kiuchumi.

Alisema wanaotuhumiwa katika sakata hilo hawataweza kuwa na majibu ya kueleweka kwa kuwa mabeberu wamejikita kwa wazawa na kwamba hali hiyo inaweza kuifikisha nchi katika hatua iliyopo Nigeria kwa sasa.

Aliongeza kuwa kukosekana kwa majibu ya msingi kutoka kwa mamlaka husika kunadhihirisha uwepo wa tatizo katika sakata zima na kwamba wananchi watakaposhinikiza kupata majibu ya kueleweka hali itakuwa mbaya zaidi.

“Badala ya Watanzania kujadili watu wamesema nini, wanapaswa warejee kashfa za Buzwagi na EPA na namna wahusika walivyojitetea awali na matokeo yake baadaye yakawaweka katika mazingira ya namna gani.

“Ni vizuri tukajadili sera inayoendesha uchumi wetu na nguvu zinazotumika kwani hali hii haina tofauti na kashfa nyingine zilizotokea katika wizara hii hii, kinachonitisha mimi ni mambo kujirudia rudia kila wakati na katika sekta ile ile,” alisema Bashiru.TANZANIADAIMA.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: