MARIO GOETZE ATIBUA NDOTO ZA ARGENTINA KUTWAA KOMBE LA DUNIA MBELE YA LIONEL MESSI WAKATI UJERUMANI IKIILAZA KWA BAO 1-0 FAINALI KOMBE LA DUNIA BRAZI 2014.
mchezaji wa ujerumani Mario Goetze kushoto akipiga mpira uliozaa bao dhidi ya Argentina katika fainali ya kombe la dunia 2014 Maracana Rio de Janeiro Brazil.
Mchezaji kiungo Mario Goetze --Super Mario-- alijiandika kwenye vitabu vya historia pale alipopachika goli la ushindi katika fainali za kombe la dunia, lililoipatia Ujerumani ubingwa wa dunia.
Baada ya kujaribu bila mafanikio kulitwa kombe la kandanda la dunia tangu walipofanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1990, hatimaye ndoto ya vijana wa Jogi (timu ya taifa ya Ujerumani) ilitimia usiku wa Jumapili.
Nyota huyo wa klabu ya Bayern Munich alitegua kitendawili cha ubingwa katika dakika ya 113 na kuinyamanzisha Argentina, huku ndoto ya Lionel Messi ya kufuata nyayo za nguli Diego Maradona ikiishia kwa kushindwa.
Bastian Schweinsteiger akipongezwa na Kansela Angela Merkel huku mchezaji mwenzake Andre Schuerrle akipongezwa na rais Joachim Gauck.
Ushindi mtamu
Ujerumani sasa imeshinda kombe la dunia mara nne, na kulifanya taifa hilo kubwa duniani kuwa nyuma tu ya Brazil yenye rekodi ya ushindi mara tano. Muda wa maamuzi wa fainali hiyo iliyojawa na msisimko na magoli yaliyofungwa kwa ustadi mkubwa ulikuja wakati timu hizo zikinyemelewa na mikwaju ya penati mbele ya watazamaji 74,738 katika uwanja maarufu wa Maracana mjini Rio de Janeiro.
Mchezaji bora wa mechi hiyo ya fainali Goetze aliituliza kifuani krosi ya Andre Schuerrle na bila kufanya ajizi akasukuma mkwaju uliyomduwaza mlinda mlango wa Argentina Sergio Romero, kwa goli la ushindi lililomfanya nahodha Philip Lahm kubeba kombe la dunia.
"Siamini kama sisi ndiyo mabingwa wa dunia. Suala la iwapo tuna mchezaji bora mmoja mmoja halijalishi hata kidogo, kilichomuhimu ni kuwa na timu bora. Tumekuja tukiboresha mchezo wetu wakati wote wa mashindano, na hatukukata tamaa pale mambo yalipotuendea vibaya, tuliendelea kushika njia yetu, na mwishowe tumesimama hapa kama mabingwa wa dunia. Ni hisia isiyoelezeka," alisema nahodha wa timu hiyo Philip Lahm
Baada ya kosa kosa za miaka mingi
Ujerumani ambayo iliinyeshea Brazil mvua ya magoli 7 -1 katika mchezo wa nusu fainali, imekuwa timu ya kwanza ya Ulaya kubeba kombe la dunia katika Amerika ya Kusini.
Walianza kushinda taji hilo mwaka 1954, na kulirudia mwaka 1974 na 1990. Wamekuwa wakilikosakosa ama kwa kutolewa kwenye hatua ya nusu fainali au fainali katika miaka ya hivi karibuni.
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew (Jogi).
Taji hilo ni matokeo ya mbadiliko katika mfumo mzima wa soka ya Ujerumani mwanzoni mwa karne hii, na kutawazwa kwa kizazi cha dhahabu kikiongozwa na Lahm na Bastian Schweinsteiger, kama alivyosema kocha wa Ujerumani Joachim Loew.
"Ninaamini kazi hii ilianza tangu miaka 10 iliyopita na Juergen Klinsman na sisi tulifanya kuendeleza kile alichokianzisha. Tumefanya kila kitu kuhakisha tunafika siku hii. Timu yetu imefanya kazi kubwa sana, imekuwa na hamasa kubwa na hasa katika wiki hii ya mwisho, kila mchezaji amejituma na ndiyo maana tumeweza kushinda fainali hii hapa."
Kina Messi wajilaumu wenyewe
Argentina ambao walishinda taji hilo mwaka 1978 na 1986 kwa kuifunga Ujerumani, wamemaliza wakiwa washindi wa pili kama ilivyokuwa mwaka 1930 na 1990, na nyopta wao Lionel Messi hakucheza kama alivyotarajiwa. Kiungo wa kati Javier Mascherano alisema ni vigumu kueleza, kwani walifanya kila kitu kushinda na walikuwa na nafasi nzuri zaidi.
Messi, Gonzalo Higuain na Rodrigo Palacio walikosa nafasi nzuri cha juu wakati kichwa cha Benedikt Hoewedes kiligonga mwamba kwa upande wa Ujerumani mbele ya maefu ya mashabiki wakiwemo rais wa Ujerumani Joachim Gauck, Kansela Angela Merkel, rais wa Urusi Vladmir Putin na mwenyeji wao rais wa Brazil Dilma Roussef.
Lionel Messi akisononeka baada ya kupulizwa kwa firimbi ya mwisho.
Upinzani usiotarajiwa
Ujerumani ilimiliki mpira kwa sehemu kubwa kama ilivyotarajiwa huku mashabiki wake wakiipa morali ya nyimbo za "ole", lakini Argentina ilionyesha upinzani mkali tofauti na ilivyokuwa katika mchezoi wa nusu fainali na Uholanzi.
Tofauti na robo fainali dhidi ya Ufaransa, na nusu fainali dhidi ya Brazil, Ujerumani ilishindwa kupata goli la mapema dhidi ya safu imara ya ulinzi ya Argentina, ambayo ilikuwa haijafungwa katika michezo mitatu ya mwisho ya mtoano, na ilikuwa na haiba tofauti na Brazil.
Wakiwa wamebeba kombe mikononi mwao, wachezaji wa Ujerumani waliimba pamoja na mashabiki wao, wimbo maarufu wa Am Tag Wie Diesen (Katika siku kama hii) uliyopigwa na bendi ya Ujerumani ya Die Toten Hosen na kuchezwa uwanjani. Ilikuwa ndoto iliyotimia baada ya subira ya miaka mingi.DW
0 comments:
Post a Comment