KAMA UNATAKA KUONA UCHAPAJI KAZI WA SAMWEL SITTA, NI KATIKA BUNGE MAALUMU LA KATIBA DODOMA, AKOMAA KUHAKISHA KATIBA MPYA INAPIGIA KURA OKTOBA 4.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta
Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ‘amekomaa’ kuhakikisha Bunge Maalumu la Katiba linafanya kazi kwa kasi na kukamilisha kila kitu ifikapo tarehe yake ya mwisho, Oktoba 4, ikiwamo kupiga kura za kupitisha Katiba inayopendekezwa kazi ambayo amesema itafanywa hadi nje ya nchi kwa wajumbe watakaokuwa huko.
Sitta alilazimika kutoa matamko mawili kwa nyakati tofauti, mara ya kwanza wakati kikao cha Bunge kilipoanza jana akieleza jinsi Rasimu ya Katiba inayopendekezwa itakavyokamilika ifikapo Septemba 21 na baadaye mchana wakati akiahirisha Bunge alipotangaza mikakati ya kukusanya kura za wajumbe hadi nje ya nchi kuanzia Septemba 26, mwaka huu.
Sitta alitumia fursa hiyo kuwataka wajumbe wa Bunge hilo watakaokuwa nje ya nchi kwa matibabu au sababu nyingine kuacha mawasiliano yao ili waweze kupiga kura wakiwa hukohuko.
Alisema uongozi wa Bunge umeanza kufanya mawasiliano na balozi mbalimbali za Tanzania nje ya nchi ili wawepo watumishi wake watakaokula kiapo cha kisheria ili wasimamie upigaji kura.
Kauli za Sitta zimekuja siku moja baada ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kuweka bayana makubaliano baina ya wajumbe wake na Rais Jakaya Kikwete kuwa hataongeza muda wa uhai wa Bunge hilo, hivyo litakoma Oktoba 4, mwaka huu na hakutakuwa na upigaji wa kura ya maoni kupitisha Katiba hiyo hadi baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2015.
Kauli za Sitta
Akizungumza bungeni kwa kujiamini lakini bila kugusia ratiba ya Bunge hilo iliyokuwa inafikia Oktoba 30, mwaka huu, Sitta alisema ratiba ya Bunge hilo itaendelea kama tangazo la Rais katika Gazeti la Serikali linavyosema.
GN hiyo namba 254 iliyotolewa Agosti Mosi, mwaka huu, ililiongezea Bunge hilo siku 60 ambazo zinamalizika Oktoba 4, mwaka huu baada ya siku 70 za awali kumalizika bila kupatikana katiba inayopendekezwa.
“Kwa taarifa tu na msisitizo, ni kwamba ratiba yetu ya Bunge Maalumu inaendelea kama ilivyopangwa,” alisema Sitta huku akishangilia kwa makofi na wajumbe waliokuwamo.
“Siku 60 za Bunge hili ambazo ni nyongeza ya siku tulizopewa na Rais kwa mujibu wa sheria usipohesabu siku za Jumamosi, Jumapili na sikukuu, zinaishia tarehe 4 Oktoba,” alisema Sitta.
Alisema kikao cha Kamati ya Uongozi kilichoketi juzi, kimeelezwa kuwa Bunge hilo linakwenda vizuri na kwamba Kamati ya Uandishi imejipanga kuwapatia Rasimu ya Katiba Septemba 21, mwaka huu.
“Kwa hiyo ni dhahiri kabisa kwamba lengo tulilopewa na Taifa la kutoa Katiba inayopendekezwa tutalimudu ndani ya wakati,” alisema Sitta ambaye pia ni Mbunge Urambo Mashariki (CCM) na kuongeza:
“Tunaangalia upigaji kura wa wenzetu ambao hawapo kwa sababu mbalimbali nje ya ukumbi huu ukiacha wale waliosusa, wapo wengine wana sababu za kutokuwapo kama vile hospitalini. Kwa hiyo itakapofika wakati wa kupiga kura, tutatoa maelezo ya utaratibu upi utatumika kuweza kuwapata hao kwa sababu akidi inahusu sisi sote ambao tuliteuliwa na Mheshimiwa Rais.”
Kwa mujibu wa tafsiri ya Kanuni za Bunge, “Akidi” maana yake ni idadi ya wajumbe inayoruhusiwa kwa madhumuni ya kuanza kikao cha Bunge Maalumu, Kamati au kufanya uamuzi wa Bunge Maalumu au wa Kamati ya Bunge Maalumu.
Sitta alitangaza pia kuwa mjadala ambao ulianza Jumanne iliyopita ungeendelea hadi keshokutwa, tofauti na tangazo lililotolewa awali na Makamu Mwenyekiti wake, Samia Suluhu Hassan kuwa majadiliano yangechukua siku nane hadi Alhamisi ijayo.
Ili kukamilisha dhamira hiyo, Jumamosi imerudishwa kuwa siku ya kazi, licha ya awali kuondolewa pamoja na siku za Jumapili na sikukuu na kuzifanya za kazi kinyume na utaratibu uliokuwa umezifuta kwa kuzingatia “sheria za kazi.”
Baadaye, kabla ya kusitisha shughuli za Bunge mchana, Sitta alitoa tangazo jingine, akibainisha kuwa upigaji kura utaanza Septemba 26 na utafanyika hata kwa wajumbe watakaokuwa nje ya nchi.
Sitta alikuwa akitoa tangazo hilo kurejea maombi ya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo ambao ni waumini wa Kiislamu wanaopanga kwenda Hija kuanzia Septemba 22, mwaka huu.
Lukuvi ajiweka kando
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alipoulizwa jana iwapo anadhani siku zilizobaki zitatosha kumaliza shughuli za Bunge zilizokuwa zimepangwa hadi mwisho wa Oktoba, alitaka tamko la Sitta ndilo linukuliwe.
“Si umemsikia mwenyekiti mwenyewe leo (jana) asubuhi akiji-commit (akiahidi) kwamba Bunge hili litamaliza kazi yake mpaka kupatikana kwa katiba inayopendekezwa? Unataka nini tena,” alisema.
Alipoulizwa ratiba ya awali inayokoma Oktoba 31, mwaka huu, Lukuvi alisema GN iko wazi juu ya ukomo wa Bunge hilo.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alipoulizwa iwapo Rais ajaye atawajibika kisheria au la kuendeleza mchakato wa Katiba pale ulipoishia alisema:
“Katiba na sheria tuliyonayo haimbani rais ajaye kuendeleza mchakato kwa sababu anaweza kuja na vipaumbele vyake, lakini njia pekee ya kumbana ni kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema.
Hata hivyo, Jaji Werema alisema wataangalia uwezekano wa kuifanyia mabadiliko sheria hiyo ili itamke kuwa upigaji wa kura ya maoni unaahirishwa hadi wakati wa Rais ajaye ili mchakato uendelee kuwa hai.
Hata hivyo, pamoja na Bunge hilo kuongeza kasi ili kukamilisha kazi, taarifa zinasema bado Katiba inayopendekezwa inaweza kukwamishwa na upatikanaji wa theluthi mbili.
“Baadhi ya Kamati hazikupata theluthi mbili, sidhani kama tutapata Katiba inayopendekezwa. Angalia mawaziri na wabunge wenyewe wa CCM hawahudhurii,” ilidokezwa.
Kigogo mmoja wa Serikali alisema juzi kuwa ijapokuwa CCM wanajiaminisha kupata theluthi mbili Bara na kwamba wasiwasi uko Zanzibar lakini hata bara theluthi mbili inaweza isipatikane pia.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment