ETI WAZIRI MKUU WA AWAMU YA TATU ENZI ZA BENJAMIN MKAPA AAMBIWA ANAPOTEZA MUDA JAPO ANAZUNGUMZA KWELI.
ALIYEKUWA Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, ameambiwa kuwa mihadhara anayoifanya ya kijamii inayohusu kupiga vita rushwa, anapoteza muda kwa kuwa hakuna anayemsikiliza ingawa anachozungumza kina ukweli.
Akizungumza katika kipindi cha Medani ya Siasa cha Star Tv kilichorushwa jana, Sumaye alisema ameambiwa hayo na rafiki zake.
Pamoja na kukatishwa tamaa, Sumaye alisema hataacha kukemea rushwa na hasa katika siasa kwa kuwa ikiachwa itaua Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuangamiza Taifa.
Alisema mihadhara yake, haihusu uchaguzi mkuu ujao wa 2015, kwa kuwa hata uchaguzi huo ukifanyika 2020, hataacha mihadhara hiyo kwa kuwa lengo ni kutoa elimu zaidi na si kupata sifa au fedha.
“Nilianza kupambana na rushwa tangu nikiwa madarakani…utakumbuka nilianzisha kura ya siri ya kuwapata wala rushwa. Sasa hata kama nitagombea urais mwakani mapambano ndio yatazidi na hata nisipogombea mapambano haya yataendelea,” alisema Sumaye ambaye aliweka wazi kuwa wakati ukifika atagombea urais.
Alisema rushwa katika siasa haijaanza wakati huu, kwani ilikuwepo hata wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambako wakati huo wagombea walikuwa wakitoa vitu ikiwemo chai.
Kwa mujibu wa Sumaye, Mwalimu Nyerere alikuwa akihamasisha kwa wapiga kura kuwa wasiwape kura waliowapa chai kwa kuwa wamepoteza maadili na wapiga kura walimuelewa na kweli waliotoa chai walikosa uongozi.
Hata hivyo, tofauti na wakati huo, kwa sasa kwa mujibu wa Sumaye wagombea wanatoa fedha zaidi na si katika urais tu, bali hata udiwani na ubunge na hakuna anayeweza kupinga kuwa ipo.
Alisema mbaya zaidi, kama uongozi unatumia rushwa kuweka watu ambao wananchi hawawataki na siku wakikataa viongozi hao na kusema liwalo na liwe, hata nchi inaweza kuanguka, na kwa kuwa hataki hilo litokee, hataacha kupambana na rushwa.
Sumaye alisema Tanzania ya sasa si ya zamani na kutoa mfano kwa nini gari la Polisi limegonga dereva wa bodaboda, wananchi wakachoma nyumba ya mbunge wakati mbunge si askari wa Usalama Barabarani.
Alionya kuwa hiyo ni dalili kuwa jamii ina hasira ya kuachwa na viongozi waliowachagua.HABARILEO.
0 comments:
Post a Comment